Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye kipengele hiki cha #HadithiZaKocha ambapo nakushirikisha hadithi fupi za kale ambazo zina mafunzo mazuri sana kuhusu maisha.

Wajibu wako ni kusoma hadithi kwa utulivu kisha kushirikisha kwenye maoni hapo chini ni nini umejifunza kwenye hadithi na unaenda kutumiaje kile ulichojifunza kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Hapa tunapata hadithi ya Mbwa Mwitu na Mwanakondoo.

Mbwa mwitu alikuwa kwenye mto anakunywa maji, haikuwa siku nzuri sana kwake kwani alikuwa na njaa na hakuwa amepata chakula.

Muda mfupi baadaye alikuja mwanakondoo naye akawa anakunywa maji kwenye mto ule. Mbwa mwitu alijiambia tayari amepata chakula kizuri. Ila akawa anajiuliza atumie sababu gani ili aweze kumla yule mwanakondoo.

Baada ya kufikiri kwa muda, mbwa mwitu alipata jibu ambalo aliona ni sababu nzuri. Mazungumzo yao yalienda hivi;

Mbwa mwitu; “Wewe mwanakondoo kwa nini unachafua maji ambayo nakunywa?”

Mwanakondoo; “Hapana bwana mkubwa, mimi nipo chini yako, maji yanatoka kwako kuja kwangu, siwezi kuwa nimeyachafua mimi.”

Mbwa mwitu alifikiria na kuona jibu la mwanakondoo ni la kweli. Lakini bado alitaka sababu ya kumla mwanakondoo yule. Alifikiri kidogo na kupata sababu nyingine.

Mbwa mwitu; “Nimekumbuka, mwaka jana kipindi kama hiki ulinitukana.”

Mwanakondoo; “Hapana bwana mkubwa, mimi nina miezi sita tu sasa, siwezi kuwa nilikutukana mwaka mmoja uliopita.”

Mbwa mwitu; “Basi kama siyo wewe ni baba yako.”

Pale pale mbwa mwitu akamrukia mwanakondoo na kumla.

Mwisho wa hadithi yetu fupi.

Rafiki, tafakari kwa kina kisha sehemu ya maoni hapo chini shirikisha nini umejifunza kwenye kisa hicho na unaenda kutumiaje hayo uliyojifunza. Karibu ushirikishe na kujifunza kwa wengine.

Nimehadithia kisa hiki kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini, unaweza kukiangalia na ukajifunza na kuweka maoni yako. Karibu.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.