3478; Fanya kama unalipwa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo mengi ambayo huwa tunapenda kuyafanya hata kama hakuna mtu anayetulipa kwa kufanya.

Moja ya mambo hayo ni kuwakosoa au kuwasahihisha wale wanaokosea.
Kwetu tunaona ni jambo sahihi kufanya, kwa kuona tunawasaidia wengine.

Lakini mapokeo ya hao tunaoona tunawasaidia huwa ni ya tofauti kabisa.
Wengi huwa hawafurahishwi na hatua hiyo yenye manufaa kwao tuliyochukua.

Hiyo ni kwa sababu baadhi ya wanaokosea wanajua kabisa kwamba wanakosea lakini bado wanafanya makosa hayo.
Kwa wewe kuwakosoa au kuwarekebisha wanakuona kama una kimbelembele na mambo yasiyokuhusu.

Na wengine wanabaki, wanakuwa hawajali sana juu ya kile wanachofanya. Hivyo hata kama wanakosea, ni kitu ambacho hawakipi uzito mkubwa wa kuboresha.
Kwa wewe kuwakosoa au kuwarekebisha wanakuona ulijihangaisha na mambo yasiyokuwa muhimu.

Kama hivi mambo ndivyo yalivyo, yaani watu hawapendi kukosolewa au kurekebishwa, tunapaswa kufanya nini?

Moja ni wakosoe na kuwarekebisha wale ambao wanawajibika kwako moja kwa moja.
Wale ambao hata kama hawataki, wanalazimika kukusikiliza ndiyo unapaswa kuhakikisha wanafanya kwa usahihi.

Mbili ni wakosoe na kuwarekebisha wale ambao wanakulipa kwa kufanya hivyo.
Wale ambao wanakulipa ili uwasaidie kupiga hatua, unalazimika kuwaeleza ukweli hata kama unawaumiza.
Kwa sababu huo ukweli ndiyo utakaowasaidia kupiga hatua wanazotaka kupiga.

Nje ya makundi hayo mawili, usijihangaishe na kuwakosoa na kuwasahihisha wengine.
Kwa sababu hakuna namna watafurahishwa na hilo.
Hata kama watakuonyesha wanafurahishwa, ndani yao hali huwa ni tofauti.

Ukifuata hili, utapunguza sana msongo kwenye maisha yako.
Utaridhika kuwaacha wengine wakifanya makosa bila ya kusumbuka nao.

Tayari una mengi ya kukuhangaisha kweye maisha yako. Usiongeze kujihangaisha na mambo ya watu ambao hawathamini wewe kufanya hivyo.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe