Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kutoka kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Lengo letu ni kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kupitia uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo, kwa muda mrefu bila kuacha.
Kwa masomo ambayo tumeshayapata mpaka sasa kuhusu utajiri na uwekezaji, tunaona wazi kabisa kwamba kila mtu, bila ya kujali ni kipato kiasi gani anaingiza, anaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake.
Pamoja na uwezo huu wa kila mtu mwenye kipato kujenga utajiri, bado ni wachache sana ambapo wamekuwa wanafanikiwa kujenga utajiri.
Karibu kila mtu anakuwa na miaka isiyopungua 30 ya kuingiza kipato kwenye maisha yake. Kama mtu angewekeza asilimia 10 tu ya kipato chake kwa kipindi cha miaka hiyo 30, ni lazima atajenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake. Na hata kama atakuwa amechelewa, bado kwa miaka 20 au hata 10, anaweza kufanya uwekezaji utakaobadili kabisa maisha yake.

Lakini uhalisia umekuwa ni tofauti kabisa. Watu wanafika mwisho wa maisha yao wakiwa na hali duni za kifedha, licha ya kuteseka kufanya kazi kwa maisha yao yote. Wanateseka wakati wana nguvu za kufanya kazi halafu wanakuja kuteseka zaidi pale nguvu za kazi zinakuwa zimeisha.
Kinachopelekea hali hii ni kukosekana kwa tabia muhimu mbili na uwajibikaji kwenye safari ya kujenga utajiri. Kwenye somo hili unajifunza tabia hizo na kupata uwajibikaji ambao utahakikisha unajenga utajiri kweli.
NIDHAMU KALI YA FEDHA.
Tabia ya kwanza unayopaswa kujijengea ili kuweza kujenga utajiri kwenye maisha yako ni nidhamu kali ya fedha. Nidhamu hiyo ni kuhakikisha kwa kila kipato unachoingiza, unatenga kwanza pembeni kiasi cha akiba kabla ya matumizi.
Unapoingiza kipato hupaswi kuanza matumizi halafu kinachobaki ndiyo uweke akiba na kuwekeza. Matumizi huwa hayaishi, hivyo ukianza nayo una uhakika wa kumaliza kipato chote na usibaki na kitu.
Nidhamu sahihi ni pale unapoingiza kipato kutenga kwanza kiasi cha akiba halafu inayobaki ndiyo unaitumia. Kwa kuwa umeshaondoa kile ulichopanga, itakulazimu ujibane kwenye kile kilichobaki.
Na hili siyo geni, kwa kipato chochote ambacho mtu unaingiza, kuna makato huwa yanafanyika, na unajifunza kuishi kwenye kile kilichobaki baada ya makato.
Hivyo pia ndivyo unavyochukulia kwenye akiba unayopaswa kuweka, ona ni makato ambayo lazima yafanyike kabla hujafanya matumizi.
Kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako, hakikisha unajijengea nidhamu kali ya fedha.
MSIMAMO WA KUWEKEZA BILA KUACHA.
Tabia ya pili muhimu unayopaswa kujijengea ili uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako ni kuwekeza kwa msimamo bila kuacha. Uwekezaji unaopaswa kufanya ni wa kiasi kidogo kidogo na wenye marejesho ya kawaida. Ukiangalia kwa muda mfupi, unaweza kuona bora kutumia fedha hizo kwa mambo mengine ambayo yatazalisha kwa ukubwa zaidi. Lakini faida kubwa ya uwekezaji ni kwenye muda ambao mtu unawekeza.
Ukikosa msimamo kwenye kuwekeza kwa muda mrefu bila kuacha, hutaweza kunufaika na uwekezaji. Na hilo ndiyo limekuwa linatokea kwa wengi. Wanazipata fursa za kuwekeza, lakini kwa kukosa subira na msimamo, wanahangaika na mambo mengine. Mwisho wanakuja kujikuta umri umeenda na hakuna wanachoweza kuonyesha.
Wewe unapaswa kuchagua uwekezaji ambao utaufanya kwa kipindi chote cha maisha yako bila kuacha. Unawekeza kwa msimamo, inyeshe mvua, liwake jua, hakuna kinachokukwamisha.
Ukiweza kujenga msimamo wa aina hii, hakuna kinachoweza kukuzuia kujenga utajiri. Kwa sababu muda tayari unao, kipato unacho, ni msimamo tu unaohitaji ili kupate matokeo makubwa.
SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.
MFUMO WA KUKUWAJIBISHA.
Kupanga mambo huwa ni rahisi, kufanya kama ulivyopanga huwa ni ngumu. Bila ya mfumo wa kukuwajibisha ili ufanye yale uliyopanga, hutaweza kufanya.
Utaanza kwa nia njema kabisa, lakini maisha yataingilia katikati na utaacha. Kama hakuna kinachokulazimisha kufanya kitu, hutakifanya.
Hivyo ili uweze kujenga nidhamu kali ya fedha na uwekezaji kwa msimamo bila kuacha, unahitaji mfumo wa kukuwajibisha.
Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU, tunapata mfumo wa uwajibikaji wa kundi ambao unatufanya tutekeleze mchakato wetu bila kuacha.
Kwa sababu tumeweka ahadi yetu mbele ya wengine na tunapaswa kutuma ushahidi, inatusukuma tutekeleze bila ya kuacha.
CHAGUA KUTESEKA WAKATI MMOJA TU.
Maisha huwa yana mateso, hicho ni kitu ambacho hatuwezi kukikwepa kabisa. Lakini kwa bahati mbaya, watu wamekuwa wanachagua kuteseka kwa maisha yao yote.
Wanateseka wakati wana nguvu za kufanya kazi, kwa kipato kutokutosheleza na kutokuweka akiba wala kuwekeza.
Halafu tena wanakuja kuteseka wakati nguvu za kufanya kazi zimeisha, kwa kutokuwa na uwekezaji wa kuwawezesha kuendesha maisha yao.
Wewe hupaswi kukubali hilo, chagua kuteseka wakati una nguvu za kufanya kazi, lakini ujenge uwekezaji ambao utayafanya maisha yako yaweze kwenda vizuri pale nguvu za kazi zinapokuwa zimeisha.
Hapa utachagua kuhakikisha unafanya uwekezaji kama ulivyopanga bila kuacha, hata kama utateseka kiasi gani, kwa sababu hutaki kupeleka mateso hayo mbele.
ADHABU YA KUTOKUFANYA.
Ili ikuume na ufanye uwekezaji, programu ya NGUVU YA BUKU itakuwa na adhabu kwa wale wote ambao hawatawekeza na kutuma ushahidi kwenye kundi kama ilivyoelekezwa.
Utaratibu wa programu ya nguvu ya buku ni kama ifuatavyo;
1. Kufanya uwekezaji kila siku ya jumatatu, kiwango kisichopungua elfu 7 na kutuma ushahidi kwenye kundi.
2. Kutuma salio la uwekezaji kila siku ya ijumaa, ili kujizuia usitoe uwekezaji wako.
3. Kusoma masomo ya uwekezaji na kutoa mrejesho kwa siku za jumatatu na ijumaa.
Kutekeleza hayo kwa msimamo bila kuacha inakupa nafasi ya kuendelea na programu kwa kipindi kisichopungua miaka 10 ambacho tumejipa.
Kushindwa kutekeleza hayo, kutafanya uwe na faini ambayo ni sawa na kiwango cha uwekezaji ambacho umekuwa unafanya kila wiki. Na kama utashindwa kulipa faini hiyo basi utaondolewa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU.
Nia yetu siyo kumpoteza mwekezaji yeyote, lakini kwa tabia zetu binadamu, bila ya kuwa na mfumo wa uwajibikaji na unaoumiza, ni rahisi kuacha kufanya yale ambayo yana manufaa kwetu.
Hivyo mfumo huu wa adhabu ni kwa lengo la kuhakikisha tunapata msukumo wa kufanya bila kuacha, kwa manufaa yetu wenyewe.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Ni nidhamu gani kali ambayo umeshaweza kujijengea kwenye eneo la fedha ili kuhakikisha matumizi hayazidi mapato?
2. Ni msimamo gani ambao umejijengea ili uweze kufanya uwekezaji kwa msimamo bila kuacha, hata pale unaposhawishika kufanya vitu vingine vinavyoonekana kulipa zaidi?
3. Unatumiaje mfumo wa uwajibikaji wa programu ya NGUVU YA BUKU kuhakikisha unaweza kujenga utajiri wa uhakika kwenye maisha yako?
4. Karibu kama una swali, maoni na mapendekezo yoyote kwa somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kwenda kufanyia kazi somo hili la uwekezaji.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.