3469; Kinachowanufaisha.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Unaweza kuwa unauza bidhaa au huduma ambayo ni bora sana, lakini bado wateja unaowalenga wasikuelewe na kuwa tayari kununua.

Ni kitu ambacho kimekuwa kinawashangaza watu wengi, pale wanapokuwa na kitu chenye manufaa makubwa kwa wengine, lakini wengine hao wanashindwa kuelewa na kunufaika nacho.

Hali hiyo ndiyo imekuwa inaleta mgawanyiko mkubwa kati ya wenye kitu na wanaokihitaji kitu hicho.

Wenye kitu wanakuwa wanalalamika kwamba hawawapati wenye uhitaji wa kitu hicho.
Wakati huo huo wenye uhitaji wa kitu wanakuwa wanalalamika kwamba hawakipati kitu hicho.

Mgawanyiko huo mkubwa uliopo kati ya wenye kitu na wanaohitaji kitu hicho unatokana na kushindwa kuelewana kwenye lugha inayotumika.

Kitu kimoja ambacho kila anayeuza au kuwashawishi wengine anapaswa kufanya ni kuwaeleza wengine jinsi maisha yao yanaenda kuwa bora kupitia kitu husika.

Tukumbuke kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunachukua hatua kama kuna manufaa binafsi ambayo tunayapata.

Kwa mtu kuona jinsi maisha yake yanavyokwenda kuwa bora kwa kutumia bidhaa au huduma fulani, anashawishika zaidi kuwa na hiyo huduma au bidhaa.

Mara zote jikumbushe kwamba kile unachouza siyo kwa ajili yako, bali kwa ajili ya wale unaowalenga.
Waonyeshe jinsi ambavyo maisha yao yanakwenda kuwa bora zaidi ya vile yanavyokuwa kabla.

Ukiweza kuliwasilisha hilo vizuri, hakuna namna ambayo kuwashawishi wengine kutakuwa kugumu kwao.
Waonyeshe watu kile wanachoenda kunufaika nacho na watakusikiliza kwa makini na kuchukua hatua sahihi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe