3435; Ni kujitakia mwenyewe.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Changamoto na vikwazo vingi ambavyo watu wanakutana navyo kwenye maisha, huwa ni vitu vya kujitakia wenyewe.

Mtu anakuwa kuna vitu alifanya au kushindwa kufanya huko nyuma na sasa ndiyo wakati wa kulipa.

Mtu anaweza kuonekana kulalamika na kuumizwa sana, lakini ni yeye mwenyewe anayekuwa amesababisha mambo hayo.

Hata jinsi ambavyo watu wanamchukulia mtu, ni jinsi ambavyo mtu mwenyewe amewaruhusu watu wamchukulie.
Kadiri mtu anavyojichukulia wa chini na kuwaruhusu watu pia wamchukulie wa chini, ndivyo anavyowafundisha wengine kufanya hivyo.

Watu wanaokuzunguka, ambao wanakukwamisha na kukuangusha, ni wewe mwenyewe umewapa nafasi kwenye maisha yako.
Hakuna anayekulazimisha uendelee kuwa na watu hao.

Binadamu wote tunazaliwa na uhuru mkubwa wa kuweza kuamua chochote tunachotaka kwenye maisha yetu.
Katika kutaka mambo yawe rahisi, watu wamekuwa wanapoteza uhuru huo.
Wanafika hatua ambayo hawana kabisa uhuru na kulalamikia hilo.
Unapoangalia, unaona kabisa wao wenyewe walikubali kuachia uhuru wao ili kupata vitu walivyokuwa wanataka.

Kadiri unavyokuwa na utegemezi kwa watu na vitu vingi, ndivyo pia nafasi ya kukwamishwa inakuwa kubwa na uhuru kuwa kidogo.
Hatua unazopiga zinategemea sana uhuru unaokuwa nao.
Iko ndani ya uwezo wako kutunza uhuru ulionao, lakini hilo litaanza na wingi wa watu na vitu unavyotegemea katika kutekeleza mambo yako.

Somo hapa siyo kutokushirikiana na wengine kabisa, hilo haliwezekani.
Bali somo ni wewe kutunza uhuru wako na kuutumia kwenye maamuzi yote muhimu kwako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe