Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Hongereni wote kwa kuendelea kukaa kwenye mchakato wetu wa programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo, kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Kwa kutumia kikokotoo cha riba mkusanyiko, shilingi elfu 1 ikitengwa kila siku na kuwekezwa, kwa riba ya asilimia 12 kwa mwaka, haya ndiyo matokeo yanayopatikana;

Mwaka 1 inakuwa Tsh 380,475.09

Miaka 5 inakuwa Tsh 2,450,090.10

Miaka 10 inakuwa Tsh 6,901,160.68

Miaka 20 inakuwa Tsh 29,677,660.96

Miaka 30 inakuwa Tsh 104,848,923.98

Miaka 40 inakuwa Tsh 352,943,175.31

Miaka 50 inakuwa Tsh 1,171,750,191.00

Unajionea mwenyewe hapo maajabu ya kuchukua hatua ndogo ndogo kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha. Kinachohitajika zaidi ni muda kuliko hata kiasi kinachowekezwa.

Unaweza kusema miaka 30 au 50 ni mingi sana. Lakini ukizingatia umri wa watu kuishi sasa, ambapo wapo wanaoishi zaidi ya miaka 80, miaka 30 mpaka 50 siyo mingi. Mtu akianza uwekezaji akiwa na miaka 30, mpaka anafika miaka 60 anakuwa amewekeza kwa miaka 30. Hivyo kuwahi kuna faida yake kubwa.

Lakini hata kwa ambao wamechelewa kuanza, bado kufanya uwekezaji kwa msimamo kuna manufaa kwao. Kwani kuwekeza kwa msimamo bila kutoa wala kuacha kwa miaka 10 na kuendelea, kuna faida kubwa sana.

SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.

MIEZI SITA YA KWANZA YA NGUVU YA BUKU.

Tuliianza rasmi programu hii ya NGUVU YA BUKU tarehe 01/01/2024, mpango ukiwa ni kutenga pembeni elfu 1 kila siku na kuwekeza kwa miaka 10 bila kuacha wala kutoa.

Kama ilivyo safari yoyote ndefu, hatua ndogo ndogo ndiyo zinazokamilisha safari. Tumeweza kuimaliza miezi sita ya kwanza ya programu yetu ya nguvu ya buku.

Kwa miezi hiyo sita tumekuwa na wiki 26 ambapo kwa utaratibu wetu wa kuwekeza angalau elfu 7 kila wiki, uwekezaji wa chini kabisa ambao mtu unapaswa kuwa umefanya ni Tsh 182,000/= (26 X 7,000/=).

Ni wakati sasa wa kujifanyia tathmini kwa kuangalia kiwango ambacho umewekeza ukilinganisha na kiasi ambacho ulipaswa kuwa umewekeza.

Katika kufanya tathmini hiyo, fuata hatua hizi;

1. Omba taarifa yako ya uwekezaji kwa kutuma ujumbe wa barua pepe kwenda UTT AMIS. Kwenye ujumbe huo wa barua pepe eleza unaomba kutumiwa taarifa ya uwekezaji wako na weka namba yako ya akaunti ya uwekezaji ya UTT. Tuma kwenda barua pepe; uwekezaji@uttamis.co.tz

2. Kokotoa kiasi ambacho ulipaswa kuwa umekiwekeza kwa wiki 26 za nusu mwaka wa uwekezaji. Chukua lengo lako la uwekezaji kila wiki kisha zidisha mara 26. Kama ulipanga kuwekeza elfu 10 kila wiki, unapaswa kuwa umewekeza Tsh 260,000/=.

3. Pokea taarifa ya uwekezaji wako kutoka UTT na jumlisha uwekezaji wako kuanzia Januari 2024 mpaka Juni 2024.

4. Linganisha kiasi ulichopaswa kuwa umewekeza kutoka namba 2 na kiasi ambacho umewekeza kwa uhalisia kutoka namba 3.

5. Kama umewekeza sawa na mpango au zaidi, jipongeze, uko pazuri, endelea. Kama umewekeza chini ya mpango, jua tofauti kisha ifidie. Weka mpango wako wa kufidia kile kiasi ambacho kimepelea kutoka kwenye mpango wako.

Kamilisha mchakato huu wa tathmini ya nusu mwaka wa uwekezaji ili ukae kwenye njia sahihi kulingana na mpango tulionao.

MABORESHO KWENYE PROGRAMU YA NGUVU YA BUKU.

Katika kuhakikisha programu inaendelea kuwa bora na kuwasaidia watu wote wenye nia ya kujenga utajiri bila ya kumtenga yeyote, tunakwenda kuwa na maboresho madogo. Maboresho hayo ni kama ifuatavyo;

1. Utaratibu wa kutuma salio kila siku ya Ijumaa tunauondoa, badala yake salio litakuwa linatumwa kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi. Salio litaombwa kwa njia ya email kutoka UTT na kisha kutumwa kwenye namba ya wasimamizi wa programu. Salio halitawekwa tena kwenye kundi wazi. Tukumbuke lengo la kutuma salio ni kuwajibika ili usitoe uwekezaji wako kwa sababu zozote zile.

2. Masomo ya wiki itakuwa mara moja badala ya mara mbili kama sasa, somo litakuwa siku ya Ijumaa na kila mshiriki atapaswa kusoma na kushiriki mjadala wa somo.

3. Kupata nafasi kwenye programu ya UHURU WA KIFEDHA, ambapo unasimamiwa kwa karibu zaidi kwenye uwekezaji, itategemea ufanisi wako kwenye programu ya NGUVU YA BUKU. Ni kama umeweza kutekeleza vizuri utaratibu wa NGUVU YA BUKU ndiyo unaweza kupata nafasi kwenye UHURU WA KIFEDHA.

Taratibu nyingine za programu zitaendelea kama zilivyo, uwekezaji wa lazima kufanya na kutuma ushahidi ni siku ya Jumatatu, kiasi kisichopungua elfu 7. Unaweza kwenda zaidi ya hapo kadiri uwezavyo. Pia unaweza kuwekeza kila siku au mara kwa mara kadiri ya mpango wako na kutuma kwenye kundi kama sehemu ya kupata uwajibikaji.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Kwa wiki 26 za uwekezaji ambazo tumekuwa nazo, je umeweza kuwekeza wiki zote bila kuacha? Kama jibu ni hapana, nini kilikukwamisha na unahakikishaje hukwami tena kwenye huu mpango?
2. Kwa mpango wako wa kuwekeza kila wiki, kwa wiki 26 unapaswa kuwa umewekeza kiasi gani?

3. Kwa salio uliloomba UTT, kwa nusu mwaka umewekeza kiasi gani?

4. Kama kiasi halisi ulichowekeza ni tofauti na mpango uliokuwa nao, kokotoa tofauti na ahidi unakwendaje kuifidia.

5. Ni kitu gani umejifunza katika hiki kipindi cha miezi sita ya kwanza ya programu ya NGUVU YA BUKU?

6. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.