Rafiki yangu mpendwa,
Dharura huwa zinatokea kwenye maisha yetu na pale ambapo mtu anakuwa hajajipanga kwa dharura, huwa zinamrudisha nyuma sana.
Watu wengi wamenasa kwenye umasikini kwa sababu ya dharura mbalimbali wanazokutana nazo na kuwa hawajajipanga. Kwenye mipango yako ya kujenga utajiri na kufikia uhuru wa kifedha, unapaswa kuwa na mpango mzuri wa kukabiliana na dharura za maisha ili uweze kufikia lengo.
Kukosa mipango sahihi ya kukabiliana na dharura kumepelekea watu wengi kuingia kwenye madeni ambayo yanakuwa gereza la umasikini. Kwa kuwa madeni ya kutatua dharura huwa hayazalishi, yanamwingiza mtu kwenye gharama kubwa sana.

Ili kujizuia usirudishwe nyuma kifedha na dharura mbalimbali unazokutana nazo kwenye maisha, unapaswa kufuata hatua hizi tano za kupata pesa ya kutatua dharura kwenye maisha yako.
Hatua Ya Kwanza; Tumia Akiba Yako Ya Dharura.
Unapaswa kuwa na akina ya dharura na hiyo kuwa ndiyo hatua yako ya kwanza kutatua dharura unazokutana nazo kwenye maisha. Unapaswa pia kueleza mapema dharura ni nini ili ujizuie kutumia akiba hiyo ya dharura kiholela.
Kama umetumia akiba ya dharura na ikaisha au kama hukuwa na akiba ya dharura kabisa, nenda kwenye hatua ya pili.
Hatua Ya Pili; Uza Vitu Visivyozalisha Ulivyonavyo.
Kila mtu huwa ana vitu ambavyo havizalishi ambavyo anakuwa navyo. Hiyo ndiyo hatua ya pili ya kupata fedha kwa ajili ya kutatua dharura ambazo mtu anakutana nazo kwenye maisha. Kwa kuwa vitu tayari unavyo na havina uzalishaji wowote kwako, haina ubaya kuviuza ili kutatua dharura unazokutana nazo. Kabla hujaingia gharama kubwa zaidi, ni vyema kuachana na vitu visivyozalisha unavyokuwa navyo.
Ukishauza vitu visivyozalisha ulivyonavyo na bado dharura ipo au kama huna kabisa vitu visivyozalisha vya kuuza, nenda kwenye hatua ya tatu.
Hatua Ya Tatu; Omba Watu Wakusaidie.
Una ndugu, jamaa na marafiki mbalimbali ambao umekuwa unashirikiana nao kwenye maisha. Moja ya manufaa ya watu hao ni kusaidiana wakati wa shida na raha. Hivyo unapokuwa umekutana na dharura kubwa, nenda kwa watu wako wa karibu na waombe wakusaidie kuitatua kwa namna wanavyoweza. Inaweza kuwa kukuchangia fedha au kukupa rasilimali nyingine unazohitaji katika kutatua dharura hiyo.
Ukishaomba watu wa karibu msaada na bado dharura hujaweza kuitatua, nenda hatua ya nne.
Hatua Ya Nne; Uza Uwekezaji Ulionao.
Kuna uwekezaji mbalimbali unaokuwa umeufanya kwenye maisha yako kwa lengo la manufaa ya baadaye. Pale unapokutana na dharura ambayo umetumia rasilimali zako zote kuitatua na imeshindikana, unaweza kuuza uwekezaji wako kutatua dharura hiyo. Japo ulifanya uwekezaji kwa ajili ya kukuzalishia baadaye, kama dharura inaathiri uwezo wa wewe kunufaika na uwekezaji wako, ni vyema kuuza uwekezaji na kutatua dharura kwanza. Ukishaondokana na dharura unaweza kufanya uwekezaji mwingine.
Kama umeuza uwekezaji uliofanya ili kutatua dharura na bado dharura imeendelea kuwepo, nenda hatua ya tano.
Hatua Ya Tano; Chukua Mkopo.
Kama umeshafanya kila kinachowezekana kufanywa ili kupata fedha za kutatua changamoto na bado ipo, hatua ya mwisho ni kuchukua mkopo. Hii inapaswa kuwa hatua ya mwisho kabisa baada ya kuwa umefanyia kazi mengine yote. Hiyo ni kwa sababu mikopo huwa ina gharama kubwa, unapochukua unairudisha kwa riba, japo huitumii kwa kuzalisha. Hivyo pambana kwa njia nyingine zote na zote zikishindwa ndiyo uende kwenye mikopo.
Utaona hapo kuchukua mkopo ni njia ya mwisho kabisa kwenye mipango sahihi, wakati kwa wengi ndiyo njia yao ya kwanza. Ni muhimu sana uweke na kuzingatia mpango huu ili uweze kukabiliana na dharura bila ya kunasa kwenye umasikini.
Huenda unajiuliza vipi kama baada ya kuchukua mkopo bado dharura ipo? Hapo inakuwa tena siyo dharura, bali mwisho wa maisha. Yaani kama dharura haitaweza kutatuliwa na mkopo baada ya kupitia hizo hatua nyingine, itakuwa ndiyo hatima ya maisha yenyewe na mtu huna namna ya kufanya.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimezifafanua hatua hizo tano kwa kina na jinsi ya kuzifanyia kazi pale unapokuwa unapitia dharura. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili uvuke vyema dharura na ubaki imara.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.