3436; Ya Msingi Kwanza.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanapenda kuhangaika na mambo makubwa na magumu, ambayo hata hawayaelewi, wakati yale ambayo ni rahisi na ya msingi kabisa hawayajui.
Mambo hayo makubwa na magumu huwa yanawasilishwa kwa namna ambayo yanasisimua sana.
Kwa kuwa watu wanapenda vitu vinavyosisimua, huwa wananasa kirahisi.
Mambo rahisi na ya msingi huwa hayana mbwembwe, hivyo hayasisimui.
Watu huwa wanachoshwa haraka na mambo ambayo ni ya kawaida.
Ambacho watu wanahitaji ili kupata matokeo ya uhakika kwenye maisha yao siyo hayo makubwa na magumu ya kusisimua, bali yale rahisi na ya msingi.
Mfano mzuri sana ni kwenye fedha na utajiri.
Kila siku watu wanakimbizana na njia za siri za kujenga utajiri.
Na huwa wanakutana na njia ngumu na za kusisimua za kujenga utajiri.
Mara nyingi wanakutana na aina ya uwekezaji ambapo mtu unaweka fedha halafu hujui nini kinaendelea, ila mwisho unavuna pesa nyingi sana.
Watu wananasa kwenye huo mpango wa kusisimua, ambao hata hawauelewi na matokeo yake ni huishia kupoteza.
Njia ya kujenga utajiri kwa uhakika ni rahisi na ya msingi kabisa, ambayo haina mbwembwe zozote.
Ni mtu kuwa na matumizi ambayo ni pungufu ya kipato, kufanya uwekezaji endelevu na kuepuka madeni.
Kila mtu anaweza kutumia njia hiyo na akajenga utajiri.
Lakini kwa sababu haina mbwembwe na kwa sababu inahitaji muda mrefu na kazi kubwa kuleta matokeo, watu hawahangaiki nayo kabisa.
Ni rahisi kuhangaika na vitu vya kusisimua ambavyo havifanyi kazi, kuliko vitu visivyosisimua lakini vinafanya kazi.
Kama bado hujaweza kufika ngazi ya kuvuka yale ya kusisimua na kwenda na yaliyo sahihi, hujakomaa vya kutosha kupata mafanikio ya uhakika.
Ili ukomae na kupata utulivu utakaokupa mafanikio unahitaji kujifunza kwa kina sana au kuumia sana kiasi cha kuamua kutulia na kutokuhangaika.
Kwa bahati mbaya wengi hawapo tayari kujifunza na hata wakiumia, bado wanaendelea kuamini kuna siri hawajaijua.
Hivyo wanaendelea kuumia maisha yao yote.
Kama umeweza kupata neema wa kuyaelewa haya ya msingi na kuyafanyia kazi, hongera, hiyo ni bahati nzuri sana kwako.
Lakini kama bado unakimbizana na siri zilizojificha zitakazokupa mafanikio ya haraka, pole, maana hakuna kitakachoweza kukusaidia.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe