Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Sababu yoyote inayoweza kuwaleta watu wengi sehemu moja au kuwafanya wajue kuhusu kitu fulani, ni njia nzuri ya kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafikia kwa wingi zaidi.
Moja ya njia ya kuwaleta watu wengi pamoja au kuwafikia ni kutumia kampeni maalumu.

Kampeni maalumu ni matukio yanayoandaliwa ambayo yanawavutia watu wengi na taarifa zake kusambaa kwa watu wengi. Matukio hayo huwa yanaandaliwa na biashara ili kuwafikia wateja wengi kwa taarifa kusambaa kwa wengi zaidi.
FAIDA ZA KAMPENI MAALUMU.
Kampeni maalumu huwa zina manufaa kwenye biashara ya kuwafikia wateja wapya tarajiwa na kuwakumbusha wa zamani. Baadhi ya faida za kampeni maalumu ni kama ifuatavyo;
1. Kuwafikia watu wengi kwa kipindi kifupi. Kipindi cha kampeni huwa ni rahisi kuwafikia watu wengi ndani ya kipindi kifupi.
2. Kutumia gharama ndogo kuwafikia watu wengi zaidi. Njia za kawaida za masoko na matangazo huwa zinaweza kuwa na gharama kubwa. Lakini njia ya kampeni maalumu gharama yake huwa ni ndogo ukilinganisha na watu waliofikiwa.
3. Watu kuambiana wao kwa wao na hivyo taarifa kusambaa kwa kasi kubwa. Kulingana na aina ya kampeni, watu huwa wanapeana taarifa wao kwa wao na hivyo kusambaa kwa kasi kubwa.
4. Kuwepo kwa hatua za uhakika za watu kuchukua. Njia nyingine za masoko na matangazo huwa zinawapa watu taarifa ambapo hatua wanaweza kuamua wao wenyewe. Lakini kampeni zinawapa watu hatua za kuchukua moja kwa moja.
5. Uhaba na ukomo kuwasukuma watu kuchukua hatua haraka. Kampeni huwa ni za muda fulani au kwa kiasi fulani. Hilo huwa linawasukuma watu kuchukua hatua ili wasipitwe na kampeni husika.
SOMA; Tumia Matukio Maalumu Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MPANGO WA KAMPENI MAALUMU.
Ili kampeni maalumu iweze kuwa na tija kwenye kuwafikia watu wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa wengi, mpango unapaswa kuwekwa vizuri. Katika kuweka mpango wa kampeni maalumu, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.
1. Kuandaa ofa ambayo haiwezi kukataliwa.
Kampeni huwa inaambatana na ofa ambayo wateja hawawezi kuikataa, kwa sababu hawawezi kuipata mahali pengine. Ofa hiyo ndiyo inawasukuma watu kuchukua hatua na hata kuwaambia wengine.
Ofa inayotolewa kwenye kampeni inaweza kuwa ya hasara kwenye biashara, lakini mauzo ya ziada yatakayofanyika kwa wateja waliopatikana kwenye kampeni yatafidia hasara hiyo.
Biashara inapaswa kuangalia ni kitu gani inaweza kutoa kwa wateja ambacho hawawezi kupata kwingine kisha kukitoa kama sehemu ya kampeni.
2. Kuwa na njia ya kukusanya taarifa za wateja.
Kama kampeni itaendeshwa kwa watu kuja na kupata ofa kisha kuondoka, itakuwa hasara kubwa kwenye biashara. Kwani watu huwa wanapenda sana ofa bila kujali anayetoa ofa anapata nini.
Kitu ambacho biashara inapaswa kubaki nacho kwenye kampeni maalumu ni taarifa za kutosha za wateja ili kuweza kuwafuatilia na kuwauzia zaidi. Kampeni maalumu inapoendeshwa kunapaswa kuwa na njia ya kukusanya taarifa za wote waliovutiwa na kampeni hiyo.
Taarifa muhimu ikiwa ni mawasiliano yao ambayo yatatumika kuendelea kuwafuatilia hata baada ya kampeni. Hata kama kampeni imekuwa ya hasara, hiyo inakuwa ndiyo gharama ya kupata taarifa za wateja, ambazo zikiendelea kutumiwa vizuri, watanunua kwa wingi.
3. Kuwafuatilia wateja baada ya kampeni.
Baada ya kampeni kuisha, wateja wote waliokuja kwa njia ya kampeni wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu na msimamo bila kuacha. Kwa sababu walinufaika na ofa iliyotolewa kwenye kampeni, huwa ni rahisi kuanza kuwafuatilia kujua wanaendeleaje.
Njia mbalimbali za kufuatilia zinapaswa kutumika kama kutembelea, kupiga simu na jumbe mbalimbali. Ufuatiliaji unapaswa kuanza mara moja baada ya kampeni ili wateja wasisahau kuhusu biashara. Hilo litafanya ufuatiliaji endelevu kuwa rahisi.
Katika kuhakikisha biashara inawafikia wateja wengi na kuwa na sababu za kuendelea kuwafuatilia bila ukomo, kampeni maalumu zinapaswa kuandaliwa na kuendeshwa kila baada ya muda fulani. Maandalizi bora yanapaswa kufanywa kabla ya kampeni ili iweze kuwafikia watu wengi na kukusanya taarifa za wateja wengi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.