3461; Deni Lisilolipika.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inasema hujaishi kama hujawahi kumfanyia mtu kitu ambacho hawezi kukulipa.
Yaani maisha yako yanakuwa yamekamilika, kwa kuwa na maana kwa wengine, pale ambapo unakuwa umetoa mchango wa kipekee kwao.
Kuwafanyia watu wengine kitu chenye manufaa kwao na hawawezi kukulipa ndiyo kuishi maisha yenye maana.
Mahusiano mengi kwenye maisha huwa ni ya kimiamala, yaani mtu anafanya jambo fulani kwa kutegemea kulipwa kwa namna fulani.
Hakuna ubaya wowote kwenye hilo, kwa sababu maisha lazima yaende.
Na kama kila upande utanufaika, basi ni kitu kizuri.
Ila kuna ngazi ya juu zaidi ya hapo, ngazi ya kufanya ambacho mtu hawezi kukulipa.
Hawezi kukulipa kwa kufanya kama ulivyofanya na pia hawezi kukulipa kwa fedha.
Hiyo inamwacha na deni la milele, ambapo njia pekee ya kukulipa ni kukushukuru na kukuheshimu.
Uzuri ni kwamba kila mtu anayo fursa ya kutengeneza deni lisilolipika kwa wengine.
Ambacho mtu anapaswa kufanya ni kufanya kwa ubora sana kile ambacho amechagua kufanya.
Chochote unachofanya, ukachagua kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana na kujali maslahi ya wengine, lazima utaacha alama ya kipekee kabisa.
Iwe ni kazi, biashara, huduma au chochote, unapokazana kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora, unaacha alama isiyofutika.
Huhitaji akili nyingi, elimu kubwa au mamlaka makuu ndiyo ufanye hayo.
Badala yake unahitaji kuweka umakini na ubora kwenye hicho unachofanya sasa.
Kifanye kwa viwango vya juu sana, viwango ambavyo havijawahi kuwepo kabisa.
Wafanye watu waone kuna kitu wanakosa pale wewe unapokuwa haupo.
Kama ni siku hujaenda kazini au hujafungua biashara, watu wawe na kitu ambacho wanakikosa.
Imalize kila siku yako ukijua umeacha tabasamu kwenye uso wa mtu hata mmoja tu, kupitia yale unayofanya.
Na ukizikusanya hizo siku zikawa nyingi, ndiyo unajenga maisha ya mafanikio makubwa.
Ralph Waldo Emerson amewahi kusema; “Mafanikio ni kucheka sana na mara nyingi; Kuheshimiwa na watu wenye akili na kupendwa na watoto; Kukubalika na wakosoaji waaminifu na kuvumilia usaliti wa marafiki wa uongo; Kuthamini uzuri, kutafuta ubora kwa wengine: Kuiacha dunia ikiwa bora kuliko ulivyoikuta, iwe ni kw watoto wenye afya, kipande cha bustani au kukomboa hali ya kijamii; Kujua japo maisha ya mmoja yamepumua kwa urahisi kwa sababu wewe umeishi.”
Rafiki, orodha ni ndefu na imebeba kila kitu kuhusu mafanikio.
Ni wewe tu kuchagua kuyaishi hayo ili kunufaika na kuwanufaisha wengine.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe