Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya KUMI NA MOJA ambayo ni WEKA IGIZO.
Na kwenye kanuni ya KUMI NA MOJA tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni; kama unataka kuwashawishi watu wakubaliane na wewe, tumia maigizo yanayogusa hisia zao moja kwa moja.
Kwa kila unachotaka kuwashawishi wengine, tafuta tendo ambalo litagusa hisia zao na lifanye kwani matendo yana nguvu kuliko maneno matupu.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Kumi Na Moja
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya KUMI na MBILI ambayo ni WAPE WATU CHANGAMOTO.
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Mwandishi Dale Carnegie anatuambia kama njia nyingine zote za kuwashawishi watu zitashindwa kuzalisha matokeo tunayotaka, basi kuna njia ya mwisho ambayo ni ya uhakika itakapotumiwa vizuri.
Njia hiyo ni kuwapa watu changamoto, kuwapa shindano ambalo linawasukuma kufanya zaidi.

Kama tulivyojifunza, sisi binadamu huwa tunajithamini zaidi sisi wenyewe na hivyo huwa tunapenda wengine watuthamini pia.
Inapotokea tumepewa changamoto fulani, huwa tunapambana kuitatua ili kuonesha umuhimu wetu.
Dale Carnegie anatushirikisha mfano kutoka kwa Charles Schwab aliyekuwa mkurugenzi wa kiwanda cha chuma. Kulikuwa na changamoto ya uzalishaji wa chuma kwenye moja ya viwanda vyake na walijaribu kila njia kuwapa watu motisha ya kuongeza uzalishaji lakini njia hizo hazikufanya kazi.
Siku moja Schwab alitembelea kiwanda hicho wakati watu wa zamu ya mchana walikuwa wanatoka, akawauliza, wamezalisha tani ngapi za chuma, wakamjibu sita.
Akachukua chaki na kuandika namba sita kwenye mlango wa kuingia.
Watu wa zamu ya usiku walipoingia waliuliza namba sita ni ya nini ? Wakajibiwa bosi aliuliza tumezalisha tani ngapi tukamjibu sita, na akaandika namba hiyo.
Watu wa zamu ya usiku walijituma sana kweli ili washinde namba ile, na ilipofika asubuhi wakati wanatoka, walifuta namba sita na kuandika 7 ambacho ni kiasi walichozalisha.
Watu wa zamu ya asubuhi walipokuja na kuona 7, walijituma zaidi na zamu ilipoisha waliandika namba 8.
Hali ilienda hivyo mpaka kufikia zaidi ya 10 kwa kila zamu.
Hivyo basi, uzalishaji ukawa umeongezeka zaidi ya mara mbili kwa kufanya kitu kidogo tu, ambacho ni kuwapa watu changamoto.
Kwenye biashara unayofanya wape wateja wako changamoto ya kufanya manunuzi makubwa. Wape namba kwamba atakayefikia manunuzi ya kiasi fulani kwenye biashara, atapata zawadi fulani.
Utashangaa watu watakapopambania kufanya manunuzi makubwa. Kwa mfano, moja ya biashara ambayo iko kwenye CHUO CHA MAUZO na BILIONEA MAFUNZONI ya Singo parts spare wanafanya hivyo na wateja wa jumla huwa wanapambania kununu zaidi ili tu wafikie kuwa na manunuzi makubwa na mwisho wa siku kupata zawadi.
Tumejifunza watu wanapenda ushindani, hivyo wape changamoto na watakuwa tayari kukupa matokeo unayoyataka kuyaona kutoka kwao.
Watu huwa wanapenda ushindi, hivyo basi, unapotaka kuwashawishi wakubaliane na wewe au wabadilike, tafuta kitu kinachowaweka katika hali ya kushindana na watashindana ili kushinda.
Hata kama hakuna zawadi kubwa, kitendo cha kushinda kinamfanya mtu ajisikie vizuri.
Kwenye mazingira yoyote ya kazi, kama unataka kuwashawishi au kuwabadili watu, igeuze kazi kuwa mchezo ambapo watu kuna kitu wanashindania.
Hapo watu watajikuta kweli kweli kuhakikisha wanashinda.
Mwisho, nia ya ushindi ndiyo kitu pekee kinachowasukuma watu kupenda michezo mbalimbali na hata kushiriki kwenye bahati nasibu au kamari.
Weka hali ya ushindani kwenye kile unachotaka kuwashawishi watu na watakuwa tayari kukifanya.
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504