3485; Dunia ni yako.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri muda unavyokwenda, viwango vya ushindi vinashushwa kwa kasi kubwa sana.
Vitu ambavyo vilitaka mtu aweke juhudi kubwa sana huko nyuma, kwa sasa vinahitaji juhudi ndogo sana.
Maendeleo ya teknolojia yamerahisisha sana ufanyaji wa mambo mengi.
Hivyo ilitegemewa kwa uwepo wa teknolojia, watu wengi zaidi wawe wamefanikiwa.
Lakini cha kushangaza ni wanaofanikiwa wanazidi kuwa wachache.
Kadiri mafanikio yanavyokuwa rahisi, ndivyo wanaoyapata wanavyozidi kuwa wachache.
Matarajio yasiyo sahihi imekuwa ni sababu kubwa ya watu kushindwa kufanikiwa licha ya mazingira kuwa rahisi.
Wengi wanatarajia matokeo makubwa sana bila ya kuweka juhudi kubwa.
Wanadhani ujio wa teknolojia umeondoa hitaji la kuweka kazi.
Ukweli ni kwamba hakuna kinachoondoa hitaji la mtu kuweka kazi ili kufanikiwa.
Usumbufu wa fursa nyingi zinazoonekana kulipa vizuri ni sababu nyingine inayowakwamisha wengi kufanikiwa kwa ukubwa kwenye zama hizi.
Teknolojia zimefanya kila kitu kionekane rahisi kwa mtu yeyote kufanya na kufanikiwa.
Kuzikataa fursa zinazoonekana rahisi ili kuweka juhudi na unakini kwenye mafanikio makubwa unayojenga ni hitaji muhimu kwenye zama hizi.
Mtazamo wa matokeo makubwa ya muda mfupi umechochewa sana kwenye zama hizi.
Watu hawana tena subira, matokeo yakichelewa hawasubiri mpaka yapatikane, badala yake wanakimbilia kufanya vitu vingine kwa kutarajia matokeo ya haraka.
Kinachokuja kutokea ni mtu kuwa ameanza mambo mengi, lakini hakuna hata moja alilokamilisha.
Kwa haya tuliyoyaona hapa, tutakubaliaba kwamba kadiri mafanikio yanavyokuwa rahisi, ndivyo kuyapata kunakuwa kugumu.
Hivyo basi, ili mtu kujihakikishia ushindi mkubwa mara zote ni lazima awe tayari kuweka juhudi kubwa sana, aweke umakini kwa kusema hapana kwa fursa zinazoonekana ni nzuri na kuwa na subira kwenye matokeo.
Anayeyaweza hayo kwenye hizi zama, dunia inakuwa ni yake kwa ajili ya kuitumia vile mtu anavyokuwa anataka.
Usitafute urahisi kwenye safari ya mafanikio, hata kama mambo yanaonekana kurahisishwa sana.
Mafanikio makubwa yanataka juhudi za kipekee pia, kuwa tayari kuziweka hizo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe