Rafiki yangu mpendwa,
Kama umekuwa unatamani sana kufanikiwa ila hujafanikiwa, wewe mwenyewe ndiye wa kulaumiwa kwa kuyakosa mafanikio.
Japo unaweza kuwa na malalamiko yako wa watu na vitu vingine, lakini yote yanaanza na wewe mwenyewe.
Kwenye maisha, kila mtu ana rasilimali kuu nne ambazo zipo ndani ya udhibiti wake na akiweza kuzitumia atajenga mafanikio makubwa sana.
Rasilimali hizo hazitegemei jinsia, umri, elimu, rangi, dini wala kabila. Ni rasilimali ambazo zina usawa kwa watu wote, lakini kwenye matumizi ndipo tofauti kubwa inapoanzia.

Leo nataka nikukumbushe kuhusu rasilimali hizo na jinsi ya kuzitumia vizuri ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Rasilimali ya kwanza ni Uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Kila binadamu aliye hai, ana uwezo mkubwa na wa kipekee kabisa ambao upo ndani yake. Huo ni uwezo ambao akiweza kuutumia anaweza kupata chochote anachotaka kwenye maisha yake.
Kwa bahati mbaya sana, wengi wanapuuza uwezo wao na kuishia kuiga wengine na kufuata mkumbo. Hilo linawapelekea kupata matokeo ya kawaida au hata ya chini kabisa.
Kujenga mafanikio makubwa, tambua una uwezo mkubwa ndani yako na utumie kufanikiwa. Sikiliza sauti yako ya ndani na ifuate hiyo. Usiige wengine wala kufuata mkumbo wa kufanya yale yanayofanywa na wengi.
Rasilimali ya pili ni Vipaji ulivyonavyo.
Kuna vitu ambavyo wewe unaweza kuvifanya vizuri kuliko watu wengine wote. Vitu hivyo ndiyo vimebeba mafanikio makubwa unayoyataka, kwani unaweza kuongeza thamani kubwa kwa wengine kupitia vitu hivyo.
Kwa bahati mbaya sana, watu wengi wamekuwa wanapuuza vipaji vyao na kufanya mambo ambayo ni ya kawaida. Kwa hayo ya kawaida wanayokuwa wanafanya wanashindwa kutoa thamani kubwa kwa wengine na hilo kuwanyima mafanikio makubwa.
Kujenga mafanikio makubwa, tambua vipaji ulivyonavyo kisha vifanyie kazi hivyo kwa uhakika. Kwenye yale mambo ambayo unaweza kuyafanya vizuri kuliko wengine, angalia thamani kubwa unayoweza kuitoa kwa wengine kupitia hayo, kisha itoe hasa. Mwanzo unaweza kufanya hata kama hakuna anayekulipa, lakini baadaye utaweza kulipwa sana kwa sababu ya thamani kubwa utakayokuwa unaitoa.
SOMA; Hizi Rasilimali Zako Tatu Muhimu Zinawindwa Na Wengi, Zilinde Ili Ufanikiwe.
Rasilimali ya tatu ni Muda wako.
Kama kuna demokrasia ya kweli hapa duniani basi ipo kwenye muda tu. Hiyo ni kwa sababu muda ndiyo kitu ambacho kimetolewa kwa usawa kabisa kwa watu wote. Kila mtu ana masaa 24 pekee kwa siku, masikini na matajiri, wote sawa. Hayupo anayeweza kupata hata dakika moja ya ziada kwenye siku yake.
Kama muda wa watu unalingana, lakini matokeo yao yanatofautiana, hiyo ina maana kwamba jinsi wanavyotumia muda wao inatofautiana pia. Wengi wanapoteza muda wao kwenye mambo ambayo hayana tija kabisa kwao. Wanahangaika na mambo ambayo hayana mchango kwenye mafanikio wanayotaka kuyajenga. Wanaishia kupoteza muda na kukosa mafanikio.
Kujenga mafanikio makubwa, kuwa na usimamizi sahihi wa muda wako. Pangilia muda wako vizuri na utumie kwa hayo tu uliyopangilia. Usifanye chochote ambacho hakina mchango kwako kufanikiwa. Na kadiri unavyokuwa unapiga hatua, nunua muda wa wengine pia ili uweze kuzalisha matokeo makubwa zaidi.
Rasilimali ya nne ni Nguvu za mwili wako.
Mwili wako ni kama betri ya simu, unapolala ni kuuchaji. Hivyo unaamka mwili ukiwa umejaa chaji, ambazo ni nguvu za mwili. Sasa basi, kila unachofanya kinakuwa kinapunguza nguvu hizo. Mpaka siku inaisha, mtu anakuwa ametumia nguvu zake zote. Swali ni je anakuwa amezalisha matokeo gani?
Kwa walio wengi, wanatumia nguvu zao za mwili kufanya mambo ambayo hayana tija kabisa. Yaani wanafanya mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye mafanikio yao. Hilo linawapelekea kuchoka sana, lakini hakuna hatua wanakuwa wamepiga.
Kujenga mafanikio makubwa, pangilia vizuri mambo yote unayofanya. Muda wa mapema kwenye siku yako usifanye mambo ambayo hayana mchango kwenye mafanikio yako. Hayo ni mambo unayopaswa kuyafanya ukiwa na nguvu, kwa sababu ukiyafanya umechoka, inakuwa rahisi kuahirisha. Tenga muda wa mapema kwenye siku yako kwa majukumu muhimu ya mafanikio yako. Kwa njia hiyo utaweza kutumia nguvu zako kufanya makubwa.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeeleza kwa kina matumizi sahihi ya hizo rasilimali nne ili kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yetu. Karibu ujifunze kwenye kipindi hicho na uchukue hatua ili kujijengea mafanikio makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.