Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya kwanza ambayo ni anza kwa kusifia.

Na kwenye kanuni ya kwanza tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Kazi ya uongozi ni kuwashawishi watu wengine kufanya vitu ambavyo wanaweza kuwa hawataki kuvifanya, lakini vina manufuu kwao.
Uongozi ni ushawishi, bila ushawishi unaishia kuwa wa mabavu.
Kama kiongozi kuna wakati utahitaji kutoa taarifa mbaya kwa wengine, labda ni mahali wamekosea au kufanya vibaya.
Ukiwakabili watu na kuwapa taarifa hizo mbaya moja kwa moja, hawatazipokea vizuri na watatafsiri hilo vibaya.

Njia sahihi ya kutoa taarifa za aina hiyo ni kuanza na kitu cha kusifia kwa mtu huyo.
Kama ni kazi anza kusifia yale maeneo ambayo ni mazuri. Na baada ya sifa ndiyo unaweza kueleza maeneo ambayo siyo mazuri.

Wewe kama muuzaji, unapaswa kuwasifia wateja wako. Kuwa kama daktari wa meno ambaye huwa anawachoma kwanza wagonjwa sindano ya ganzi kabla kuong’oa jino.
Ganzi inakuwa inapunguza maumivu unayopata wakati wa kung’olewa jino.

SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya pili ambayo ni usiende kwenye kosa moja kwa moja.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Mtu anapokuwa amekosea na unahitaji kumrekebisha, unapaswa kuwa makini kwenye kufanya hivyo.
Watu wengi huwa wanaanza kwa kusifia kile mtu ambacho mtu amefanya vizuri, kisha kwenda kwenye kile ambacho hajafanya vizuri.

Japokuwa mtu atakuwa ameipata sifa, lakini kuelezwa kile ambacho hajafanya vizuri bado kutamuumiza, na hilo litamfanya asiwe na tayari kukubaliana na wewe unayemkosoa.

Kama unataka kumkosoa mtu kwa namna ambayo atakubaliana na wewe, usiende kwenye kosa moja kwa moja.
Badala yake mwoneshe kuna eneo anaweza kuliboresha zaidi, lakini usilitaje kama kosa.

Kwa mfano, kama una mtoto ambaye hafanyi vizuri shuleni kutokana na kutokuzingatia masomo, katika kumrekebisha kama mzazi utapendelea kumwambia; muhula huu umejitahidi kukuza ufaulu LAKINI somo la hisabati bado hujafanya vizuri.
Ukiweka juhudi zaidi utafaulu kwenye somo hilo.

Kwa kumweleza hivyo, unakuwa umemsifia kwa ufaulu wake, kitu ambacho atajisikia vizuri, ila ulipoweka neno lakini na kisha kutaja kile aliposhindwa, inamfanya asahau kabisa kile alichosifia.

Njia sahihi ya kumrekebisha mtoto kwenye hali kama hiyo ni kumwambia; muhula huu umejitahidi kukuza ufaulu NA ukiendelea na juhudi hizi kwenye muhula ujao, utaweza kufanya vizuri zaidi kwenye somo la hisabati pia.

Baada ya kumsifia mtu, usitumie neno LAKINI kwenda kwenye kile ambacho amekosea, badala yake tumia neno NA kisha onesha jinsi gani anaweza kufanya vizuri zaidi.

Tunalitumiaje somo hili kwa wateja?tunapowasifia wateja wetu, tusiweke neno LAKINI badala yake tumia neno NA.

Kwa mfano, kama mteja wako unataka aongeze mauzo zaidi na kupata faida zaidi, unamsifia kwa mauzo anayofanya sasa na kumtaka aongeze juhudi ili apate mauzo zaidi.
Kwa mfano, hongera Juma kwa manunuzi mazuri unayoendelea kufanya na ukifanya manunuzi zaidi utapata faida zaidi na kupata zawadi yako ya mwaka.

Yafanye mauzo yako kuwa ya ushawishi zaidi bila kutumia mabavu.
Kama unataka kuwarekebisha watu, usiende moja kwa moja kwenye kosa hilo litapoteza ushawishi wako kwa wengine.

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504