3431; Kupata furaha ya kudumu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanachanganya sana furaha na raha.
Furaha huwa ni kitu cha muda mrefu na huwa inaanzia ndani ya mtu.
Wakati raha ni kitu cha muda mrefu na kibaanzia nje ya mtu.

Watu wengi wamekuwa wanahangaika na raha, wakidhani ni furaha.
Wanahangaika wapate vitu vya nje ambavyo vinawapa raha, lakini bado haviwaridhishi.
Kwani kila wanapopata raha, inadumu kwa muda mfupi na hivyo kulazimika kutafuta kitu kingine kitakachompa raha.

Matokeo yake ni mtu kujikuta kwenye hali ya uteja ambapo kila mara anakimbizana na vitu vinavyompa raha ya muda mfupi.

Kuondokana na hilo, unapaswa kuchukua hatua ambazo zinakula furaha ya kudumu.
Na furaha ya kudumu huwa inapatikana pale mtu anaporudi kwenye asili yake na kufuata mchakato sahihi kwake.

Asili ya binadamu ni ukuaji na watu huwa wanakuwa na furaha pale wanapokuwa na ukuaji.
Pale mtu anapoona ametoka hatua moja kwenda nyingine, anakuwa na furaha.

Hivyo basi, ili kuwa na furaha inayodumu, hakikisha mara zote kuna vitu unajenga kwenye maisha yako.
Kuwa na mchakato wa kujenga vitu mbalimbali kwenye maisha yako, ukitoka chini na kwenda juu kabisa.

Haijalishi unajenga nini, muhimu ni kuwa kwenye ule mchakato wa ukuaji endelevu.
Unaweza kujenga biashara, mahusiano, kazi, utajiri n.k.

Watu huwa wanakuwa na furaha zaidi pale wanapokuwa wanajenga vitu mbalimbali kwenye maisha yao.
Ni zile hatua ambazo mtu anakuwa anapiga kwenye ukuaji ndizo zinachochea furaha ndani ya mtu.

Na kwa sababu ukuaji ni endelevu, basi furaha nayo inakuwa endelevu.

Kila mara unapojikuta huna furaha au unataka kukata tamaa na maisha, jiulize nini unajenga kwa wakati huo.
Utajikuta kwamba hakuna kikubwa unachojenga na hivyo akili yako kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija.

Unapokuwa unapambania ukuaji, akili yako yote inakuwa kwenye ukuaji huo na hivyo kutokuwa na nafasi ya kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija.

Mara zote kuwa na malengo ya ukuaji zaidi ambayo yanataka umakini wako wote.
Hapo utaondoa hali zote za wasiwasi unaokuwa unakukwamisha.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe