3455; Ngozi Ngumu Ya Mafanikio.

Kutoka Mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kitu kinachofanya mafanikio yawashinde wengi ni ngozi ngumu inayohitajika ili mtu aweze kufanikiwa.

Mafanikio siyo lele mama, yanataka mtu uwe na ngozi ngumu sana.
Uweze kuvumilia mengi ya kuumiza utakayokutana nayo.

Ngozi ngumu inaanzia kwenye kazi unayopaswa kuweka.
Lazima uwe tayari kuweka kazi kuliko watu wengine wote.
Utahitajika kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana na kwa muda mrefu kuliko unavyotarajia.
Na mbaya zaidi matokeo ya kazi kubwa unayoweka unaweza usiyaone haraka kama ambavyo unakuwa unataka.

Ngozi ngumu inahitajika kwenye kuwa na ung’ang’anizi licha ya kuanguka na kushindwa. Kabla hujafanikiwa utashindwa sana.
Utashindwa mara nyingi mno.
Lakini hupaswi kukata tamaa na kuacha, badala yake unapaswa kuendelea.
Bila ngozi ngumu hutaweza kuendelea hasa baada ya kushindwa mara kadhaa.
Kila unapoanguka, unakuwa tayari kuinuka tena na kuendelea.

Ngozi ngumu inahitajika kwenye kuwapuuza wengine ambao wanakudharau, kukudhihaki na kukukatisha tamaa.
Hapa ndipo ndoto za watu wengi zimekuwa zinafia.
Mtu anakuwa na ndoto kubwa, kabla hata hajaanza kuzifanyia kazi anaambiwa haziwezekani.
Anaamua kujizima data na kuzifanyia kazi ndoto zake, anapokutana na kushindwa wanamwambia, tulikuambia.
Hapo inakuwa vigumu sana mtu kuendelea, kwa sababu ataona hao wapo sahihi kuliko yeye.
Unahitaji ngozi ngumu sana kuendelea licha ya kuambiwa haiwezekani na kushindwa.
Kwa kuziamini ndoto zako na kuzipambania bila kuacha, lazima utazifikia.

Kujenga ngozi ngumu ya mafanikio ni kujua kabisa kila ugumu utakaokutana nao kwenye safari yako.
Halafu kukataa kata kata kukatishwa tamaa na chochote kile.
Jitoe hasa kwamba lazima ufanikiwe au utakufa ukiwa unayapambania mafanikio yako.
Usiruhusu chochote kikurudishe nyuma.

Ni pale unapokataa kupokea chochote tofauti na unachotaka ndiyo dunia inakuwa haina namna bali kukupa hicho unachotaka.
Lakini kwanza lazima uwe na ngozi ngumu sana.

Je kwa kujitathmini wewe mwenyewe, una ngozi ngumu kiasi gani?

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe