Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya 4 ambayo ni TOA MAPENDEKEZO BADALA YA MAAGIZO
Na kwenye kanuni hiyo ya NNE tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Badala ya kuwapa watu maagizo ya fanya hivi au fanya vile, wewe wape MAPENDEKEZO ya jinsi gani wanaweza kuboresha zaidi kile ambacho wanafanya.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Nne
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya TANO ambayo ni USIMKOSOE MTU MBELE YA WENGINE.
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Mtu anapokosea, hata kama ni kosa la wazi, usimkosoe mbele ya wengine. Badala yake muite mtu faragha na kisha mweleze jinsi anavyoweza kuboresha zaidi.
Hata kama hutamwambia mtu amekosea moja kwa moja, kufanya hivyo mbele ya wengine kutawaumiza. Ili usiwe na chuki au hasira na mtu, wakosoe watu faraghani au wakiwa peke yao. Kwenda kinyume na hapo ni kuibua chuki au hasira.

Tunapoteza vitu vingi vizuri tukiwa na tunawakosoa watu mbele ya wengine. Wakati mwingine tunashindwa kujizuia kwa sababu ya hasira tulizokuwa nazo baada ya kuwa mtu ametenda kosa fulani. Usiwe mtu wa makasiriko mbele ya wengine.
Jifunze kuwa mtu wa kujichelewesha kuchukua hatua pale tu unapokuwa na hisia za hasira.
Chukulia kwamba, hata kama mtu amekosea ni kwa sababu hajui, hivyo unapaswa kumfundisha tena kwa upendo. Kama umeshindwa kumsaidia kwa upendo, basi usimuumize. Unamuumiza kwa kumkosoa kitu ambacho kitapunguza ushawishi wako kwake kwenye kile unachotaka kumshawishi.
Hata kama umefanya kwa nia njema kabisa, mtu huyo atakasirika na kuchukia kwa kuwa unakuwa umemdhalilisha kwa wengine. Mpe mtu nafasi ya kutunza heshima yake kwa wengine kwa kumkosoa faraghani.
Wasifie watu hadharani lakini wakosoe faraghani. Kuwaambia watu wamekosea hata kama ni kweli huwa hata haisaidii kwa sababu sisi binadamu huwa hatufanyi maamuzi yetu kwa fikra, bali kwa hisia. Jifunze kuwaelewa wengine kabla ya kufanya maamuzi ya kuwakosoa.
Kwenye makala yake ya kurasa 3478, mwandishi kocha Dr. Makirita Amani anasema kwamba, wengi tunapenda kufanya mambo ambayo hata hakuna anayetulipa kwa kufanya. Na moja ya mambo hayo ni kuwakosoa au kuwasahihisha wale ambao wanakosea. Lakini, mapokeo ya hao tunaoona tunawasaidia huwa ni tofauti kabisa. Wengi huwa hawafurahishwi na hatua hiyo yenye manufaa kwao tuliyochukua.
Kama hivi mambo ndivyo yalivyo, yaani watu hawapendi kukosolewa au kurekebishwa, tunapaswa kufanya nini?
Moja, ni wakosoe na kuwarekebisha wale ambao wanawajibika kwako moja kwa moja. Wale ambao hata kama hawataki, wanalazimika kukusikiliza ndiyo unapaswa kuhakikisha wanafanya kwa usahihi.
Mbili ni wakosoe na kuwarekebisha wale ambao wanakulipa kwa kufanya hivyo. Wale ambao wanakulipa ili uwasaidie kupiga hatua, unalazimika kuwaeleza ukweli hata kama unawaumiza.
Kwa sababu huo ukweli utawasaidia kupiga hatua wanazotaka kupiga.
Nje ya makundi hayo mawili, usijihangaishe na kuwakosoa na kuwasahihisha wengine. Kwa sababu hakuna namna watafurahishwa na hilo.
Hata kama watakuonyesha wanafurahishwa, ndani yao hali huwa ni tofauti.
Wasaidie watu kuuona ukweli kwa kuwakosoa faraghani, usiwaambie wamekosea au hawako sahihi hawatakuelewa hata kama ulifanya kwa nia njema.
Kwenye tawasifu yake Benjamini Franklin anasema kwamba muige Yesu na Socrates (imitate Jesus and Socrates) kwa unyenyekevu (humility). Socrates yeye aliwahi kusema anachojua ni kwamba, hana anachojua. Licha ya kuwa mtu anayejua sana katika zama zake. Ili ujenge ushawishi na wengine kama muuzaji bora kuwahi kutokea, usiwakosoe wateja wako mbele ya watu wengine.
Wasifie watu hadharani kwenye yale mazuri ambayo umeyaona kwake na yanakusaidia kupata manufaa. Kwa kuwakosoa watu faraghani ni bora kuliko kuwasoa watu hadharani, kumbuka kuwasifia watu wako hadharani kwa mazuri waliyofanya na wakosoe faraghani.
Kumbuka kuwakosoa wale ambao wanakulipa au wanawajibika kwako moja kwa moja na nje ya hapo achana nayo kwa sababu wewe siyo kiranja wa dunia. Jali mambo yako au biashara yako ndiyo kitu muhimu zaidi.
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504