3477; Usichukue ushauri wao.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanajitolea kukupa ushauri hata kama hujawaomba ushauri.
Yaani wewe unaweza kuchagua tu kuyaishi maisha yako kwa namna ambayo unaona inakufaa.
Halafu watu wakawa na ushauri mbalimbali kwenye hicho ulichochagua kufanya.

Wengi watakazana sana kukuonyesha kwamba wapo sahihi kwenye yale wanayokushauri.
Watakuwa wanataka ukubaliane na yale wanayokushauri.
Lakini kuna sharti moja tu la wewe kukubaliana na ushauri wao.

Sharti hilo ni kama maisha waliyonayo watu hao wanaokushauri ndiyo aina ya maisha unayotaka kuwa nayo wewe.
Yaani wao tayari wanayaishi maisha ya ndo yako, tayari wamefika kule unakotaka kufika.

Kama watu hawaishi yale maisha ambayo ndiyo unataka kuwa nayo, hupaswi kuchukua ushauri wowote ambao wanakupa.
Kwa sababu chochote ambacho watu wanakushauri, ndiyo utaishia kuwa kama wao.

Kwa bahati mbaya sana, wale ambao tayari wanayaishi maisha ya ndoto yako hawana muda wa kukushauri kwenye yale unayofanya, maana wametingwa sana na hayo wanayofanya.
Huku wale ambao wanaishi maisha ambayo huyataki, ndiyo huwa wana muda mwingi wa kukushauri ni kwa namna gani uyaishi maisha yako.

Hiyo ndiyo sababu kubwa kwa nini unapaswa kupuuza ushauri ambao watu wengi wanajitolea kukupa bila hata ya kuwaomba.
Kwa sababu ni ushauri usiokuwa sahihi kwako.

Na hata kama kuna kitu cha maana ambacho watu hao wanaweza kukushauri, unapaswa kuwa tayari unakijua.
Kama mtu ambaye hujamwomba ushauri anaweza kukuambia kitu na ukakiona ni bora kabisa, basi tatizo lako ni kubwa zaidi.
Kwa sehemu kubwa unakuwa hujui nini hasa unachotaka au unachopaswa kufanya ili kukipata.

Simamia kile unachoamini ni sahihi kulingana na aina ya maisha unayoyataka.
Na pale watu wanapojitolea kukushauri, wapuuze kama hawana maisha unayotaka kuwa nayo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe