Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya pili ambayo ni usiende kwenye kosa moja kwa moja.

Na kwenye kanuni ya kwanza tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;

Kama unataka kuwarekebisha watu, usiende moja kwa moja kwenye kosa hilo litapoteza ushawishi wako kwa wengine.

Kama unataka kumkosoa mtu kwa namna ambayo atakubaliana na wewe, usiende kwenye kosa moja kwa moja.
Badala yake mwoneshe kuna eneo anaweza kuliboresha zaidi, lakini usilitaje kama kosa.

Kwa mfano, kama una mtoto ambaye hafanyi vizuri shuleni kutokana na kutokuzingatia masomo, katika kumrekebisha kama mzazi utapendelea kumwambia; muhula huu umejitahidi kukuza ufaulu LAKINI somo la hisabati bado hujafanya vizuri.
Ukiweka juhudi zaidi utafaulu kwenye somo hilo.

Kwa kumweleza hivyo, unakuwa umemsifia kwa ufaulu wake, kitu ambacho atajisikia vizuri, ila ulipoweka neno lakini na kisha kutaja kile aliposhindwa, inamfanya asahau kabisa kile alichosifia.

Njia sahihi ya kumrekebisha mtoto kwenye hali kama hiyo ni kumwambia; muhula huu umejitahidi kukuza ufaulu NA ukiendelea na juhudi hizi kwenye muhula ujao, utaweza kufanya vizuri zaidi kwenye somo la hisabati pia.

SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Pili

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya tatu  ambayo ni ongelea makosa yako kabla ya kumkosoa mwingine.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Kabla hujamkosoa mtu kwenye kile ambacho amekosea na unataka arekebishe, elezea kwanza makosa yako kwenye eneo hilo.

Kwa kuanza na kuelezea makosa yako, inamfanya mtu aone anajitahidi na wewe humkosoi kumkomoa, bali unataka awe bora zaidi.

Kwa mfano, kama una msaidizi ambaye amekosea jukumu ulilompa, kabla hujamweleza  kosa lake, mweleze jinsi ambavyo wewe pia ulikuwa unakosea kwenye jukumu hilo kabla hujawa mzoefu.

Kwa njia hiyo, ataona una lengo la kumsaidia awe bora kama ulivyo wewe.

Utaitumiaje hii kanuni kwenye mauzo?

Kwa mfano, una mteja wako ambaye anakosea katika jambo fulani.
Labda anachukua vitu au bidhaa ambazo hazina faida kubwa na hazitoki kwa haraka.

Ukienda kumkosoa moja kwa moja kwamba wewe unanunua bidhaa ambazo hazitoki haraka na hazina faida kubwa huenda asikuelewe na ataona unamkosoa.
Kitu ambacho kitapunguza sana ushawishi kwako.

Ili uweze kumnasa kirahisi, tumia kanuni ya tatu ambayo ni ongelea makosa yako kabla ya kumkosoa mwingine.

Hapa utamwambia, mwanzoni ulikuwa unanunua vitu ambavyo havitoki kitu ambacho kilipelekea mauzo kuwa duni.

Mweleze namna ambavyo ulikuwa unakosea kwanza wewe mwenyewe kwenye eneo hilo.
Kwa kuanza na makosa yako, itamfanya mtu aone namna ya kubadilika yeye mwenyewe kwa kuongeza juhudi na kuwa bora.

Mwisho, kabla hujamkosoa mtu kwenye kile ambacho amekosea na unataka arekebishe, elezea kwanza makosa yako kwenye eneo hilo.
Kwa kuanza na makosa yako, inamfanya mtu aone anajitahidi na wewe humkosoi kumkomoa bali unataka awe bora zaidi.

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504