Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.
Kwenye maisha huwa hatupati kile tunachostahili, bali tunapata kile tunachoweza kuwashawishi wengine wakatupa kupitia majadiliano. Hivyo ili uweze kupata mafanikio makubwa kadiri ya unavyotaka kwenye maisha yako, unapaswa kuwa bora kwenye majadiliano.
Kama muuzaji, kazi yako kila siku inakutaka uwe vizuri sana kwenye majadiliano. Kwani wateja watakuwa wanakupa mapingamizi kila wakati. Bila ya kuwa vizuri kwenye majadiliano, utaishia kuuziwa na wateja badala ya wewe kuwauzia.
Kuwa vizuri kwenye majadiliano ndiyo kuna nguvu ya kukupa wewe yale yote unayotaka kwenye maisha yako. Na huyapati kwa kuwanyang’anya au kuwadhulumu wengine, bali kuwashawishi wao wenyewe wawe tayari kukupa.

Ili kuwa bora kwenye majadiliano na kupata yale yote unayoyataka, zingatia mambo haya ya msingi.
1. Jua unachotaka na upo tayari kutoa nini.
Hatua muhimu kwenye majadiliano ni wewe kujua unataka nini na ili kupata unachotaka upo tayari kutoa nini. Hapo ndipo mambo yote yanapoamuliwa. Kwa kujua wazi unachotaka na kuwa tayari kutoa ili kupata, inafungua milango mingi.
2. Jua upande wa pili unachotaka.
Kwa kuwa unachotaka kinatoka kwa wengine, jua wale wenye kile unachotaka wao wanataka nini. Bila kujua kile ambacho unaojadiliana nao wanataka, hamtaweza kuelewana, kila mtu atakuwa anaongea lugha yake. Lakini kwa kujua upande wa pili unataka nini, kisha kuuonyesha kwamba unaweza kupata hicho kinachotakiwa kupitia wewe, watashawishika.
3. Kuwa msikilizaji zaidi kuliko mwongeaji.
Kwenye majadiliano ya aina yoyote ile, anayeongea sana ndiye huwa anaishia kushindwa. Hiyo ni kwa sababu anayeongea sana huwa anaishia kutoa taarifa nyingi na kutoa fursa kwa upande wa pili kuweza kuzitumia kwa ushawishi. Kuwa msikilizaji zaidi na uliza maswali ili upande wa pili ujieleze na wewe upate njia nyingi za kushawishi.
4. Kuwa na machaguo mengi au hitajika zaidi.
Kwenye majadiliano ya aina yoyote ile, yule mwenye machaguo mengi au anayehitajika sana ndiye huwa anapata kile anachotaka. Hivyo mara zote hakikisha wewe una machaguo mengi kuliko upande wa pili, kwa kuwa na vitu ambavyo haviwezi kupatikana kwingine ila kwako. Pia jiweke kwa namna ambayo upande wa pili utakuwa unakuhitaji zaidi. Hayo yote yatawezekana kama utakuwa bora sana kwenye kile unachofanya.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupata Unachotaka…
5. Fikiria ushindi wa pande zote.
Pamoja na kwamba unataka kupata kile unachotaka, majadiliano siyo mwisho, hivyo hakikisha upande wa pili nao unapata kile ambacho walitaka. Kushiriki majadiliano ambayo kila upande unapata ushindi inakujengea sifa nzuri ya watu wengi zaidi kuwa tayari kushirikiana na wewe. Lakini kama kila majadiliano unashinda wewe huku pande nyingine zikipoteza, utakuwa na sifa mbaya na wengi kutokuwa tayari kushirikiana na wewe.
6. Kuwa tayari kuondoka.
Kwenye baadhi ya majadiliano, unapaswa kuwa tayari kuondoka kwenye meza ya majadiliano. Hapo unakuwa umekubali kutokukubaliana na kutokuendelea na majadiliano kwa sababu kile unachotaka hakiwezi kupatikana. Ukiwa na nguvu ya kuondoka kwenye majadiliano, inafanya upande mwingine kutafuta sababu ya kukuweka kwenye majadiliano hayo ili kwa pamoja kufikia maamuzi mazuri.
7. Endelea kujifunza na kuwa bora kwenye majadiliano.
Kwa kitu chochote unachotaka kuwa bora kwenye maisha, ni lazima uwe na utaratibu wa kujifunza endelevu. Unajifunza kwa nadharia na vitendo ili kuzidi kuwa bora kwenye majadiliano. Kwa kila majadiliano unayoshiriki, iwe umeshinda au kushindwa, jifunze na boresha zaidi wakati mwingine. Kwa maboresho hayo endelevu utaweza kuwa bora sana kwenye majadiliano na kupata yote unayoyataka.
Jua kwa kina kile unachofanya, kuwa na thamani kubwa sana unayoitoa kwa wengine na fikiria ushindi kwa pande zote. Hayo yatakufanya ukubalike zaidi na wale unaojadiliana nao. Lakini muhimu zaidi ni kuhakikisha una machaguo mengi zaidi na upo tayari kuondoka kwenye meza ya majadiliano, kitu kitakachofanya pande unazojadiliana nazo kutokuwa tayari kukupoteza. Hayo yote yatakuwezesha wewe kuwa bora kwenye majadiliano na kuweza kupata yale yote unayoyataka.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.