3463; Kupoteana.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Licha ya mazingira ya mafanikio kuwa rahisi kwenye zama hizi kuliko kipindi cha nyuma, bado wanaofanikiwa ni wachache sana.
Hilo halitokani na mafanikio kuwa magumu, bali linatokana na watu kupoteana.
Kwenye zama tunazoishi sasa, watu wamepoteana.
Watu hawajitambui wao binafsi na nini wanachotaka.
Kuna sababu mbili za watu kupoteana kwenye zama hizi.
Moja ni kutokujisikiliza wao wenyewe. Kila mtu huwa ana sauti ya ndani yake inayomwambia nini anapaswa kufanya.
Wengi wamepuuza sauti hiyo na kujikuta hawajui nini hasa wanachotaka kwenye maisha yao.
Mbili ni kukosekana kwa tamaduni zinazowaongoza watu kwenye mambo ya kufanya.
Kwa kipindi kirefu, maisha ya wanadamu yamekuwa yanaongozwa na tamaduni walizonazo.
Tamaduni zinawafanya watu walazimike kufanya au kutokufanya vitu fulani.
Kumekuwa na hali ya ‘ukisasa’ kwenye zama hizi ambapo watu hawafuati tena vile ambavyo tamaduni zinawaongoza.
Kwa kukosa miongozo sahihi, kwao wenyewe na kwa tamaduni, watu wamekuwa wanajiendea kwa misukumo isiyo sahihi.
Moja ni wanaiga yale ambayo wengine wanafanya. Hapo wanafuata mkumbo, kitu ambacho kinawapoteza zaidi kwa sababu mambo wanayoiga hayaendani na wao.
Mbili ni wanapangiwa cha kufanya na watu wengine. Hapo wanatawaliwa na kutumika kuwanufaisha wengine, hivyo wanayolazimishwa kufanya yanakuwa hayana manufaa kwao bali kwa wengine.
Kupata mafanikio unayoyataka, anza kwa kusimama wewe kama wewe.
Ondokana na hali ya kupoteana kwa kujitambua wewe mwenyewe kupitia kujisikiliza.
Pia chagua utamaduni au mchakato utakaokuongoza kwenye mambo yote unayofanya ili usivurugwe na yale unayokutana nayo.
Kama hujui nini hasa unachotaka na kama hujijui wewe mwenyewe, utaishia kuwasindikiza na kutumika na wengine kuwajengea wao mafanikio.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe