3441; Unapata unachotaka.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kimoja kuhusu maisha ni kwamba, kila mtu huwa anaishia kupata kile anachotaka.
Kile ambacho watu wanakipigania kweli ili kitokee, ndiyo kinachotokea kwenye maisha yao.
Inaweza kuchukua muda mrefu kwa matokeo kuonekana, lakini huwa yanatokea tu.
Pia watu wanaweza kusahau nini wamekuwa wanataka, hivyo wanapopata, wanashangaa na kulalamika.
Wasijue kwamba muda wote hicho ndiyo kitu wamekuwa wanakitaka zaidi.
Hiyo ndiyo sababu wanaofanikiwa wamekuwa wanaendelea kufanikiwa, huku wanaoshindwa wakiendelea kushindwa.
Wanaoshinda huwa wanakazana kujaribu kila kitu wanachoweza kufanya kuthibitisha kwamba inaweza kufanya kazi kwao.
Kwa juhudi hizo wanazoweka, wanaishia kupata matokeo mazuri na ya ushindi.
Wanaoshindwa huwa wanakazana kutoa kila aina ya sababu na visingizio kwa nini kitu hakiwezi kufanya kazi kwa upande wao.
Kwa sababu na visingizio hivyo vingi wanavyotoa, wanaishia kupata matokeo mabaya ya kushindwa.
Mwisho wa yote, kila mtu anakuwa sahihi.
Anayekazana kuonyesha inawezekana inawezekana kweli.
Na anayekazana kuonyesha haiwezekani, haiwezekani kweli.
Hakuna muujiza wowote hapo isipokuwa tu ni kila mtu kupata kile anachotaka zaidi.
Kwa matokeo yoyote unayopata sasa na huyataki, anza kwa kujiuliza kwa nini ulitaka yawe hivyo na nini ulifanya au kutofanya mpaka ukaishia na matokeo hayo.
Kwa kuanzia hapo inakuwa rahisi kubadili matokeo unayopata sasa na kupata yale unayokuwa unayataka hasa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe