Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Fedha ni kitu muhimu kwenye maisha ya kila mtu. Fedha ndiyo inayotuwezesha kupata mahitaji yote muhimu kwenye maisha yetu. Na pia fedha ni moja ya vitu vinavyotusukuma kufanya kazi tunazofanya.
Usimamizi wa fedha binafsi ni muhimu kwa kila mtu kufanyia kazi. Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa hawafundishwi. Na hilo limekuwa linapelekea watu kuwa na maisha ya mateso licha ya kufanya sana kazi.
Ili kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, unapaswa kuwa na utulivu mkubwa kwenye kazi yako ya mauzo. Na ili uweze kuwa na utulivu mkubwa kwenye kazi ya mauzo, unapaswa kuwa na USIMAMIZI MZURI WA FEDHA ZAKO.

Kwenye USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI, kuna mambo matano unayopaswa kuyafanyia kazi ili upate utulivu wa kufanya shughuli zako kwa viwango vya juu. Karibu ujifunze mambo hayo matano na kuyafanyia kazi ili uwe bora binafsi, kwenye mauzo na uuze sana.
MOJA; KIPATO ENDELEVU.
Kuwa na kipato endelevu ndiyo hatua ya kwanza kwenye usimamizi wa fedha binafsi. Kwa bahati nzuri sana, tayari wewe una kipato kupitia kazi ya mauzo. Unachohitaji kufanyia kazi ni kukuza kipato chako na kukifanya kuwa endelevu. Kitu ambacho una bahati nzuri kuwa kwenye mauzo, kwa sababu ukiweza kuuza zaidi, hata kipato chako kitaongezeka zaidi kupitia mpango wa bonasi na kamisheni.
Hatua ya kuchukua; kila mara jisukume kukaa kwenye mchakato wa mauzo ili ufanye mauzo makubwa na kuwa na kipato endelevu na kinachokua.
MBILI; DHIBITI MATUMIZI.
Kuwa na kipato ni hatua muhimu, lakini kama matumizi hayatadhibitiwa, kipato hakiwezi kutosha. Watu wengu huwa wanatumia kipato chote mpaka kinaisha na kwenda hatua ya ziada kwa kukopa. Wewe usiwe hivyo, hakikisha matumizi yako hayazidi kipato unachoingiza. Haijalishi kipato chako ni kidogo kiasi gani, yapange maisha yako kwa namna ambayo matumizi yatakuwa chini ya kipato hicho. Na kama una mahitaji zaidi ya msingi, rudi kwenye hatua ya kwanza na upambane kuongeza zaidi kipato chako.
Hatua ya kuchukua; hakikisha matumizi yako hayazidi kipato unachoingiza. Panga bajeti ya kipato unachoingiza na fuata bajeti hiyo bila kuivunja.
TATU; ONDOKA KWENYE MADENI.
Madeni ni kikwazo kikubwa sana kwenye eneo la FEDHA BINAFSI. Madeni yanakunyima amani na kukukosesha utulivu kwenye kazi yako ya mauzo. Unapokuwa na madeni unakuwa mtumwa kwa wale wanaokudai na hilo linakuathiri kwenye kila unachofanya. Ili ufanye chochote vizuri, lazima akili yako iwe huru. Na akili yako itakuwa huru kama hutakuwa na madeni. Kama tayari una madeni, weka mpango wa kuyalipa. Na kama bado hujaingia kwenye madeni, jizuie usiingie.
Hatua ya kuchukua; ondoka kwenye madeni yote uliyonayo na jizuie usiingie tena kwenye madeni.
SOMA; Zungukwa Na Watu Sahihi Ili Uweze Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
NNE; WEKA AKIBA.
Kwa kila kipato unachoingiza, ukishaweza kuwa na matumizi ambayo ni chini ya kipato hicho, unapaswa kuweka pembeni akiba. Akiba hiyo inakuwa kwa malengo maalumu unayokuwa nayo kwenye maisha yako na unaiweka mahali ambapo huwezi kushawishika kuitumia. Kuwa na akiba ya dharura ili inapotokea usijikute kwenye madeni. Pia kwa yote unayopanga kufanya siku za mbeleni, yawekee akiba.
Hatua ya kuchukua; kuwa na akaunti maalumu ambayo unaweka akiba zako na hakikisha huwezi kuzitoa kirahisi.
TANO; FANYA UWEKEZAJI.
Uwekezaji ni kuifanya fedha yako ikufanyie kazi na kukuingizia faida hata kama umelala. Kwa sasa una nguvu za kufanya kazi ya mauzo, ila miaka inavyokwenda utafika umri ambao huwezi kufanya tena kama unavyofanya sasa. Kwenye huo umri bado utakuwa na matumizi ya kuendesha maisha na hapo ndipo unapohitaji kuwa na uwekezaji unaokuzalishia. Ukianza kufanya uwekezaji sasa, miaka 10, 20 mpaka 30 ijayo utakuwa umefanya uwekezaji mkubwa wa kukuwezesha kuishi maisha hata kama huna kipato cha moja kwa moja.
Hatua ya kuchukua; fanya uwekezaji kwenye kila kipato unachoingiza, kwa kutumia mifuko ya pamoja kama ya UTT AMIS.
Muuzaji bora kuwahi kutokea, pata utulivu kwenye eneo la fedha kwa kuwa na USIMAMIZI MZURI WA FEDHA BINAFSI. Fanyia kazi mambo haya matano uliyojifunza hapa na utaweza kupata utulivu wa kufanya kazi yako ya mauzo kwa viwango vya juu kabisa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.