Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Moja ya vitu tunavyopaswa kuvifanyia kazi ili kuwa watu bora ni kuwa na shukrani. Maisha huwa yanatupitisha kwenye hali mbalimbali, jinsi tunavyopokea yote tunayopitia na kukutana nayo, inaamua ni mafanikio kiasi gani tunapata.
Kwenye mauzo na hata maisha kwa ujumla, kuwa mtu wa shukrani inalipa sana. Kwa kushukuru kwa kila jambo unalokuwa unapitia, unafungua milango ya mambo mazuri zaidi kutokea kwako.

Karibu kwenye somo hili ujifunze jinsi ya kuwa mtu wa shukrani na kutumia shukrani kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
KUWA MTU WA SHUKRANI.
Kwenye maisha, pale mambo mazuri yanapotokea, huwa tunayafurahia na kuona tumeweza kuweka juhudi kupata matokeo hayo mazuri. Lakini matokeo hayo mazuri huwa yanatokea mara chache, tena baada ya kupitia matokeo yasiyokuwa mazuri.
Sehemu kubwa ya matokeo ambayo huwa tunayapata kwenye maisha, ni tofauti kabisa na tulivyokuwa tunategemea. Jinsi tunavyopokea matokeo hayo ya tofauti, huwa inaamua kama tutaweza kuendelea na kupata matokeo mazuri baadaye au ndiyo inakuwa mwisho.
Kwenye kukabiliana na matokeo ambayo hatukutegemea, unaweza kuchukua upande mmoja kati ya pande hizi mbili;
Upande wa kwanza ni kulalamika na kulaumu kwa yale unayokuwa unapitia. Hii ndiyo njia ambayo huwa inatumiwa na wengi, kwa sababu ni rahisi kutumia. Njia hii haihitaji uwajibikaji wowote, ni kuangalia tu nani anayeweza kubeba lawama na anabebeshwa hizo. Njia hii huwa ni mwisho wa ufanyaji na mtu hawezi kupata mafanikio makubwa.
Upande wa pili ni kushukuru kwa yale unayokuwa umepitia. Hii ni njia inayotumiwa na watu wachache kwa sababu ni vigumu kushukuru pale matokeo yanapokuwa tofauti na matarajio. Kwa kushukuru, mtu anapata fursa ya kujifunza na kuweza kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.
Ili uweze kuwa mtu wa shukrani, lazima ukubali kuwajibika. Lazima ukubali kwamba kila matokeo unayoyapata, wewe ndiye uliyechangia kwa sehemu kubwa. Hata pale kunapokuwa na mchango wa wengine kwenye kusababisha matatizo hayo, bado unajua wewe ndiye mhusika mkuu.
Kwa kukubali kuwajibika na kushukuru, unafungua fursa ya kujifunza na kuweza kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.
SHUKURU KWA KAZI YAKO YA MAUZO.
Kazi ya mauzo imekuwa inachukuliwa kama kitu ambacho mtu anafanya pale anaposhindwa kufanya vitu vingine ambavyo alitaka. Hivyo wengi huwa hawaipi heshima ya kutosha, kitu kinachowafanya wasipate matokeo mazuri.
Wengi wameingia kwenye mauzo kama sehemu ya kujishikiza wakati wanasubiri wapate kazi za ndoto zao. Hawaoni mauzo kama kazi inayoweza kukamilisha ndoto kubwa za maisha yao.
Kuwa mtu wa shukrani kunaweza kukusaidia kubadili mtazamo wako kuhusu kazi ya mauzo. Unachopaswa kufanya ni kuangalia watu wote ambao wananufaika kupitia mauzo unayofanya wewe.
Kwa kuanza na wateja ambao wanatumia bidhaa au huduma unayouza, hebu jiulize maisha yao yangeendaje kama wasingeweza kupata kile unachouza, kwa ubora na bei nzuri ambayo inapatikana kwako.
Nenda kwa biashara na jiulize biashara ingewezaje kujiendesha kama kusingekuwa na mauzo, maana mauzo ndiyo njia pekee ya kuingiza fedha kwenye biashara.
Rudi kwenye maisha yako binafsi, ona jinsi ambavyo kazi ya mauzo imekuwezesha kuingiza kipato cha kuyaendesha maisha yako, tena kwa heshima. Jiulize maisha yako yangekuwaje kama usingekuwa na kazi hiyo ya mauzo.
Huwa wanasema kazi inaonekana mbaya au inachosha pale unapokuwa nayo na kuizoea. Lakini ukijikumbusha ulikotoka na mchango ambao kazi yako ya mauzo inakuwezesha kufanya kwa wengine, ni jambo la kushukuru sana.
Na pale unaposhukuru kwa kazi ya mauzo uliyonayo, unaifanya kwa moyo mmoja na hivyo kuifanya vizuri zaidi.
Kila siku ya mauzo unayoianza, shukuru kwa fursa nzuri uliyopata ya kuwa na mchango kwenye maisha ya wateja wako, biashara ambayo wewe ni muuzaji na maisha yako ninafsi. Haya ni ya kujikumbusha kila siku ili usiruhusu mazoea kuingia na kuvuruga kazi yako.
SOMA; Kutumia Shukrani Kufanya Makubwa Kutoka Falsafa Ya Ustoa.
SHUKURU KWA KILA HATUA YA MAUZO.
Kila hatua unayopiga kwenye mauzo ni jambo la kushukuru. Badala ya kusubiri mpaka unapokamilisha mauzo ndiyo ufurahie, unapaswa kufurahia kila hatua. Na utaweza kufurahia kila hatua kama utashukuru kwa hatua hiyo.
Kumpata mteja tarajiwa ambaye anaweza kunufaika na kile unachouza ni jambo la kushukuru na kufurahia. Kwa sababu unakuwa umepata mtu wa kumfuatilia na kumshawishi kununua.
Kumfuatilia mteja na kukataliwa ni jambo la kushukuru, kwa sababu angalau amejua uwepo wako. Anayekukataa anakujua, asiyekujua kabisa anakupuuza. Badala ya kuumizwa na kukataliwa na mteja, unashukuru na hivyo kuchukua hatua nyingine ya kumfikia bila kukata tamaa.
Unapopata miadi na mteja ni jambo la kushukuru, kwa sababu unapata fursa ya kumshawishi zaidi.
Mteja anapokupa mapingamizi ni jambo la kushukuru, kwa sababu wateja wenye mapingamizi ndiyo huwa wananunua. Kwa kuweza kujibu mapingamizi yao unawashawishi kununua.
Unapokamilisha mauzo kwa mteja ni jambo la kushukuru, kwa sababu unakuwa umepata fursa ya kumhudumia, umeingiza mapato kwenye biashara na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa na kipato kikubwa.
Shukuru kwa kila hatua unayochukua kwenye mchakato wa mauzo na utaweza kudumu kwenye mchakato huo na kuwa muuzaji bora unayefanya mauzo makubwa.
WASHUKURU WATEJA MARA ZOTE.
Watu wa mauzo wanapokutana, huwa wanapeana hadithi za wateja wao wenye changamoto. Wanaambiana jinsi wateja walivyo na ahadi za uongo, wanavyokuwa na mapingamizi yasiyo na tija na wasivyokuwa na shukrani kwa kuweza kukuacha muda wowote na kwenda kwa washindani.
Pamoja na changamoto hizo nyingi ambazo wateja wanazo, maana nao ni watu, bado kuna mambo mengi mazuri ambayo wateja wanayo pia. Kwa kuchagua kuwashukuru wateja, inakulazimisha uone mambo mazuri kwao kitu kinachokupa fursa ya kuwahudumia vizuri.
Kwa kila mteja uliyenaye, awe tarajiwa au kamili, tafuta kitu unachoweza kumshukuru kwa hicho. Kila mteja ambaye unaye, hakikisha unakuwa na kitu cha kumshukuru moja kwa moja.
Kabla ya kukutana au kuwasiliana na mteja, tafuta kitu ambacho utawashukuru nacho. Na baada ya kuwasiliana au kukutana na mteja, mshukuru kwa yale ambayo mmeafikiana kwenye mazungumzo au mawasiliano ambayo mmefanya.
Ukifanya zoezi hili la kuwashukuru wateja wako mara zote, utapata faida mbili;
Moja ni kuwa na mtazamo chanya kwa kila mteja, kitu ambacho kitakufanya uwe na ushawishi mzuri kwao. Unaposhukuru unakaribisha zaidi kile ambacho umekishukuru.
Na mbili ni kuwafanya wateja wakuonyeshe ushirikiano mzuri kwa sababu ya shukrani unazokuwa nazo kwao. Watu huwa wanajisikia vizuri pale wanapopewa shukrani na hivyo kuendelea kufanya yale ambayo wameshukuriwa kufanya.
Kwa sababu huwa tunaona kile tunachotaka kuona, tunapotafuta kitu cha kushukuru kwa kila mteja, tunakipata na hilo kurahisisha mchakato wetu wa mauzo.
Kama unaona huna cha kushukuru kwa kila mteja wako, maana yake hufanyii kazi vizuri mchakato wako wa mauzo. Kwa sababu ukifanyia kazi mchakato vizuri, fursa za kushukuru wateja ni nyingi. Kwa kila hatua lazima utapata kitu cha kushukuru.
Kumpata mteja tarajiwa shukuru, kupata mazungumzo au mawasiliano naye shukuru, kupata mapingamizi shukuru, kukamilisha mauzo shukuru, kupata wateja wa rufaa shukuru.
Una fursa nyingi za kuwashukuru wateja, zitumie na itaboresha mahusiano yako na wateja, kukufanya kuwa muuzaji bora na kukamilisha mauzo makubwa zaidi.
Shukrani ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukitumia kuwa bora na kufanya kwa ukubwa kile anachofanya. Kwenye mauzo shukrani ni muhimu katika kuyapenda mauzo na kuimarisha mahusiano na wateja. Mara zote kuwa mtu wa shukrani na utaweza kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.