3430; Unachovutia wewe mwenyewe.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Matokeo ambayo tunayapata kwenye maisha yetu, huwa tumeyatengeneza au kuyavutia sisi wenyewe.

Unatengeneza matokeo pale unapochukua hatua za aina fulani kwenye kitu husika.
Na unavutia matokeo pale unapokuwa na tabia za aina fulani.

Ni muhimu sana ujue pande zote mbili za matokeo, yanayotengenezwa na yanayovutiwa.
Hilo litakusaidia kuweza kuleta matokeo makubwa unayoyataka.

Hapa kuna baadhi ya matokeo na mambo yanayoyavutia;

Pesa huwa inavutiwa na kasi.
Ukiwa mtu wa kasi kwenye mambo yako, utavutia pesa zaidi kuja kwako.
Pale unapokuwa mtu wa kuchukua hatua kwa wakati bila ya kuahirisha mambo na kukamilisha vitu ndani ya wakati, unaishia kuvutia pesa nyingi kuja kwako.
Hivyo kama unataka kupata pesa zaidi, weka kasi zaidi kwenye mambo yako yote.

Utajiri huwa unavutiwa na muda.
Kadiri mtu anavyojipa muda wa kutosha kwenye kitu anachofanya, ndivyo anavyouvutia utajiri kuja kwake.
Utajiri unajengwa kwa mkusanyiko wa vitu sahihi vilivyofanyika kwa muda mrefu bila kuacha.
Ukiweza kujipa muda mrefu zaidi kwenye kufanya kitu, hakuna namna utaweza kuukwepa utajiri.

Umasikini unapenda kutokufanya maamuzi.
Ni pale mtu anapojiendea tu kwa mazoea na kufuata mkumbo bila ya kuamua chochote yeye mwenyewe ndiyo anaishia kwenye umasikini.
Wengi wanaonasa kwenye umasikini wanakuwa wanajua kabisa wanachopaswa kufanya. Lakini huwa wanashindwa kufanya maamuzi na kutekeleza hayo yanayohitajika.
Matokeo yake yanakuwa ndiyo kukaa kwenye umasikini wakati wote.

Popote ulipo sasa, jiulize umepavutiaje wewe mwenyewe.
Na popote unapotaka kufika, jiulize nini unapaswa kufanya ili kuweza kupafikia.

Ni kwa kuwa na tabia sahihi zinazovutia mafanikio pamoja na kuchukua hatua sahihi zinazojenga mafanikio, ndiyo mafanikio makubwa yanapatikana kwa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe