Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye #HadithiZaKocha ambapo tunapata hadithi fupi zenye masomo makubwa sana kuhusu mafanikio na maisha kwa ujumla.

Leo tunakwenda kupata hadithi fupi ya kisa cha Watawa wawili na Mwanamke kahaba.

Siku moja watawa wawili, mmoja mwalimu na mwingine mwanafunzi walikuwa wanavuka mto kwenda ng’ambo ya pili.

Walipofika kwenye ukingo wa mto, walimkuta mwanamke kahaba ambaye alitaka kuvuka lakini aliogopa kuchukuliwa na maji.

Mwanamke yule alipowaona akashukuru sana na kuwaomba wamsaidie kuvuka kwa kumbeba mgongoni.

“Sisi ni watawa na haturuhusiwi kuwashika wanawake”, alijibu kwa haraka yule mtawa mwanafunzi.

Alimwangalia mwalimu wake akitegemea asisitize hilo kisha wavuke na kumwacha mwanamke yule.

Lakini mwalimu hakusema kitu, badala yake alimwambia mwanamke yule; “Panda mgongoni kwangu nikuvushe.”

Mwanamke alipanda mgongoni kwa mtawa na akavushwa mpaka ng’ambo ya pili. Mtawa alimshusha na mwanamke yule akashukuru sana.

SOMA; #HadithiZaKocha; Kisa Cha Kuku Anayetaga Mayai Ya Dhahabu.

Watawa waliendelea na safari yao, kwa muda walitembea bila ya kusemezana. Baada ya muda mrefu kupita, yule mtawa mwanafunzi akaanza kumsemesha mwalimu wake.

“Nashindwa kukuelewa kabisa mwalimu, kwa nini umembeba yule mwanamke wakati sisi watawa haturuhusiwi kuwagusa wanawake?”

Mwalimu alimjibu kwa upole; “Mimi nimembeba mwanamke na kumtua baada ya kuvuka mto, kwa nini wewe umembeba mpaka sasa?”

Rafiki, maneno hayo yalimwingia sana yule mwanafunzi na akawa amepata somo kubwa sana la maisha.

Je ni somo gani ambalo umeondoka nalo kwenye kisa hiki kifupi? Unaendaje kulitumia somo hilo ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi? Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.

Hapo chini nimekielezea kisa hicho pia, fungua ujifunze na kuweka maoni yako ya nini umejifunza kutokana na kisa hicho. Karibu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.