Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambayo ni maalumu kwetu kujenga utajiri kupitia uwekezaji wa muda mrefu.

Kwenye programu hii tunajifunza na kuchukua hatua kwenye uwekezaji ili kupata matokeo ya uhakika kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye somo hili ambapo tunakwenda kujifunza kutokujaribu mchezo unaowashinda wenye uzoefu, ujuzi na muda wa kuucheza kuliko wewe. Hili ni somo muhimu kutusaidia tutulie kwenye mpango wetu na kuepuka tamaa zinazowapoteza wengi.

AINA ZA UWEKEZAJI NA SAHIHI KWAKO.

Inapokuja kwenye uwekezaji, kuna aina mbili;

Aina ya kwanza ni uwekezaji wa kushiriki kwenye soko moja kwa moja (Active Investing).

Huu ni uwekezaji ambao wewe mwenyewe unaingia kwenye soko la uwekezaji na kuchagua uwekezaji wa kufanya. Lengo kuu likiwa ni kulizidi soko kwa kupata faida kubwa kuliko ile inayopatikana kwa wastani. Aina hii inataka mtu kuwa na ujuzi, uzoefu na muda mwingi wa kufuatilia uwekezaji kwa upana.

Aina ya pili ni uwekezaji ambao siyo wa moja kwa moja (Passive Investing).

Huu ni uwekezaji ambao huingii kwenye soko la uwekezaji moja kwa moja na kuchagua uwekeze wapi. Badala yake unawekeza kwa kuchagua mifuko ya pamoja au mifuko ya soko zima. Uwekezaji huu huwa unaleta rejesho la wastani wa soko, ambalo siyo kubwa sana. Lakini uwekezaji huu hauhitaji wewe kuwa na ujuzi, uzoefu au muda mwingi wa kufuatilia uwekezaji.

TAMAA INAVYOWAPOTEZA WATU KWENYE UWEKEZAJI.

Baadhi ya watu, kwa tamaa ya kutaka kupata marejesho makubwa, huwa wanaona ni bora waingie kwenye uwekezaji wa moja kwa moja. Wanaona marejesho ya uwekezaji usio wa moja kwa moja ni madogo na wanaweza kupata zaidi.

Ambacho wanakuwa hawaoni kwa haraka ni kwamba kwenye uwekezaji wa moja kwa moja kuna watu ambao ndiyo kazi yao kamili. Wana ujuzi mkubwa, uzoefu wa hali ya juu na muda wa kutosha. Lakini bado wanapata hasara kila baada ya muda fulani.

Sehemu kubwa ya wawekezaji wa moja kwa moja huwa wanapata hasara pale wanapojaribu kuvizia au kuzidi soko. Kumbuka hao uwekezaji ndiyo kazi yako kuu. Sasa fikiria wewe ambaye uwekezaji siyo kazi yako kuu, ni matokeo gani unayokwenda kupata?

Ndiyo maana somo la leo linatutaka tusijaribu mchezo unaowashinda wale wenye ujuzi, uzoefu na muda kuliko sisi.

SOMA; Mpango Wa Uwekezaji Kwenye Mifuko Ya Pamoja Kulingana Na Umri.

KAZI YAKO KUU SIYO UWEKEZAJI.

Tumechagua kujenga utajiri mkubwa kupitia uwekezaji kwa muda mrefu bila kuacha wala kuvuruga. Lakini kazi yetu kuu siyo uwekezaji, tuna majukumu mengine ambayo ndiyo yanatuingizia kipato.

Hivyo hatuna ujuzi mkubwa, uzoefu wala muda mwingi wa kupeleka kwenye kufanya uwekezaji kwa kina. Kujaribu kushindana au kuwaiga wale ambao wanacheza na soko muda wote, ni kujipoteza sisi wenyewe.

Tunapaswa kujikumbusha hili kila mara, hasa tunaposikia baadhi ya watu wamepata faida kubwa kwenye uwekezaji fulani.

Kwenye safari ya kujenga utajiri, tamaa na wivu vimewapoteza wengi sana.

TOFAUTISHA BAHATI NA JUHUDI.

Tukiendelea na hilo la baadhi ya watu kupata faida kubwa kwenye uwekezaji fulani, huwa ni rahisi kuona mafanikio au faida hiyo ya mara moja. Lakini nyuma ya pazia mambo huwa ni tofauti kabisa.

Mara nyingi faida kubwa huwa ni za mara moja na zinatokana na bahati. Haiwi juhudi ambazo mtu ameweka. Hivyo hata hao hao wanaokuwa wamepata faida kubwa ya mara moja, hawawezi kurudia kupata tena faida ya aina hiyo.

Hivyo kabla hujachotwa na hadithi za waliopata faida kubwa, jiulize kwanza kipi kimechangia, juhudi au bahati. Kama mtu ameweza kupata faida kubwa kwa kurudia rudia kwa muda mrefu, jua ni juhudi. Lakini kama ni mara moja tu na hajaweza kurudia tena, basi ilikuwa bahati.

Usije ukahangaika kubadili mipango yako kwa sababu ya matokeo ya wengine ambayo yametokana na bahati.

KAA KWENYE MKAKATI WAKO.

Kwenye maisha, kila kitu huwa kinafanya kazi kama kitafanyiwa kazi kwa muda mrefu. Watu wengi huwa hawapati matokeo mazuri kwa sababu hawafanyii kazi kitu kwa muda mrefu.

Wanakuwa na mkakati na kuanza kuufanyia kazi, lakini matokeo yanapochelewa, wanaachana na mkakati huo. Au wakikutana na changamoto au vikwazo, wanaachana na mkakati.

Kubwa zaidi ni pale wanaposikia wengine wamepata matokeo makubwa na mikakati yao, wanaona hiyo ndiyo inafanya kazi. Hapa tena tamaa na wivu unawafanya watu waachane na mikakati yao na kuiga ya wengine, wakati matokeo yanaweza kuwa yametokana na bahati tu.

Ukishaweka mkakati wako, kaa kwenye mkakati huo kwa muda mrefu. Ufanyie kazi hasa mkakati huo, kwa msimamo bila kuacha na matokeo yatakuja mazuri na kwa wakati wake.

Muda utakaopoteza kwenye kubadili mikakati kila mara unakugharimu kwa kuchelewa kujenga utajiri ambao ungeupata kama ungetulia na mkakati wako mmoja.

NGAZI ZA JUU ZAIDI.

Kwenye nguvu ya buku tumechagua uwekezaji usio wa moja kwa moja, ambapo tunawekeza kwenye mifuko ya pamoja. Je huo ndiyo mwisho? Jibu ni hapana, kuna ngazi za juu zaidi, hizi ni kwa wale ambao wanafanikiwa kujenga uwekezaji mkubwa sana, ambao kwa kuwekeza moja kwa moja wanaweza kuboresha faida wanayopata.

Unapofika ngazi hizo za juu, unaweza kuchagua kuingia kwenye soko moja kwa moja, kwa kufanya mwenyewe au kuajiri wasimamizi wa uwekezaji wenye ujuzi, uzoefu na muda wa kufanya hilo.

Unaingia mwenyewe kama utachagua kufanya uwekezaji kuwa kazi yako kuu. Na kama umefika hatua hiyo, unakuwa pia na fursa ya kusimamia fedha za wengine na hivyo kuongeza kipato na utajiri kupitia kulipwa na hao unaosimamia fedha zao.

Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni wakati gani wa kwenda ngazi za juu zaidi? Na jibu ni utajua pale unapofikia, kwa sababu utakuwa unaona jinsi ambavyo usimamizi bora wa uwekezaji mkubwa ulionao unaweza kuleta matokeo mazuri zaidi kuliko ambayo unapata kwenye mifuko ya pamoja inayosimamiwa na wengine.

Hii ni ngazi ambayo wanaopaswa kuifanyia kazi ni wale ambao wanapenda hasa mchezo wa uwekezaji. Lakini kwa wengi ambao lengo ni kuwa na utajiri na uhuru wa kifedha, haina haja ya kujihangaisha na hizo ngazi za juu.

Ukishaweza kufikisha kiwango cha uwekezaji ambacho rejesho lake linatosha kuendesha maisha yako huku uwekezaji ukiendelea kukua, inakutosha.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;

1. Elezea aina mbili za uwekezaji na tofauti zake.

2. Eleza kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua aina ipi ya uwekezaji na kwa nini.

3. Unawezaje kutofautisha matokeo yanayotokana na bahati na yanayotokana na juhudi?

4. Utawezaje kuzuia tamaa na wivu unaotokana na matokeo ya wengine visikuondoe kwenye mkakati wako mkuu wa uwekezaji?

5. Karibu uulize swali au kutoa maoni kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Shirikisha majibu ya maswali hayo kama uthibitisho kwamba umesoma, kuelewa na kwenda kufanyia kazi yale uliyojifunza kwenye somo hili.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.