Rafiki yangu mpendwa,

Kila kitu kwenye maisha huwa kina misingi yake, ambayo inapaswa kufuatwa ili matokeo mazuri yaweze kupatikana.

Inapokuja kwenye fedha, watu wengi hawana misingi sahihi, badala yake huwa wanafuata mazoea ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu.

Tatizo kubwa ni mazoea hayo huwa siyo sahihi, kwa sababu yamezalisha watu wenye changamoto nyingi kifedha.

Ukiangalia umasikini ambao watu wengi wanao, licha ya kuwa na njia za kuingiza kipato, huwa unatokana na mazoea ya PATA PESA, TUMIA PESA. Hicho ndiyo kitu pekee ambacho watu wamezoea kwenye fedha na imekuwa sababu ya kuwepo kwa umasikini.

Ili kuondokana na tatizo hilo la mazoea yanayozalisha umasikini, kuna misingi mitano ambayo inapaswa kufuatwa mara zote.

Uzuri wa misingi hiyo ni huwa haibadiliki, ipo hivyo nyakati zote na kwa watu wote. Ni misingi inayomfaa kila mtu na kila wakati. Karibu uijue na kuitumia kwa mafanikio.

Msingi wa kwanza; KIPATO ENDELEVU.

Msingi wa kwanza na muhimu kwenye kujenga utajiri ni kuwa na kipato. Kipato ndiyo chanzo cha mambo yote kwenye maisha.

Kila mtu mwenye kipato, anaweza kujenga utajiri, bila ya kujali kipato chake ni kiasi gani. Kama mtu akifuata vizuri misingi mingine, utajiri unakuwa ni uhakika.

Kwenye eneo la kipato, haitoshi tu kuwa kipato, bali pia kinapaswa kuwa endelevu. Yaani kipato ambacho kinaendelea kuwepo na kuendelea kukua pia. Kuna watu huwa wanakuwa na vipato visivyo vya uhakika na hivyo misingi mingine haiwezi kufanya kazi.

Msingi wa pili; DHIBITI MATUMIZI.

Kipato pekee hakitaweza kumpa mtu utajiri kama hataweza kudhibiti matumizi yake. Na kama ambavyo tayari tumeshaona, mazoea ambayo wengi tunayo ni pata pesa, tumia pesa. Hapo ndipo umasikini ambao watu wanao unapotengenezwa, kwa sababu wakipata pesa hawafikirii kitu kingine chochote isipokuwa kutumia.

Na ndiyo maana kipato hakijawahi kutosheleza, kwa sababu matumizi ya kipato huwa hayaishi. Pale kipato kinapoongezeka, matumizi nayo yamekuwa yanaongezeka.

Hivyo msingi wa pili kwenye kujenga utajiri ni KUDHIBITI MATUMIZI. Hapa unapaswa kufuata kanuni moja tu, MATUMIZI YASIZIDI KIPATO. Ukiweza kanuni hiyo umeishinda vita.

Unachopaswa kuhakikisha ni matumizi unayokuwa nayo hayazidi kipato chako. Ishi chini ya kipato chako na kama hiyo haitoshelezi matumizi yako basi unachopaswa kufanya ni kuongeza kipato kwanza na siyo kuwa na matumizi yanayozidi kipato.

Dhibiti matumizi yako ili uweze kujenga utajiri kwenye maisha yako.

SOMA; Ngazi Ya Juu Ya Usimamizi Wa Kujenga Utajiri; Staafu Na Uhuru Wa Kifedha.

Msingi wa tatu; ONDOKA KWENYE MADENI.

Madeni ndiyo kaburi la utajiri. Huwezi kujenga utajiri ukiwa na madeni, hasa madeni binafsi ambayo hayana uzalishaji. Hiyo ni kwa sababu madeni huwa yanakuwa na riba ambazo unatozwa na hizo ni fedha unazotoa ambazo hujazizalisha.

Msingi huu wa tatu ni muhimu, kama upo kwenye madeni ya aina yoyote ile, unapaswa kuondoka kwenye madeni hayo kabla ya kuendelea na hatua nyingine zozote.

Kwa sababu hata ukikazana kuweka akiba na kufanya uwekezaji, kama una madeni ambayo unalipa kwa riba, ni kazi bure. Unazidi kupoteza fedha nyingi kwenye riba unazokuwa unalipa.

Ndiyo maana unapaswa kuondoka kwenye madeni na ukishaondoka au kama bado hujaingia, kujizuia usiingie tena kwenye madeni. Na pale utakapofuata hatua hizi, hutaweza kurudi tena kwenye madeni.

Msingi wa nne; WEKA AKIBA.

Pale matumizi yanapokuwa pungufu ya kipato, kinachobaki unakiweka akiba. Akiba inakuwa ya malengo mbalimbali unayokuwa nayo.

Unapaswa kuwa na akiba ya dharura ambayo utaitumia pale unapopata dharura.

Unapaswa kuwa na akiba ya maendeleo unayotaka kufanya ili kukusanya fedha hizo.

Na pia unapaswa kuwa na akiba ya uwekezaji ambayo itaenda kwenye msingi wa tano.

Muhimu ni unapoweka akiba uwe na mpango kabisa ili isije ikamezwa na matumizi ambayo huwa ni rahisi sana kujitokeza.

Msingi wa tano; FANYA UWEKEZAJI.

Kuweka akiba peke yake haikutoshi kujenga utajiri kwenye maisha yako. Hiyo ni kwa sababu akiba ni fedha inayokaa tu bila kufanya chochote. Fedha inapokaa tu inapoteza thamani yake kutokana na mfumuko wa bei ambao unakuwa unaendelea.

Hivyo kwenye kujenga utajiri, uwekezaji ni muhimu kufanyika. Uwekezaji ni kuifanya fedha ikufanyie kazi. Hapo fedha inaingia kwenye shughuli za uzalishaji bila ya wewe kuhusika moja kwa moja. Fedha yako inafanya kazi na kukuingizia wewe faida.

Uwekezaji ndiyo njia ya kujenga na kutunza utajiri. Kila anayetaka kufikia utajiri na uhuru wa kifedha ni lazima afanye uwekezaji. Na uwekezaji huwa na manufaa makubwa pale unapofanyika kwa muda mrefu, hivyo kuanza mapema na kuwekeza kwa msimamo bila kuvuruga ina manufaa makubwa.

Rafiki, hiyo ndiyo misingi mitano ya kifedha isiyobadilika ambayo ukiweza kuifanyia kazi kwa uhakika, lazima utajenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeielezea misingi hii kwa kina na hatua za kuchukua ili uweze kuitumia kujenga utajiri mkubwa. Karibu ujifunze ili uelewe kwa kina na kuchukua hatua kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.