Rafiki yangu mpendwa,
Kupitia vipindi vya ONGEA NA KOCHA, tumepata masomo ya uchambuzi wa kitabu kinachoitwa THE RULES OF MONEY ambacho kimeandikwa na Richard Templar.
Ni kitabu ambacho kina sheria 107 za fedha ambazo kila mtu anayetaka kupata fedha na kujenga utajiri anapaswa kuzijua na kuzizingatia.
Sheria hizo za fedha zimegawanyika kwenye sehemu kuu tano;
Sehemu ya kwanza ni kufikiri kitajiri.
Kila kitu huwa kinaanzia kwenye fikra. Utajiri au umasikini unaanzia kwenye fikra ambazo tunakuwa nazo. Watu wengi wamekwama kwenye umasikini kwa sababu wanatawaliwa na fikra za kimasikini. Ili kujenga utajiri ni lazima uanze kufikiri kitajiri.
Sehemu hii ina sheria za kufikiri kitajiri ili kuweza kuziona na kuzitumia fursa sahihi za kupata fedha na kujenga utajiri.

Sehemu ya pili ni kujenga utajiri.
Fikra pekee hazitoshi kuleta matokeo, ni lazima hatua zichukuliwe ndiyo fursa hizo ziweze kuleta matokeo. Sehemu ya pili ya kitabu imesheheni sheria za kujenga utajiri. Hii ndiyo sehemu ndefu zaidi kwa sababu mambo ya kufanya ili kujenga utajiri ni mengi.
Kujenga utajiri kunaanza na malengo, ambayo yanawekewa mipango na kisha kutekelezwa. Katika kutekelezwa kwa mipango, maboresho yanapaswa kufanyika ili kuzalisha matokeo bora zaidi.
Sehemu ya tatu ni kukuza utajiri.
Watu wengi huwa wanaanza kuchukua hatua za kujenga utajiri, lakini wengi wanapokutana na vikwazo na changamoto, huwa wanakata tamaa na kuacha. Wachache ambao wanavuka vikwazo na changamoto hizo, huwa wanafika hatua ya kupata matokeo mazuri. Wanakuwa wamejenga utajiri kiasi.
Utajiri huo kiasi huwa unakuwa kikwazo kwa wengi kujenga utajiri mkubwa zaidi. Kwani wanashindwa kukuza zaidi utajiri wao na kuishia kudumaa au hata kushuka kabisa. Haitoshi tu kujenga utajiri, unapaswa pia kuweza kuukuza zaidi.
Sehemu ya nne ni kulinda utajiri.
Unapokuwa masikini, watu wengi hawakuzingatii, wanakupuuza kwa sababu unakuwa huna madhara kwao na hawana cha kunufaika nacho kwako. Lakini unapojenga utajiri, watu wanaanza kukuwinda. Wapo ambao wanakuwa wanataka kujinufaisha kupitia utajiri wao na wapo wanaokuwa wanataka tu kukuangusha.
Unapaswa kulinda utajiri wako ulioujenga kwa taabu, kwa sababu ukishindwa kufanya hivyo, utatenganishwa nao haraka sana. Tumekuwa tunaona watu ambao wanapata utajiri lakini hawadumu nao, sababu kubwa ikiwa ni kushindwa kuulinda.
Sehemu ya tano ni kugawa utajiri.
Kitu kimoja kuhusu utajiri ni kwamba hutaondoka nao, utakapokufa, utaacha kila kitu. Kwa bahati mbaya sana, ukifa hujagawa utajiri wako vizuri, siyo tu utapotea hovyo, bali pia utaleta mafarakano kwa wale unaowaacha.
Hivyo jambo la busara ni pale unapojenga utajiri ni kuhakikisha unaugawa vizuri kabla hujaondoka hapa duniani. Hiyo inaanza na kutawanya utajiri wako kwa usahihi kwa watu wa karibu na kutoa misaada. Na pia inakutaka uandike wosia wa jinsi utajiri unaokuwa umebaki unavyopaswa kugawanywa. Hilo litaondoa mafarakano kwa wale unaowaacha.
Unaweza kurejea masomo yote ya uchambuzi wa kitabu hicho kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.
Mjadala wa kitabu.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA kilichopo hapa kimekuwa ni cha mjadala wa sheria za fedha na usimamizi wa fedha binafsi. Washiriki wa kipindi wameweza kushirikisha jinsi mambo ya kifedha ambayo wamekuwa wanajifunza na kuyafanyia kazi yameweza kubadili maisha yao na kuyafanya kuwa bora zaidi.
Karibu usikilize kipindi hiki cha mjadala, kisha na wewe ushirikishe mchango wako kwenye sehemu ya maoni hapo chini. Shirikisha uliyojifunza kwenye kitabu hiki na hatua ambazo umekua unachukua kwenye usimamizi wa fedha zako binafsi ili kuondoka kwenye umasikini na kujenga utajiri.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.