3470; Tabia ya kulegeza msimamo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Msimamo ni kiungo muhimu kwenye kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
Hiyo ni kwa sababu matokeo yoyote makubwa yanapatikana baada ya mtu kufanya kitu kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha.
Ni sawa na kuchochea maji kutoka kwenye kisima. Kadiri unavyochochea, maji yanakuwa yanapanda. Lakini ukiacha tu kuchochea, maji yote yanarudi chini. Ukija kuchochea tena inabidi uanze upya.
Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wanajikuta wanaanza upya safari ya mafanikio kila wakati.
Ni kwa sababu ya kukosa msimamo wa kufanya kwa mwendelezo bila kuacha.
Kukosa msimamo huwa hakutokeo tu, bali ni tabia ambayo mtu anakuwa amejijengea. Na kitu kikishakuwa ni tabia, huwa ni ngumu kuvunja.
Tabia ya kulegeza msimamo huwa inaanzia kwenye upekee ambao mtu unauweka kwenye kile ambacho amepanga kufanya.
Yaani mtu anapanga nini atafanya, halafu anaruhusu baadhi ya vitu kuingilia mipango hiyo.
Huo ndiyo upekee ambao huwa unalegeza msimamo.
Kwa mfano ukipanga kusoma kitabu kila siku, ikitokea siku umetingwa sana ukasema hiyo ni ya kipekee hivyo hutasoma, unakuwa umelegeza msimamo wako kwenye usomaji.
Pale unapopanga kufanya kitu, halafu ukaruhusu sababu yoyote kuvuruga huo mpango ulioweka, unalegeza msimamo wako.
Matokeo yake huwa ni kuishia kutokufanya kabisa.
Njia pekee ya kujenga msimamo ni kufanya kama ulivyopanga bila kuacha.
Ukishapanga, fanya, bila ya kujali nini unakutana na nini.
Ni pale unapoweza kuvuka kila aina ya changamoto na vikwazo na ukafanya ndiyo unapata mafanikio kwa uhakika.
Panga kisha fanya kama ulivyopanga bila kuruhusu chochote kuingilia mipango yako. Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe