3449; Mashindi ni mshindwa aliyekataa kushindwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Tumekuwa tunawaangalia wale waliopata ushindi na mafanikio kama vile walipata nafasi ya kipekee ambayo wengine hawajapata.
Tunaona kama njia yao ilikuwa rahisi kuliko njia ambazo sisi tunapita.
Pale tunapochukua hatua na kushindwa, tunaona sisi kuna namna hatupo kama wale walioshinda, au hatuna bahati kama zao.
Ni bahati mbaya sana huwa hatuyaoni maisha ya washindi wengi kabla hawajashinda.
Tunakuja kuwaona pale wanapokuwa wamepata ushindi.
Lakini nyuma ya kila ushindi kumekuwa na kushindwa sana.
Wale wanaoshinda huwa wameshindwa kuliko walioshindwa.
Rudia kusoma taratibu ili izame vizuri ndani yako. WALIOSHINDA WANAKUWA WAMESHINDWA MARA NYINGI KULIKO WALIOSHINDWA.
Hiyo ni kwa sababu, wanaoshindwa huwa wanakuwa wameacha pale tu wanaposhindwa. Yaani wanakata tamaa haraka na kuacha.
Lakini wanaoshinda, huwa wanaendelea hata baada ya kushindwa. Wanaposhindwa huwa hawakubali kubaki chini, badala yake wanainuka na kuendelea tena.
Kwa kukataa kushindwa, wanaishia kushinda.
Haijalishi umeshindwa kiasi gani, kama utakataa kukubaliana na kushindwa, lazima utashinda.
Hakuna upekee wowote ambao walioshinda wanao, zaidi ya kukataa kushindwa.
Wanakataa kata kata kushindwa, kitu ambacho kinawapa ushindi kwa uhakika.
Kataa kushindwa na ushindi utakuwa wako kwa uhakika.
Ukishachagua eneo ambalo unataka ushindi, endelea kulifanyia kazi mpaka upate ushindi unaoutaka.
Usikubali kukwamishwa na kitu chochote kile.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe