3444; Utapitwa tu.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Hofu ya kupitwa imekuwa ndiyo kitu kinacholeta upotevu wa muda na umakini kwa wati wengi zaidi.

Watu wanajikuta wakitumia muda wao mwingi kufuatilia yale yanayokuwa yanaendelea.
Wanakuwa wanahofia kwamba kama hawatafuatilia kila kinachoendelea kwa wakati ambao kinaendelea basi kuna mambo mazuri yatawapita.

Hiyo hofu ya kupitwa na mambo mazuri ndiyo imepelekea watu kuganda kwenye yale yanayokuwa yanaendelea hata kama hayana tija kwao.
Watu wanajikuta wakitaka kujua kila kinachoendelea kwenye wakati husika ili wasipitwe na fursa nzuri zinazoweza kujitokeza.

Kwa jinsi zama tulizopo zilivyo, kila mmoja wetu anapitwa.
Hiyo ni kwa sababu mambo ni mengi sana na yanatokea kwa kasi kubwa mno.
Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuchakata mambo yote na kuyafanyia maamuzi maalumu.

Ukitaka kujua mambo mengi tu yanakupita bila hata kujua, rudi nyuma mwaka mmoja.
Fikiria tarehe kama ya leo mwaka mmoja uliopita, kisha jibu maswali yafuatayo;

Ni taarifa zipi muhimu sana ambazo ulikuwa unajiambia huwezi kukubali zikupite?
Ni fursa gani za kipekee ulizopata kwenye hiyo siku?
Mambo gani muhimu uliyokamilisha kwenye hiyo siku?
Ni matokeo gani yaliyopatikana na yapi yalikuwa manufaa yake?

Rafiki, majibu ya maswali hayo machache na ya msingi kabisa yatakuonyesha wazi kwamba mambo mengi yanatupita.

Vitu pekee ambavyo utakuwa unavikumbuka baada ya muda kupita ni vile ambavyo ni muhimu zaidi.
Na hivyo ni vichache mno.

Hilo linafanya mahangaiko tunayokuwa nayo ili kutokupitwa na yote yanayoendelea, kuwa ni zoezi la upotevu wa muda na umakini.

Hupaswi kuendelea kupoteza muda na umakini wako kwa sababu hutaki kupitwa.
Tambua kwamba mambo yote muhimu utayapata na kuyafanyia kazi bila hata kuhangaika na yale yanayoendelea.

Linda sana muda na umakini wako, peleka maeneo yenye tija kwako na siyo kupotezwa na hofu ya kupitwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe