3474; Nini kinachokuzuia?

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Tayari unajua ni mafanikio gani unayoyataka kwenye maisha yako.
Na tayari unajua nini unapaswa kufanya ili kupata mafanikio unayoyataka.
Unajua pia jinsi ya kufanya hicho unachopaswa kufanya.

Jambo la kushangaza sana ni kwamba, pamoja na kujua yote hayo, bado hufanyi.
Ukianza kufanya ni kwa muda mfupi sana, baada ya hapo unaacha.
Swali ni nini kinachokuzuia usifanye? Nini hasa kinachokukwamisha kwenye utekelezaji wa mambo mazuri uliyopanga?

Kufikiria sana na kuchambua kupitiliza huwa inanpa mtu hali ya kupooza kwenye kuchukua hatua.
Mtu anaona mambo ya kufanya ni mengi sana na muda hana, hivyo anaghairisha.

Kufuata mkumbo wa wengine wengi ni sababu nyingine inayowakwakisha wengi.
Wengi huamini kile kinachofanywa na watu wengi ndiyo kitu sahihi zaidi.
Sasa kwa kuwa wengi hawapo kwenye safari ya mafanikio, huwa inakuwa vigumu kufanya mamgo ya tofauti.

Njia pekee ya kutoka kwenye mkwamo huo wa ufanyaji ni KUCHUKUA HATUA MARA MOJA BILA KUSITA NA KUFANYA KWA MWENDELEZO BILA KUACHA.

Ukishajua unachotaka, nini ufanye na vipi, hapo hapo chukua hatua.
Usifikirie sana, wala usichambue sana, wewe anza kufanya mara moja.

Na ukishaanza kufanya kitu, jiwekee sheria ya kutokuacha kukifanya hata itokee nini. Unaendelea kufanya kwa kuboresha na siyo kuacha.

Yote hayo yanakutaka usifikirie sana wala kutaka wengi wawe wanafanya ndiyo na wewe ufanye.
Yamiliki mafanikio yako na wajibika kwenye yote unayojihusisha nayo.
Hapo ndipo unaweza kufanya kwa msimamo bila kuacha na kwa muda mrefu.
Ukishaliweza hilo la kufanya bila kuacha, mafanikio yanakuwa ni swala la muda pekee.

Je wewe ni nini kimekuwa kinakukwamisha zaidi?

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe