3473; Kupenda unachofanya.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kupenda unachofanya ni ushauri ambao umekuwa unatolewa sana kwenye safari ya mafanikio.
Kwa sababu ya ugumu wa safari yenyewe, imekuwa inashauriwa mtu ufanye kile unachopenda ili uweze kuendelea kukifanya licha ya kukutana na magumu na changamoto.
Lakini huu umekuwa ni ushauri ambao pia ni mtego, kwa sababu unachofanya kabla hujafanikiwa na utakachokuja kufanya baada ya kufanikiwa ni tofauti kabisa.
Iwe ni kwenye kazi au biashara, kabla hujafanikiwa wewe ndiye unayekuwa mtendaji mkuu wa majukumu husika.
Lakini ukishafanikiwa, kazi yako kubwa inakuwa ni kuwasimamia wengine kwenye utendaji wa majukumu husika.
Hapo kuna mambo mawili ya kuwa na tahadhari nayo.
Moja ni kupenda unachofanya inaweza kuwa kikwazo kwako kupata mafanikio makubwa.
Kwa sababu mafanikio yanakutaka ufike mahali na uache kufanya kile ulichoanza nacho, kwa kukipenda sana kutafanya usiwe tayari kukiacha.
Kwa kuwa unapenda kutekeleza majukumu husika, hata unapofanikiwa, bado unajikuta unarudi kufanya hayo majukumu ya chini, kitu kinachokukwamisha kushughulika na majukuku mapya ya mafanikio.
Mbili ni inapokuja kwenye mafanikio, penda zaidi mafanikio kuliko kupenda majukumu ambayo unafanya ili kufanikiwa.
Kwenye kilele cha mafanikio, majukumu yanafanana licha ya yale yanayopelekea kwenye mafanikio kutofautiana.
Unapoyapenda zaidi mafanikio kuliko kingine chochote, unakuwa tayari kuyapambania mafanikio kwa kila namna.
Wajibu wako mkuu ni kuhakikisha hatua kubwa zinapigwa, pambania zaidi hilo kuliko mengine yoyote.
Kwa chochote unachofanya sasa, jua kadiri unavyofanikiwa utazidi kukiacha na kufanya majukumu makubwa zaidi ya hilo.
Unapaswa kuwa tayari kuacha chochote unachofanya na kutekeleza majukumu makubwa zaidi.
Inapokuja kwenye kupenda, penda zaidi mafanikio makubwa kuliko majukumu husika yanayofanyika.
Jua kabisa utakapofanikiwa, majukumu yako yatabadilika, kuwa tayari kwa mabadiliko hayo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe