Rafiki yangu mpendwa,
Tarehe 28 Mei huwa ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu. Kwenye siku hiyo huwa napata nafasi ya kuyatafakari maisha yangu kwa kuangalia nilikotoka, nilipo na kule ninakotaka kufika.
Nimekuwa nakushirikisha malengo yangu makubwa mawili ambayo ni UBILIONEA na URAISI. Nitakuwa BILIONEA na nitakuwa RAISI wa Tanzania. Haya sina wasiwasi nayo kwa sababu nayapambania kwa kila sekunde ninayokuwa hai.
Katika tafakari ya kukumbuka kuzaliwa kwangu, huwa naanza kwa kukushukuru sana wewe rafiki yangu ambaye umekuwa ndiyo chachu ya mimi kufanya ninachofanya.
Kusudi la maisha yangu ni kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia yale ninayofanya. Uwepo wako wewe ambaye unanifuatilia kwenye maarifa ninayoshirikisha, umekuwa na mchango mkubwa.

Lakini pia falsafa kuu inayoniongoza kwenye maisha yangu ni NINAWEZA KUPATA CHOCHOTE NINACHOTAKA, KAMA NITAWASAIDIA WATU WENGI ZAIDI KUPATA KILE WANACHOTAKA.
SOMA; Lengo Langu Kubwa Kwenye Maisha; Kuwa Rais wa Tanzania.
Hapo ndipo umuhimu wako unapokuja rafiki yangu. Nataka nikusaidie wewe upate unachotaka, ili na mimi nipate UBILIONEA NA URAISI. Kukusaidia kwangu ni kupitia kukupa MAARIFA SAHIHI na USIMAMIZI BORA wa kuyafanyia kazi maarifa hayo ili upate kwa uhakika kile unachotaka.
Rafiki, kitu kingine ambacho nimekuwa nafanyia kazi ili kuhakikisha natoa mchango mkubwa kwa watu wengine ni lengo langu la KUISHI MIAKA 100 YA AFYA. Hili ni lengo ambalo nimekuwa nalifanyia kazi kila siku kuhakikisha nalifikia. Na kwa sababu wewe ni rafiki yangu, napenda na wewe ulifikie pia.
Katika kujifunza namna ya kufikia lengo hilo, nilitafuta watu ambao wamelifikia, wakiwa na mafanikio ya utajiri na kuweza kuishi miaka 100. Nilimpata mtu mmoja ambaye niliona anafaa kuwa mfano mzuri kwangu.
Mtu huyo ni Charlie Munger ambaye alikuwa bilionea mwekezaji na mshirika wa Warren Buffet. Alifariki dunia akiwa na miaka 99 na miezi 11, kwenye rekodi zangu nahesabu ni miaka 100 tu hiyo.

Kupitia ushauri mbalimbali ambao Charlie Munger alikuwa akitoa kipindi cha uhai wake, niliweza kupata vitu 10 ambavyo anasema vimemwezesha kuishi miaka mingi na maisha ya mafanikio.
Hapa nimekushirikisha sheria hizo 10 ili na wewe uziishi na kunufaika. Karibu sana ujifunze.
1. Usiwe na wivu; pale unapokutana na waliopiga hatua kuliko wewe, wafurahie na jifunze kutoka kwao ili na wewe uweze kupiga hatua kama wao.
2. Usiwe na chuki; kumchukia mtu ni sawa na kunywa sumu wewe ili kumdhuru yeye, unaishia kudhurika mwenyewe.
3. Usitumie zaidi ya kipato chako; ongeza kipato chako, punguza matumizi, weka akiba na fanya uwekezaji.
4. Kuwa na shauku bila ya kujali kinachoendelea kwenye maisha yako; hata kama unapitia magumu, endelea kuwa na shauku kwa sababu ina nguvu ya kukupa matokeo mazuri yatakayokutoa popote unapoweza kuwa umekwama.
5. Jihusishe na watu wanaoaminika; watu ambao wanatimiza wanayoahidi na kufanya kilicho sahihi mara zote.
SOMA; Muongo Wa Kuwa Bilionea, Karibu Tusafiri Pamoja.
6. Fanya kile unachopaswa kufanya ili kuwa mtu unayeweza kuaminika na wengine; timiza yale unayoahidi na mara zote fanya kilicho sahihi.
7. Imalize kila siku ukiwa bora kuliko ulivyoianza; kila siku jifunze kitu kipya, siku zako mbili zisifanane.
8. Jua ni wapi ukienda utakufa na usiende hapo; epuka makosa ambayo yatakuondoa kwenye safari uliyopo ili ubaki kwenye safari hiyo kwa muda mrefu zaidi, maana ushindi ni kudumu kwenye safari kwa muda mrefu zaidi.
9. Badala ya kuhangaika kutumia sana akili, epuka kuwa mpumbavu; huhitaji akili nyingi ili kufanikiwa kwenye maisha, unahitaji tu usiwe mpumbavu kwa kurudia makosa yako mwenyewe au ya wengine.
10. Jua eneo lako la ustadi/ubobezi na usifanye maamuzi nje ya eneo hilo; usijifanye mjuaji wa kila kitu chagua eneo ambalo unabobea na hangaika na hilo, mengine achana nayo.
Hizo ndizo sheria 10 ambazo tukizizingatia tunaweza kuwa na maisha marefu na yenye mafanikio makubwa.
Kama ilivyo kanuni yetu, MAARIFA + VITENDO = MAFANIKIO, hapa umeshayapata MAARIFA, wajibu wako ni kuyaweka kwenye VITENDO na kupata matokeo mazuri.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeeleza sheria hizo 10 na jinsi ya kuziishi kwenye maisha yako ili kuishi miaka mingi. Karibu ujifunze na kuchukua hatua.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.