3458; Tokomeza siku za sifuri.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Pale unapotaka kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kugeuza kile unachofanya kuwa tabia.
Na kitu kinakuwa tabia kwa kukijengea mazoea ya kukifanya kila siku bila kuacha.

Katika kujenga tabia, unapaswa kufanya kila siku bila kuacha, hata kama ni kidogo kabisa.
Yaani hupaswi kupoteza siku yoyote ile kwa kutokufanya kabisa.
Japokuwa siyo kila unachofanya kitakuwa na matokeo makubwa, lakini hakuna ulichofanya na kikawa ni upotevu kabisa.

Kila juhudi unayoweka huwa ina mchango fulani kwenye kuzalisha matokeo makubwa sana ya baadaye.
Wajibu wako mkubwa ni kutokomeza siku za sifuri.
Siku za sifuri ni zile ambazo hufanyi kabisa kile unachopaswa kufanya kila siku.

Licha ya sababu za nje kuonekana kweli ni kizuizi, wewe unapaswa kuhakikisha unaendelea kufanya kila siku bila kuacha hata siku moja.

Kwa kila unachopaswa kufanya kila siku bila kuacha unapaswa kukigawa kwenye hatua ndogo kabisa unazoweza kufanya kila siku bila kukwama.

Kwenye kujifunza ni kusoma angalau ukurasa mmoja tu kwa siku.
Kwenye akiba na uwekezaji ni kuweka pembeni ni Tsh elfu moja kila siku bila kuacha.
Kwenye afya ni kula kwa usahihi na kufanya mazoezi (kutembea) kila siku bila kuacha.
Kwenye kuandika ni kuandika ukurasa mmoja au sentensi moja kila siku bila kuacha.

Utaona msingi hapo ni kufanya kitu kwa udogo sana, kila siku bila kuacha.
Ni kila siku na siyo siku ambazo unajisikia au unaona ndiyo zinafaa.

Ipo nguvu kubwa sana ya kufanya kidogo kidogo kila siku bila kuacha.
Itumie nguvu hiyo kuweza kuleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yako.

Kwa kuwa mambo yote makubwa yanajengwa kwa kuchukua hatua ndogo ndogo na za msingi bila kuacha, hilo ndiyo linalopaswa kufanyika.

Tokomeza siku za sifuri kwenye maisha yako na utaweza kufanya makubwa sana ukianzia hapo ulipo sasa.
Kilicho muhimu zaidi ni kufanya kuliko hata nini unachofanya.
Jukumu la kwanza ni kukaa kwenye mchezo, kabla hata ya kwenda kwenye majukumu mengine yaliyopo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe