Habari njema Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU.
Hii ni programu ya kujifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo ili kujenga utajiri na uhuru wa kifedha.
Kwenye somo lililopita tulijifunza jinsi tamaa ya kupata pesa kwa haraka inavyopelekea wengi kupoteza fedha.
Na kutoka kwenye mrejesho, wengi mmeshirikisha jinsi ambavyo mmewahi kupoteza fedha kwa tamaa ya kupata zaidi.
Inaumiza sana pale unapopoteza fedha, kwa sababu kama ungeiwekeza vizuri, ingezalisha faida.
Lakini kwa upande mwingine, kupoteza fedha kunaweza kuwa msukumo kwako kufanikiwa zaidi.
Pale unapopoteza fedha kwa sababu zozote zile, chukulia kama ni ada ambayo umeilipa. Wajibu wako ni kuhakikisha unatumia ada hiyo vizuri ili unufaike. Kutumia ada ni kujifunza kutokana na makosa uliyofanya, ili usiyarudie tena. Lakini pia kuwa na hasira kwenye makosa hayo na kusukumwa kuyarekebisha.
Kama utakosea na kupoteza fedha, halafu ukaja tena kurudia makosa hayo hayo kupoteza fedha, hapo unakuwa umelipa ada mara mbili.
Unakuwa hujifunzi kutokana na makosa na hivyo kuendelea kukugharimu sana.

Kwenye kitabu cha THINK AND GROW RICH, mwandishi Napoleon Hill ameshirikisha kisa cha kweli cha mtu aliyeitwa Darby.
Darby alipata habari ya machimbo mapya ya dhahabu na kwenda huko kwenye machimbo. Alifanya uchimbaji mdogo na kupata madini ya dhahabu.
Hilo lilimsukuma kufanya uwekezaji mkubwa zaidi ili apate dhahabu nyingi.
Alifanya uwekezaji huo na alipata dhahabu kiasi. Baada ya hapo hakupata tena dhahabu. Alichimba sana lakini hakupata dhahabu.
Baada ya muda kupita bila kupata dhahabu, alikata tamaa na kuamua kuuza machimbo yake na mashine kwa mtu mwingine.
Yule aliyenunua machimbo yale alitafuta wataalamu wa miamba wakapima. Alichimba futi tatu tu na akapata dhahabu nyingi kuliko aliyowahi kupata Darby.
Darby alipopata taarifa za jinsi alivyokata tamaa akiwa amekaribia ushindi, alitumia hiyo kama hasira kwenye kile alichoenda kufanya.
Alienda kuuza bima na kila alipoambiwa hapana alikataa kuipokea.
Alijiambia; “Nilikata tamaa futi tatu kufikia dhahabu, kamwe sitakata tamaa kwa sababu watu wamenijibu hapana ninapowataka wanunue bima.”
Msukumo huo ulimfanya Darby kupata mafanikio makubwa sana kwenye kuuza bima. Kwa hasira ya kushindwa kwenye dhahabu, aliweza kulipiza kwa kufanikiwa sana kwenye bima.
SOMA; Sheria Tano (05) Za Fedha Zitakazokusaidia Uwekeze Na Usipoteze Uwekezaji Wako Kwa Tamaa.
JINSI YA KUTOKULIPA ADA MARA MBILI KWENYE UWEKEZAJI.
Kwa haya tuliyojifunza hapa na ambayo tumeyapitia kwenye maisha, tunapaswa kuhakikisha hatulipi ada mara mbili kwenye uwekezaji.
Tunahakikisha hilo kwa kufanya yafuatayo;
1. Kama ulichelewa kuanza kuwekeza, umelipa ada kwa manufaa ambayo umeyakosa. Tumia hiyo kama hasira ya kuwekeza kwa kiasi kikubwa na kwa msimamo bila kuacha.
Chukua umri ulionao wakati unaanza uwekezaji utoe umri uliokuwa nao wakati unaanza kazi/biashara, hicho ndiyo kipindi umepoteza.
Kila wakati jiambie; “Nimepoteza miaka … ya uwekezaji kwa kuchelewa kuanza, kamwe sitaacha tena kuwekeza kwa kipindi chote cha maisha yangu.”
2. Kama umewahi kuwekeza ila ukatoa uwekezaji wako na kupeleka kwenye matumizi, umepoteza faida ambayo ingezalishwa na muda pekee. Hapo umelipa ada kwa kukosa manufaa ya riba mkusanyiko kwa kuiingilia pale ulipotoa.
Tumia hiyo kama hasira ya sasa kuwekeza bila kutoa ili unufaike na riba mkusanyiko ambayo inategemea muda zaidi.
Kokotoa kiasi cha uwekezaji ambacho umewahi kuwa nacho na ukakitoa kisha kokotoa faida ya asilimia 1 ambayo ungeweza kupata kila mwezi. Hiyo ndiyo ada uliyolipa.
Kila wakati jiambie; “Nimejinyima Tsh … kila mwezi kwa kuuza uwekezaji wangu, kamwe sitauza tena uwekezaji wangu, nitawekeza kwa msimamo bila kuacha au kutoa.”
3. Kama umewahi kupoteza fedha kwa kutapeliwa au kufanya uwekezaji ambao siyo sahihi, ni ada umelipa kwa hicho kiasi ulichopoteza. Jifunze kutokana na makosa uliyofanya ili usirudie tena kupoteza fedha. Pia pata hasira kwa fedha uliyopoteza na jisukume kuifidia ili unufaike.
Jumlisha kiasi chote cha fedha ambacho umeshapoteza kwa kutapeliwa na kuwekeza vibaya. Pata hasira na msukumo wa kufanya kwa usahihi kutokana na namba hiyo.
Kila wakati jiambie; “Nimepoteza Tsh ….. kwa kutapeliwa na/au kuwekeza vibaya, kamwe sitapoteza tena fedha kwa kutapeliwa au kuwekeza vibaya na nitalipa kiasi chote nilichopoteza kwa kukiwekeza.”
Kila mtu huwa anakosea kwa sababu kuna mengi tunakuwa hatuyajui. Lakini kurudia makosa yale yale ni kujitakia.
Usikubali kulipa ada mara mbili, kosea mara moja, pata funzo na litumie kuwa bora zaidi.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kujibu maswali yafuatayo;
1. Umeelewaje dhana ya “USILIPE ADA MARA MBILI”?
2. Umejifunza nini kwenye kisa cha Darby cha futi tatu kutoka kwenye dhahabu?
3. Kwenye maeneo matatu ambayo watu wanalipa ada kwenye uwekezaji, ni ada zipi ambayo wewe umeshalipa?
4. Umejifunza nini kwenye ada ulizolipa na unahakikishaje hulipi mara mbili?
5. Andika hapa kauli utakayokuwa unajiambia kila mara kuhusu ada uliyolipa na kuhakikisha hutailipa mara mbili. (Tumia mfano wa kauli za kujiambia zilizoshirikishwa kwenye somo.)
6. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya kushiriki somo hili kikamilifu.
NGUVU YA BUKU
Kila mtu anaweza kuwa tajiri.
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE | +255678977007 | https://bit.ly/makirita