Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Mauzo yanahusisha watu na ili kuelewana vizuri na watu, lazima mtu uwe vizuri kwenye mawasiliano. Mafanikio kwenye mauzo yanamtaka mtu kuwa bora kwenye mawasiliano yake na watu wengine.
Mawasiliano yapo ya aina nyingi, lakini makundi makuu ya mawasiliano ni mazungumzo na maandiko. Katika kila aina ya mawasiliano, kuelewana ni muhimu ili mauzo yaweze kufanyika.
Hali nyingi za kutokuelewana baina ya watu huwa zinaanzia kwenye mawasiliano mabovu. Upande mmoja unasema kitu hiki, upande mwingine unaelewa kitu tofauti na hapo changamoto inazaliwa ambayo inakatisha mawasiliano kuendelea.

Ili kuwa muuzaji bora na uweze kufanya mauzo makubwa, unapaswa kuwa vizuri kwenye mawasiliano. Hapa unakwenda kujifunza mambo 10 ya msingi kuzingatia kwenye mawasiliano yako na wateja na hata watu wengine pia ili uwe bora na kuuza zaidi.
1. Sikiliza Kwa Umakini.
Kusikiliza kwa makini ndiyo msingi mkuu wa mawasiliano bora. Watu wengi kwa sasa siyo wasikilizaji wazuri, wakati wa mazungumzo wanakuwa wanasubiria zamu yao ya kuongea.
Wewe kuwa msikilizaji makini, mtu anapokuwa anaongea, weka umakini wako wote kwake. Utaelewa vizuri na kuweza kutoa mrejesho sahihi. Huwezi kuwashawishi watu kama hujawaelewa na huwezi kuwaelewa kama hujawasikiliza kwa umakini mkubwa.
2. Kuwa Mwelewa.
Kuwaelewa watu ni hitaji muhimu kwenye kukamilisha mawasiliano na kuwa na ushawishi. Kuwaelewa wengine ni kuvaa viatu vyao na kuona vitu kwa mtazamo ambao wao wanao. Wewe kama muuzaji unakuwa na mtazamo ambao mteja anakuwa nao ili kuweza kumshawishi.
Kila unapowasiliana na mtu, jaribu kumwelewa kwa kuvaa viatu vyake. Jiulize kama wewe ungekuwa ndiyo yeye, vitu gani ungezingatia zaidi? Zingatia hivyo na utaweza kuwa na ushawishi mzuri.
3. Andika Vizuri.
Sehemu kubwa ya mawasiliano ya zama hizi ni ya kuandika. Kuanzia kuandika ujumbe mfupi wa simu, barua pepe mpaka maelekezo mengine mbalimbali. Kama hutaweza kuandika vizuri, siyo tu utashindwa kueleweka, bali pia wateja watakuona siyo mtu makini. Andika kwa usahihi na tumia vizuri lugha. Epuka kuandika maneno ya kifupi na boresha lafudhi yako pale inapokuwa na changamoto. Mfano matumizi ya L na R huwa na changamoto kwa wengi, unapoandika, hakikisha ni kwa usahihi.
Jifunze kuandika vizuri, kupitia kusoma na kuandika mara kwa mara. Waombe watu wakupe mrejesho kwenye jumbe unazoandika ili uweze kuwa bora.
4. Kuwa Na Udadisi.
Ili uweze kuwaelewa vizuri watu, unapaswa kuwa na udadisi. Udadisi unakufanya utake kujua zaidi kuhusu watu na hivyo kuuliza maswali sahihi. Kwa kuuliza maswali sahihi, watu watajieleza zaidi wakati wa kukujibu na hapo utapata njia bora za kuwashawishi.
Kila unapowasiliana na mtu, taka kujua mambo mengi zaidi kuhusu wao na hivyo kuwa na maswali mengi ya kuwauliza ambayo yanawafanya wajisikie vizuri kujieleza zaidi kwako.
5. Kuwa Mwaminifu.
Ili kuwa bora kwenye mawasiliano, unapaswa kuwa mwaminifu kwa kusema ukweli mara zote. Watu huwa wanatunza yale unayowasilisha, iwe ni kwa mazungumzo au maandishi. Wakati mwingine unapokuja kuwasilisha kitu kingine tofauti wanakuona siyo mwaminifu na hilo litapelekea kuwashawishi iwe vigumu.
Mara zote kuwa mwaminifu kwa kusema ukweli, utaondoa hali ya kutokuaminika inayoletwa pale mambo yako yanapokuwa yanatofautiana. Kumbuka kauli kwamba ukiwa mkweli huhitaji kukumbuka chochote na ukiwa mwongo inabidi uwe na kumbukumbu kubwa sana. Ukweli ni rahisi kuliko uongo.
SOMA; Tumia Shukrani Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
6. Ijue Biashara Yako.
Kuijua biashara kwa kina kunakupa hali ya kujiamini katika kuielezea kwa wengine na kujibu maswali pamoja na mapingamizi yao. Unapokuwa huijui vizuri biashara, unakuwa na ushawishi mdogo kwa wateja kwa sababu hawapati taarifa za kuwatosha kufanya maamuzi.
Hakikisha unajifunza na kuijua kwa kina biashara yako, jua maswali yote ambayo wateja huwa wanauliza na mapingamizi yote kuwa na majibu yake. Unapowasilisha kwa wateja, fanya hivyo kwa kujiamini na jibu maswali na mapingamizi kwa usahihi.
7. Tambua Lugha Ya Mwili.
Unapozungumza na watu, sehemu kubwa ya mawasiliano siyo maneno, bali miili yao. Lugha ya mwili ya mtu inaeleza mengi kuliko maneno anayokuwa anasema. Hivyo weka umakini kwenye kuwaangalia watu unapokuwa unazungumza nao. Angalia nyuso zao, mikono yao na mwili kwa ujumla. Mtu akiwa anatabasamu, amefungua mkono au kuinamia mbele, anakubaliana na wewe. Mtu akiwa hatabasamu, amefunga mikono au kuinamia nyuma, hakubaliani na wewe. Kuangalia lugha ya mwili inakusaidia kuchukua hatua sahihi ili kuhakikisha mawasiliano yanakamilika.
Weka umakini wako wote kwa watu unaokuwa unazungumza nao ili kuelewa lugha ya mwili. Hata kwa mazungumzo ya simu, ukiweka umakini wako kwa jinsi mtu anavyojibu, utaelewa lugha yao ya mwili kama wanakubaliana na wewe au la.
8. Boresha Mahusiano.
Mawasiliano yanakuwa rahisi na ya kueleweka pale mahusiano yanapokuwa bora. Kama watu hawakujui, ni vigumu sana kukupa umakini wako. Hivyo kila wakati boresha mahusiano yako na wateja, kwa kuwa na taarifa nyingi kuhusu wao na kuzitumia kupata umakini wao. Mfano kwa kujua tarehe ya mtu ya kuzaliwa na kumpa pongezi kwenye tarehe hiyo, itamfanya akupe umakini zaidi.
Pata taarifa nyingi kuhusu wateja wako na zitumie unapowasiliana nao ili kuboresha mahusiano. Mahusiano bora yanaleta kuelewana na ushawishi kuwa mzuri.
9. Kuwa Mnyenyekevu.
Kuna nyakati ambazo wateja wataonekana kuwa na uelewa mkubwa kuliko wewe, au kuna vitu ukawa hujui au huna uhakika navyo. Katika nyakati kama hizo unapaswa kuwa mnyenyekevu na kukubali yale madhaifu uliyonayo. Watu wanakukubali zaidi pale unapokubali madhaifu uliyonayo kuliko kujifanya huna madhaifu wakati yanaonekana wazi.
Pale madhaifu yako yanapokuwa wazi, yakiri kwa wateja au wale unaowasiliana nao. Hapo watajiona wakiwa na wajibu wa kukusaidia kwenye madhaifu hayo na hilo litafanya uwe na ushawishi zaidi kwao.
10. Kuwa Na Shauku.
Mawasiliano yoyote ambayo hayana shauku, hayana ushawishi. Pale mtu anapokuwa hana msukumo mkubwa kwenye kuwasilisha kile alichonacho, anawafanya wanaokipokea kuwa wamepoa na hivyo ushawishi kuwa mdogo.
Kuwa na shauku kubwa kwa kujikubali, kukubali na kupenda kile unachoelezea, kisha kieleze kwa msukumo mkubwa. Hilo litawafanya wale unaowaeleza kutaka kukusikiliza na hilo kuongeza ushawishi wako kwao.
Mawasiliano ni kiungo bora kwenye mauzo, fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kuboresha mawasiliano yako, uwe muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.