Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Hii ni programu maalumu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri na kufikia uhuru wa kifedha.
Kwenye NGUVU YA BUKU tunawekeza kiasi chochote tunachoweza ambacho hakipungui Tsh elfu 1 kwa siku, fedha ambayo kila mtu huwa anapoteza kwenye siku yake.
Kwenye UHURU WA KIFEDHA, tunawekeza nusu ya kipato tunachoingiza ili kufikia uhuru wa kifedha ndani ya miaka 10 mpaka 15.
Ili kuweza kuwekeza nusu ya kipato, kuna mambo mawili ya kufanya; kupunguza sana gharama za maisha na kuongeza sana kipato. Tunayafanyia kazi yote mawili ili tufanikishe kwa uhakika.

Kwenye kuongeza kipato, tumejifunza kufanya mauzo zaidi ambapo ni sehemu rahisi kwa kila mtu kuanzia. Kama umeajiriwa, tafuta kitu unachoweza kuuza nje ya ajira yako. Na kama upo kwenye biashara, kuza mauzo zaidi.
SOMA; Jinsi Ya Kufikia Uhuru Wa Kifedha Ndani Ya Miaka 15 Kwa Uwekezaji Mdogo.
Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza sifa 9 za kuangalia kwenye njia za kuongeza kipato unazofanyia kazi ili kufikia uhuru wa kifedha.
Ili njia za kuongeza kipato unazofanyia kazi zikupe uhuru wa kweli, lazima ziwe na sifa fulani. Ukichukua njia ni njia tu, unajikuta unaishia kwenye utumwa zaidi. Kwa mfano kama umeajiriwa, halafu utatumia njia ya ajira nyingine ya muda (part time) kuongeza kipato, ni kuzidi kujiweka kwenye gereza na kujinyima uhuru.
Ili uwe huru kweli, fanyia kazi njia za kuingiza kipato zenye sifa hizi tisa.
1. Mifereji mingi ya kipato.
Njia unayotumia inatakiwa kuwa na mifereji mingi ya kipato, kama unauza, basi wateja wanaonunua wawe wengi. Epuka njia ambazo wanaokulipa ni wachache, kwani hao wanakugeuza kuwa mtumwa wao.
2. Upekee.
Njia unayotumia inapaswa kuwa na upekee ambao utakuwezesha kukabiliana na ushindani ambao upo kila mahali. Lazima uwe na kitu ambacho watu wanakipata kwako na hawawezi kukipata mahali pengine. Hicho ndiyo kinakupa nguvu ya ushindani.
3. Gharama ndogo ya kuanza.
Njia unayotumia iwe unaanza na gharama kidogo au bila gharama kabisa. Huhitaji kuwekeza fedha nyingi kwenye kuanzisha kipato cha ziada. Hilo linakufanya usikwame kwa sababu maarufu ambayo watu huwa wanaitumia kwamba hawana mtaji. Fanya kitu ambacho kinahitaji mtaji kidogo au hakihitaji mtaji kabisa.
4. Kutohitaji wafanyakazi.
Njia ya kipato cha ziada unayofanyia kazi inapaswa kuwa haihitaji wafanyakazi. Kusimamia wafanyakazi ni kazi ngumu ambayo inahitaji muda wako mwingi. Kwa njia ya pembeni ya kuingiza kipato, huna muda wa kutosha kusimamia wafanyakazi. Hivyo chagua njia ambayo haihitaji wafanyakazi.
5. Faida kubwa.
Njia unayotumia inapaswa kukupa faida kubwa kulingana na muda na juhudi unazoweka. Faida inapaswa kuwa ya wazi na isiyokuwa na mlolongo mrefu kuweza kuonekana.
SOMA; Kipato Unachopaswa Kuongeza Ili Kufikia Uhuru Wa Kifedha Ndani Ya Miaka 15.
6. Kwenda na wakati.
Njia unayotumia inapaswa kwenda na wakati, yaani vitu ambavyo vina umaarufu au vinavuma kwa kipindi husika. Huhitaji kufanya kitu ambacho unatakiwa kuwashawishi watu wakielewe. Anza na kitu ambacho tayari watu wanakielewa na wanakitaka, ila wamekuwa hawakipati vizuri. Wewe unawapatia vizuri na wananunua. Kwa lugha nyingine uza kile ambacho tayari watu wana uhitaji nacho badala ya kile ambacho inabidi uwashawishi kuwa wanakihitaji.
7. Kipato cha kujirudia.
Kipato huwa ni cha aina mbili, cha mara moja (unalipwa mara moja baada ya kazi) na kipato cha kujirudia (unafanya kazi mara moja na kulipwa kwa kujirudia rudia). Njia unayochagua wewe inapaswa kuwa ya kipato cha kujirudia rudia, yaani unafanya kazi mara moja na kulipwa kwa uendelevu bila ya kufanya kazi ya ziada.
8. Mahitaji muhimu ya kila siku kwa kila mtu.
Njia ya kipato unayochagua inapaswa kulenga kuuza kitu ambacho ni mahitaji muhimu ya kila siku ambayo kila mtu anayo. Kwa njia hiyo unakuwa na uhakika wa wateja kwa sababu ya umuhimu wake kwa wengi na kuhitajika kwake kwa kila siku.
9. Shauku kubwa.
Njia ya kuingiza kipato unayotumia inapaswa kuwa ambayo una shauku kubwa kwenye kuifanyia kazi. Yaani iwe njia ambayo unafanya kile unachopenda na una msukumo mkubwa ndani yako wa kufanya kwa ukubwa na upekee. Njia unayotumia haipaswi kuwa ya mtu kukusukuma kufanya, bali tayari una msukumo mkubwa ndani yako na unafanya kuliko wengine wote.
Kwa kuzingatia haya tisa kwenye kuchagua njia ya kuongeza kipato unayofanyia kazi, utaweza kuongeza kipato chako kwa ukubwa na kufanya uwekezaji mkubwa. Hilo litakuwezesha kufikia uhuru wa kifedha mapema na kuwa na maisha huru.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili ushirikishe yale uliyojifunza kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Kwa walioajiriwa, chambua njia ya kuingiza kipato uliyochagua kwa vigezo hivyo 9?
2. Kwa wanaofanya biashara, chambua biashara yako kwa vigezo hivyo 9 na uone wapi unahitaji kuboresha ili kukuza zaidi kipato?
3. Kama ungekuwa huru kuchagua kitu kimoja cha kuuza, kwa maana kwamba usingekuwa na kikwazo chochote kinachokuzuia, ungechagua kuuza nini? Chambua hicho ulichochagua kwa vigezo hivyo 9.
4. Ni hatua gani unaweza kuchukua ili hicho ulichochagua kwenye namba 3 uweze kukifanya kwa uhalisia?
5. Karibu kwa maswali, maoni na mapendekezo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.