3454; Uhakika wa mafanikio.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Licha ya kuwepo kwa maarifa na miongozi mingi kuhusu mafanikio, bado watu wanaofanikiwa kwa ukubwa ni wachache sana.
Siri zote za mafanikio zipo wazi kabisa na wengi tayari wanazijua.
Kila mtu anajua anapaswa kuwa na shughuli ya kumwingizia kipato cha uhakika.
Na kwenye kile kipato ahakikishe anatumia pungufu ili abaki na akiba.
Na kwa kila akina anapaswa kuiwekeza kwa busara ili iweze kukua na kuzalisha zaidi.
Kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ni kitu ambacho watu wamekuwa wanaambiwa tangu wakiwa wadogo, wakikatazwa wasicheze na watoto wenye tabia mbaya.
Kujifunza endelevu ni hitaji muhimu kwenye safari ya mafanikio, mtu kujua kwenye kila hatua kuna mengi ya kujifunza ambayo bado hajayajua.
Yote tuliyopitia hapo juu, ni misingi muhimu sana kwa mtu kuweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Lakini yote yanahitaji mtu ayafanyie kazi, kwa sababu hayawezi kufanya kazi yenyewe.
Kuzijua tu siri na misingi ya mafanikio haitakuwa na msaada kwako kama hutaweka kwenye vitendo.
Na hapo kwenye vitendo ndipo wengi wanapokwama kufanikiwa.
Kuna msingi na siri moja ya mafanikio, ambayo ina nguvu sana na sijaweka kwenye hiyo orodha hapo juu.
Siri hiyo ni KUCHELEWESHA RAHA.
Kama kuna kitu ambacho kimewazuia watu wengi wasifanikiwe, ni kupenda raha za haraka.
Watu wanataka mafanikio makubwa na kwa haraka, bila ya kuweka gharama yoyote kubwa.
Matokeo yake ni wanaishia kutumbukia kwenye mambo ambayo yanawaharibia sana.
Uwezo wa KUCHELEWESHA RAHA ndiyo unaowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaoshindwa wanakimbizana na raha za haraka, ambazo huwa hazidumu na zinawazuia kufanikiwa.
Wanaofanikiwa wanaweza kuepuka raha za haraka na kuwa na subira kwenye vitu vikubwa wanavyovitengeneza.
Ukishajiona unataka kupata vitu vikubwa kwa haraka na bila ya kulipa gharama kubwa, jua upo kwenye njia ya ambao hawataweza kufanikiwa.
Jifunze kuchelewesha raha, kuwa na subira, mambo yote makubwa na mazuri huwa yanahitaji muda na kazi.
Weka kazi kubwa na jipe muda wa kutosha.
Mafanikio yanakuwa ya uhakika kabisa kwako pale unapoifuata misingi hiyo sahihi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe