3486; Kinachokuzuia siyo ulichokosa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Ukimuuliza mtu yeyote ambaye hajafanikiwa ni kitu gani kimemkwamisha, atakujibu haraka sana.
Atakuonyesha vitu ambavyo amekosa na jinsi vimemkwamisha kufanikiwa.
Mimi binafsi nakataa kukubaliana na hilo.
Nakataa kwamba kinachomzuia mtu ni kile alichokosa.
Nakataa kwa sababu kwa kila kitu ambacho mtu amekosa, kuna vitu vingine ambavyo anavyo kwa ziada.
Kama mtu akiweza kutumia vitu hivyo alivyonavyo vizuri, ataweza kufanya makubwa sana licha ya kukosa baadhi ya vile anavyohitaji.
Tuangalie mfano mzuri sana ambao kila mtu huwa anapenda kutumia kama sababu ya kutofanikiwa.
Kila ambaye hajafanikiwa atakuambia kikwazo kwake ni fedha.
Inaweza kuwa ni kweli kwamba mtu anakosa fedha za kufanya yale muhimu anayokuwa amepanga kufanya.
Lakini mtu huyo huyo kuna vitu anavyo kwa wingi, ambavyo amekuwa anavipoteza tu.
Mtu akiweza kugundua kile alichonacho kwa wingi na kukitumia vizuri, atapata mafanikio makubwa kadiri ys atakavyo.
Tukirudi kwenye mfano wa kukosa fedha ambapo kumekuwa kunahesabiwa kama sababu, wengi unakuta wana muda mwingi sana.
Ndiyo mtu anakuwa hana kiasi cha fedha anachotaka kuwa nacho ili aweze kufanya. Lakini mtu huyo huyo anakuwa na muda mwingi sana.
Kama mtu ataweza kutumia huo muda wake vizuri, anaweza kufidia fedha anazokosa na akafanya makubwa.
Hivyo tunaendelea kuona kwamba kinachomkwamisha watu siyo kile walichokosa, bali kushindwa kutumia vizuri mbadala wanaokuwa nao.
Ni kweli kabisa kwamba kuna vitu ambavyo umekosa kwenye kupata unachotaka.
Lakini ni kweli pia kwamba kuna mbadala wa hicho ulichokosa.
Kushindwa kwako kutumia mbadala ulionao ndiyo kunakukwamisha.
Unapokuwa umekwama, usiangalie ni nini umekosa, bali angalia unatumiaje mbadala wa ulichokosa.
Uzuri ni kwamba kwa chochote ulichokosa, mbadala wake upo.
Ujue mbadala na kuutumia vizuri ili uweze kufanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe