Rafiki,
Ipo wazi kwamba, kila mmoja kuna eneo pendwa analoenda mara nyingi zaidi kwa ajili ya mapumziko au sehemu ya burudani.

Anapokuwa katika eneo hilo, anakuwa hana mapingamizi mengi maana silaha anakuwa amezishusha chini. Inapotokea ukamfikia, uwezekano wa kumshawishi ni mkubwa maana, ni wachache wanaomfikia kwa njia hiyo.

Kwa hiyo, mkakati wako kufuatilia wateja wako unaangalia aina ya wateja ulionao na kufanya utafiti wa maeneo wanayokuwa wanaenda. Hapa chini nimeweka baadhi ya maeneno yanayowakutanisha wateja wengi;


Moja; Eneo la michezo.
Hili halipingiki, linawakutanisha watu wengi zaidi kwa wakati mmoja. Hii ni kwa sababu wanataka kupata burudani na kuungana na marafiki wengi.

Hivyo, unapohudhuria michezo mbalimbali unakutana na wateja hao huku ukiwasilisha biashara yako.

Mbili; Semina na mikutano ya biashara.
Hili ni eneo lingine muhimu linalowakusanya wateja wengi ndani ya muda mchache. Unachotakiwa kufanya ni kufuatilia posti zinazotolewa na waandaaji.

Waandaaji huwa wanaweka majina ya walimu na baadhi ya washiriki. Kupitia majina hayo unakuwa na nafasi ya kuwafikia na kuongea nao.

Tatu; Midahalo
Mfano, Mwanachi Communication Limited huwa wanaandaa midahalo kuhusu mada  tofauti. Hivyo, unapohudhuria midahalo hiyo unaongeza ujuzi na kukutana na wateja wengi wapya.

Nne; Mafunzo
Ukiachana na semina, kuna taasisi zinaandaa mafunzo kwa kipindi fulani. Washiriki wanaingia darasani kujifunza ili kujiongezea ufahamu.

Mfano,  Bank Of Tanzania academy mwisho wa mwezi uliopita na mwezi huu mwanzoni walitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakufunzi.

Mmoja wa washiriki ni Kocha Dr. Makirita Amani, baadhi ya mambo aliyoniambia, ni kukutana na watu wengi wapya  katika eneo la fedha.

Tano; Mbio za hisani
Inawezekana usilione kama lina uzito sana, lakini ni moja ya sehemu kukutana na wateja wapya pia.

Mbio hizi huwa zinaandaliwa na taasisi tofauti kwa lengo la kutimiza lengo fulani. Mfano Benk kama CRDB, NBC, Maendeleo na taasisi nyingi zimekuwa zinaandaa mbio hizi.

Unachofanya unafuatilia ratiba na kulipia, kisha kushiriki. Wakati unashiriki unajitahidi kwenda kimkakati ukichagua aina ya wateja unaohitaji.

SOMA;Maeneo Matatu Kufanyia Kazi Kwa Msimamo Wakati Wa Ufuatiliaji

Hatua za kuchukua leo; Fuatilia ratiba za wateja wako, ili kujua maeneo wanayopenda kwenda ili upate nafasi ya kuwafikia kwa urahisi.

Habari njema kuhusu hii ni kuwa, unapokutana nao katika maeneo yao ni rahisi kushawishika kuchukua hatua.

Je, ni eneo lipi wateja wako wanapendelea kwenda, ili uwafikie na kuwashirikisha biashara yako?

Wako Wa Daima

Lackius Robert

Mkufunzi Wa Mauzo na Mwandishi

0767702659/ mkufunzi@mauzo. tz.

Karibu tujifunze zaidi.