MAUZO NDIO MOYO WA BIASHARA
Huwa napenda kufananisha biashara na mwili wa binadamu. Ambapo mzunguko wa fedha kwenye biashara huwa naufananisha na mzunguko wa damu kwenye mwili wa binadamu.
Mfumo wa upumuaji huwa naufananisha na masoko. Pumzi ni muhimu, bila hiyo mtu anakufa. Lakini damu pia ni muhimu, maana hiyo ndiyo inasambaza pumzi na virutubisho kwenye mwili.
Kiungo kikuu kinachosukuma damu kwenye mwili ni moyo. Hivyo inapokuja kwenye biashara, ambapo damu ni mzunguko wa fedha, moyo wa biashara ni mauzo. Ni kupitia mauzo ndiyo fedha zinaingia kwenye biashara. Kama hakuna mauzo, hakuna biashara. Haijalishi una bidhaa au huduma bora kiasi gani, kama hakuna watu wanaonunua hakuna biashara. Hata kama watu wanakusifia biashara yako ni nzuri, vitu vyako ni bora, kama hakuna anayetoa fedha kununua, hapo hakuna biashara.
Kuna mengi muhimu kwenye biashara, lakini yote yanategemea kitu kimoja kikubwa; MAUZO. Ni kama ulivyo mwili wa binadamu, mtu anapokufa siyo kwamba anakuwa hapati hewa, hewa itakuwa imemzunguka vizuri tu, lakini moyo wake haudundi ili kusukuma damu kwenye mwili. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, moyo wake ukisimama, yaani kama hakuna mauzo, hakuna namna biashara itaweza kuendelea.

Mauzo ni kitu muhimu sana kwenye biashara na ndiyo kitu cha kwanza ambacho kila mfanyabiashara anapaswa kuweka juhudi zake zote kuhakikisha kinakwenda vizuri. Pamoja na umuhimu huu wa mauzo, utashangaa ni jinsi gani sehemu kubwa ya wafanyabiashara wadogo na wakati hawana uelewa kwenye mauzo yao. Wapo ambao hawajui kwa uhakika wanauza kiasi gani, iwe ni kwa siku, wiki, mwezi au mwaka. Na wapo wengi zaidi ambao hawana mpango wowote wa mauzo wanaofanyia kazi. Kwa kifupi wao wanasubiri mteja aje kuulizia na kama atataka atanunua, kama hataki basi. Pale ambapo wateja hawaji au wakija hawanunui, hawajisumbui, wanaishia tu kulalamika biashara ngumu, hali ya uchumi ni mbaya au msimu siyo mzuri. Hizo ni sababu ambazo kila mtu anazitoa na ni sababu zinazoficha uzembe ambao watu wengi wanao na unapelekea biashara zao kufa. Hawana mkakati wa mauzo wanaoufanyia kazi.
Iko hivi rafiki, tunaishi kwenye zama zenye fursa nyingi kwa kila mtu na hilo limeleta ushindani mkali sana. Biashara yoyote unayoifanya, wapo wengine pia ambao wanaifanya, hivyo mteja unayemlenga anawindwa na wengine wengi. Kama hiyo haitoshi, bado mteja siyo rahisi kukupa fedha yake. Kutoa fedha kunauma, hasa pale mteja anapojua akikupa fedha yake hawezi kuitumia tena kwenye kitu kingine. Unahitaji kuwa na mikakati sahihi ya kuwafanya wateja wawe tayari kununua kwako na siyo kwa wengine na wafurahie kabisa kutoa fedha zao na kununua badala ya kuwa wagumu kutoa fedha.
Hayo ndiyo unakwenda kujifunza kwa kina kwenye kitabu hiki cha CHUO CHA MAUZO. Chuo hiki kina masomo 60 ya kukupa uelewa, mikakati, mbinu na hatua za kuchukua ili uweze kufanya mauzo makubwa zaidi, bila ya kujali ni kitu gani unauza.
Suluhisho La Tatizo Lolote Kwenye Biashara.
Watu wengi huwa wanalalamikia matatizo mengi kwenye biashara zao. Huona kama biashara zao zimeshindikana kabisa kutokana na matatizo mengi ambayo yanaziandama. Lakini kuna suluhisho moja ambalo linaweza kutatua matatizo yote kwenye biashara. Na suluhisho hilo ni MAUZO.
Nitajie tatizo lolote kwenye biashara ambalo haliwezi kutatuliwa na mauzo zaidi. Faida ya biashara ni ndogo? Sawa, fanya mauzo zaidi na hapo kunakuwa na nafasi ya kutengeneza faida zaidi. Hakuna wasaidizi wazuri kwenye biashara? Sawa, fanya mauzo zaidi na utaweza kuajiri wasaidizi wazuri zaidi. Mtaji hautoshelezi kwenye biashara? Vizuri, fanya mauzo zaidi na utapata fursa za kukuza mtaji zaidi.
Kwa kifupi tunaweza kusema biashara yako ina tatizo moja tu, haifanyi mauzo ya kutosha. Tatizo la mauzo duni ndiyo chanzo cha matatizo mengi ambayo yanazikumba biashara na kupelekea kufa. Hivyo kuanzia sasa, jiambie wazi kabisa kwenye biashara una tatizo moja tu, MAUZO DUNI. Tatua tatizo hilo na biashara itakwenda vizuri.
SOMA; Jinsi Ya Kukuza Mauzo Mara Mbili Kwenye Biashara Yako.
Ustaarabu Pekee Kwenye Biashara Ni Kuuza.
Mauzo yamekuwa yanapewa mtazamo mbaya kwenye biashara na maisha kwa ujumla. Watu huwa wanaona kuwashawishi watu kununua ni kama kujipendekeza au kuwasumbua wengine. Kuna watu wapo kwenye biashara na wanajiona ni wastaarabu kwa sababu hawaweki juhudi kwenye kuwashawishi wateja wanunue. Wao wanachodhani ni wateja kama wanataka watanunua, kama hawataki hakuna haja ya kuwashawishi.
Rafiki, nikuambie wazi fikra za aina hiyo ndiyo zimekuwa kikwazo kwako kukuza biashara yako kwa viwango vikubwa. Kujiona ni mstaarabu kwa sababu huweki juhudi kuwashawishi wateja kununua ni kujidanganya.
Ustaarabu pekee kwenye biashara ni kuuza, kama watu wanashawishika kununua maana yake kuna thamani unatoa. Na kama watu hawashawishiki kununua biashara haiwezi kuendelea kuwepo, hata kama unajiona una ustaarabu kiasi gani.
Uza Au Utauzwa.
Kila mtu kwenye maisha anauza, kwenye kila dakika ya uhai wako, unauza au unauziwa. Kuanzia kwenye mahusiano, familia, kazi, biashara, siasa, dini kote mauzo ni kitu cha kwanza kinachofanyika.
Hivyo jua kama huuzi, basi unauzwa au unauziwa. Kama unamshawishi mteja anunue kitu na hakununua, kwa sababu yoyote ile anayokupa, jua amekuuzia. Amekuuzia sababu kwa nini kitu unachouza siyo muhimu zaidi kwake. Ungekuwa muuzaji mzuri kama ungeweza kumwonyesha kile unachouza ndiyo muhimu zaidi kwake kwa wakati huo.
Kupitia CHUO CHA MAUZO unakwenda kujifunza jinsi utakavyouza kwa wingi badala ya wewe kuuzwa au kuuziwa sababu zisizo na mashiko.
KARIBU UPATE NA KUSOMA KITABU CHA CHUO CHA MAUZO
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu uweze kupata na kusoma kitabu cha CHUO CHA MAUZO
Mauzo ni eneo linalogusa kila eneo la maisha, ndiyo maana nakuambia kitabu hiki kinaenda kuleta mapinduzi makubwa kwako. Kwani kitakujengea ushawishi mkubwa kwa wengine, uweze kuwafanya wakubaliane na wewe kwenye kile unachowataka wafanye.
Chuo hiki cha mauzo kina moduli 5 ambazo zimegawanyika kulingana na mchakato mzima wa mauzo unavyokuwa. Na pia kuna moduli moja ya ziada inayohusu maneno ya ushawishi, maneno ambayo ni muhimu sana kwenye mauzo.
Moduli ya kwanza ni maandalizi unayopaswa kuwa nayo kabla ya kukutana na mteja. Hapa unajifunza mambo yote muhimu unayopaswa kukamilisha kabla hujaenda kukutana na mteja unayemlenga. Bila kukamilisha hayo, hata ukikutana na mteja hutaweza kumuuzia.
Moduli ya pili ni njia za kutumia ili kuwafikia wateja sahihi kwako. Zama za kusubiri wateja waje kununua zimepitwa na wakati. Hizi ni zama za kuwafuata wateja walipo na kuwashawishi kununua. Kwenye moduli hii unajifunza njia nyingi za kuwafikia wateja unaowalenga.
Moduli ya tatu ni mambo ya kuzingatia pale unapokutana na wateja. Jinsi unavyokuwa na unavyofanya mbele ya mteja, kunaweza kujenga au kubomoa mauzo. Moduli hii inakufundisha tabia zote muhimu za kujijengea ili uweze kuwashawishi wateja kununua.
Moduli ya nne ni mchakato kamili wa mauzo. Hatua kwa hatua za jinsi ya kuyaendea mauzo, kuanzia kumpata mteja tarajiwa mpaka kumgeuza kuwa mteja kamili. Moduli hii ndiyo inakupa kiini kamili cha mauzo na kukuwezesha kukamilisha mauzo mengi.
Moduli ya tano ni kuwafuatilia wateja baada ya kukamilisha mauzo. Kumuuzia mteja mara moja ni hasara, kwa sababu unakuwa umeingia gharama nyingi kumpata. Unapaswa kuendelea kumuuzia mteja ndiyo upate faida. Moduli hii inakupa mbinu za kuendelea kuwafuatilia wateja ili waendelee kununua na hata kuwaleta wengine nao wanunue.
Moduli ya sita ambayo ni ya ziada, inahusu maneno ya ushawishi. Hayo ni maneno ambayo ukiyatumia kwenye mazungumzo yako na wengine, unakuwa na ushawishi mkubwa kwao kuchukua hatua. Kwenye mauzo, ushawishi ni muhimu, hivyo kuyajua na kuyatumia maneno hayo itakuwa na tija kubwa kwako kuongeza mauzo.
Kwenye kila moduli kuna masomo yanayoeleza kwa kina dhana, mbinu na mikakati mbalimbali ya kuujenga kuwa muuzaji bora kabisa kwenye kile unachouza. Kwa kubobea kwenye moduli hizi na masomo yake, utaweza kufanya mauzo makubwa na ya uhakika mara zote.
Kupata kitabu hiki cha CHUO CHA MAUZO, wasiliana na namba 0678 977 007 na utaweza kunufaika na maarifa haya yenye nguvu ya kukuza mauzo kwenye biashara yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekupitisha kwenye moduli na baadhi ya masomo ya kitabu hicho. Karibu uangalie ili uzidi kuona nguvu kubwa iliyo kwenye kitabu hicho. Wasiliana na 0678 977 007 kujipatia nakala yako ya kitabu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.