Rafiki yangu mpendwa,
Maisha huwa ni maigizo na yale ambayo kila mmoja wetu anaigiza, yana madhara chanya au hasi kwenye maisha yake.
Inapokuja kwenye fedha, masikini huwa wanaigiza kama ni matajiri. Wanakuwa na matumizi makubwa ili kujionyesha wana uwezo. Hilo linawaingiza kwenye gharama kubwa na kuingia kwenye madeni ambayo yanawafanya wabaki kwenye umasikini zaidi.
Kwa upande wa pili, matajiri huwa wanaigiza kama ni masikini. Wanakuwa na maisha ya kawaida ambayo mtu asiyewajua kwa undani hawezi kudhani kwamba wana utajiri mkubwa kama walionao. Wanakuwa na matumizi madogo na ya kawaida kabisa. Maisha yao kwa nje yanaonekana ya kawaida. Hilo linawawezesha kujenga utajiri zaidi, kwa sababu wanakuwa hawana matumizi makubwa.
Kwenye jamii, kuna watu wengi ambao wanaonekana kuwa na maisha ya kawaida, ila wanakuwa na utajiri ambao unawatosha kuendesha maisha yao kwa uhuru mkubwa. Kwa kuwa watu hao ni wa kawaida kabisa, wengi huwa hawaamini wanaweza kuwa na utajiri. Na hata wakijua watu hao wana utajiri, huwa wanaona hawakustahili kuupata.

Mwandishi Chris Hogan kwenye kitabu chake kinachoitwa EVERYDAY MILLIONAIRES ameonyesha jinsi watu wa kawaida kabisa walivyoweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao na jinsi hata wewe unaweza kufanya hivyo.
Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa mamilionea zaidi ya elfu 10 na kuweza kupata taarifa nyingi sana kuwahusu. Utafiti huo uligusa kila eneo la matajiri, kuanzia mitazamo, fikra, shughuli wanazofanya, mahusiano, familia n.k.
Mwandishi ameweza kuonyesha maeneo makubwa mawili ambayo matajiri na masikini wanatofautiana.
Eneo la kwanza ni MTAZAMO.
Mtazamo ambao masikini wengi wanao umekuwa unawakwamisha kujenga utajiri kwenye maisha yao. Ipo mitazamo mingi ambayo inawakwamisha, lakini hii sita ambayo mwandishi ameiainisha ndiyo kikwazo zaidi.
1. Matajiri wamerithi utajiri wao, huo siyo kweli, kwa sababu wengi wamejenga utajiri kwa juhudi zao na hata walioridhi, wameweka kazi kuukuza zaidi.
2. Matajiri wamekutana na bahati ambazo wengine hawajapata, siyo kweli, matajiri wanaweka juhudi kubwa kuliko wengine na kama wamekutana na bahati, ni kwa sababu ya juhudi walizoweka.
3. Matajiri wanachukua hatua za hatari ili kujenga utajiri, siyo kweli, matajiri wanakokotoa hatari na kuchukua zile ambazo wanaweza kuzimudu.
4. Matajiri wanatumia njia za mkato kujenga utajiri, siyo kweli, njia za mkato huwa zinawapoteza masikini wengi kwa sababu hazijawahi kufanya kazi.
5. Matajiri wamepata elimu kubwa na bora, siyo kweli, matajiri wengi wana elimu za kawaida na ufaulu ambao ni wa kawaida, tena wengine wakiwa hawana elimu au walifeli.
6. Matajiri wana kazi zinazowalipa mshahara mkubwa, siyo kweli, matajiri wengi wanafanya kazi na biashara za kawaida, tena wale wenye kazi zinazolipa sana huwa na gharama kubwa na kushindwa kujenga utajiri.
Ukivunja hiyo mitazamo sita, utaweza kuondoa kikwazo cha kwanza cha kujenga utajiri.
SOMA; Mjadala Wa Njia Kumi Za Kujenga Utajiri Kutoka Kitabu The Ten Roads To Riches.
Eneo la pili ni TABIA.
Kuna tabia ambazo matajiri wanazo na wanaziishi kwenye maisha yako lakini masikini hawana. Mwandishi ameweza kuanisha tabia tano za msingi kabisa.
1. Kuwajibika kwa kila kitu kwenye maisha, matajiri wanawajibika, hawalaumu wala kumlalamikia yeyote.
2. Kufanya kwa makusudi, matajiri hawafanyi mambo kwa kubahatisha au kusubiri wakutane na bahati, badala yake wanakusudia na kufanya ili kuleta matokeo wanayoyataka.
3. Kuongozwa kwa malengo, matajiri wana malengo yaliyopangiliwa vizuri, kuandikwa na kufanyiwa kazi kwa uhakika.
4. Kufanya kazi kwa juhudi kubwa, matajiri wanaweka muda na juhudi kubwa sana kwenye kazi zao kuliko masikini.
5. Kuwa na msimamo wa kufanya bila kuacha, matajiri wakianza jambo huwa hawaishii njiani, bali wanalitekeleza mpaka mwisho.
Jijengee tabia hizo tano na zifanye kuwa sehemu ya maisha yako ili uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Ukishaweza kuvuka hayo mawili, kinachobaki ni wewe kutekeleza mikakati ya utajiri kama;
1. Kuongeza kipato chako kwa uendelevu, maana kipato ndiyo hatua ya kwanza kwenye kujenga utajiri.
2. Kuhakikisha matumizi hayazidi mapato, maana matumizi ndiyo yanayozuia kujenga utajiri.
3. Kuondoka kwenye madeni na kuepuka kuingia kwenye madeni, maana madeni ndiyo kaburi la utajiri.
4. Kuweka akiba kwa malengo na mipango mbalimbali, maana akiba ndiyo mbegu ya utajiri.
5. Kufanya uwekezaji unaokua thamani na kuingiza faida, maana uwekezaji ndiyo unaokuza utajiri.
Ukifanyia kazi mikakati hii mitano, ni lazima utajenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Hapa tumejifunza hatua za kuchukua ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha kwenye maisha yako. Karibu upate UCHAMBUZI KAMILI wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRES kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.
Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRE ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.