3451; Kujipata Kwenye Maisha.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi hudhani kujipata kwenye maisha ni kupata kila unachokuwa unakitaka.
Kwamba uwe na kila unachokuwa unataka ndiyo uwe umejipata.
Lakini hiyo siyo maana halisi ya kujipata kwenye maisha.
Kujipata kwenye maisha ni pale unapojua ni nini hasa unachokuwa unakitaka kwenye maisha yako na kupeleka rasilimali zako zote kwenye kitu hicho tu.
Unaamua kuachana na vitu vingine vyote na kukomaa na hicho ulichochagua.
Iko hivi rafiki, watu wengi ambao bado hawajajipata huwa wanahangaika na mambo mengi sana ya kufanya.
Kila inapokuja fursa mpya, unawakuta wapo ndani yake, wakiona hiyo ndiyo itabadili kabisa maisha yao.
Kwa kuwa hawajui ni nini hasa wanachokitaka, huwa wanajikuta wakihamia kwenye mambo mapya kila wakati.
Hali hiyo ya kuhamia kwenye mambo mapya kila wakati inawazuia kujenga ubobezi kwenye chochote wanachofanya.
Matokeo yake ni kubaki kuwa kawaida na kushindwa kufanikiwa.
Rafiki, huwa inachukua muda mrefu sana kujipata kwenye maisha.
Ni mpaka ujaribu jaribu vitu vingi ndiyo uweze kujua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako.
Ukishajua kwa uhakika kile unachokitaka kwenye maisha yako, unapaswa kupeleka rasilimali zako zote kwenye kufikia au kupata hicho unachotaka.
Usiruhusu usumbufu wowote ukutoe kwenye hicho unachokuwa unakitaka.
Ukishajipata, unatakiwa kupeleka juhudi zako zote kwenye kile ulichochagua na kupuuza vingine vyote.
Zitajitokeza fursa ambazo zinaonekana ni nzuri na sahihi zaidi kwako, lakini utapaswa kuzipuuza ili kupambania kile ulichochagua.
Zaidi watajitokeza watu ambao watakushauri nini hasa unachopaswa kutaka na kufanya.
Hao pia ni wa kupuuza kwa sababu zoezi la kujipata ni binafsi, hakuna mtu wa nje anayeweza kukuambia nini unachopaswa kutaka na kupata.
Ni kitu kinachotokana na msukumo unaokuwa ndani ya mtu.
Kama umeshajipata, umeshajua kile hasa unachotaka kwenye maisha yako, ambacho uko tayari kufia, fia hapo bila kuyumba.
Weka kila aina ya juhudi unayopaswa kuweka, fanya kila kinachohitajika kufanyika ili kupata yale unayotaka.
Mwisho wa yote kila mtu huwa anapata yale anayokuwa anayataka.
Kama bado hujajipata, acha kukimbizana na mambo ya nje na kaa uisikilize sauti yako ya ndani.
Jisikilize pale unapojiambia ni nini hasa unachotaka. Angalia yote unayokuwa unafanya, nini kinakuridhisha zaidi.
Tafakari kama ungekuwa unafanya kitu kimoja tu, kingekuwa kitu gani kati ya vingi unavyofanya.
Unapojisikiliza kwa makini, majibu yanakuja wazo kwako na hatimaye kuweza kujipata kwa uhakika.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe