3426; Hujafanya vya kutosha.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna nyakati ambazo unafanya kitu kwa juhudi zako kubwa sana, lakini matokeo yanakuja tofauti kabisa na ulivyotegemea.

Wakati huo huo ukiwaangalia wengine ambao nao wanafanya kitu hicho hicho, matokeo yao yanakuwa ni mazuri.

Katika hali kama hiyo ni rahisi kuona wewe huwezi kama hao wengine.
Lakini unapokuja kuchunguza, unakuta hao wengine wamekuwa wanafanya kitu hicho kwa muda mrefu zaidi kuliko wewe.

Hivyo siyo kwamba wewe huwezi, bali ni hujafanya kwa kiasi cha kutosha.
Ina maana kama utaendelea kufanya kwa wingi zaidi, na wewe utakuwa vizuri kwenye kufanya kitu hicho.

Mara nyingi unakwama kwenye mambo kwa sababu unajilinganisha wewe ambaye ndiyo unaanza kufanya na ambao tayari wanakifanya kitu hicho kwa muda mrefu.
Hakuna namna mnaweza kuwa sawa, kwa sababu ambaye amefanya kwa muda mrefu  kuna vitu tayari amezoea.

Pale unapoanza kufanya kitu chochote, jipe muda wa kukifanya kwa kiwango cha kutosha kabla ya kusema ni vigumu kwako kufanya.

Na pale unapojilinganisha na wengine mwenye chochote unachofanya, hakikisha pia unalinganisha na muda ambao umewekwa kwenye ufanyaji.

Usilinganishe siku yako ya 10 na siku ya elfu 10 kwa mtu mwingine.
Weka na wewe muda wa kutosha, utaweza kuzalisha matokeo bora kwenye chochote unachofanya.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe