3487; Kasi kwenye mafanikio.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye kujenga mafanikio makubwa, kasi inahitajika.
Siyo tu kasi ya kawaida, bali kasi ambayo ni kubwa.

Muda ambao mtu anachukua kati ya kupanga na kuchukua hatua unaamua kiwango cha mafanikio ambacho mtu anaweza kupata.

Watu ambao wanachukua hatua mara moja baada ya kuamua na kupanga, huwa wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko ambao wanachelewa kuchukua hatua.

Ili kufanikiwa, lazima mtu awe wa kuchukua hatua kwa haraka na kasi.
Siyo tu kwenye mambo yanayohusisha mafanikio, bali kwenye mambo yote.

Hii inahusisha vitu vya kawaisa kama kutembea, unaweza kupima mafanikio ya mtu kwa namna anavyotembea.

Watu wasiofanikiwa huwa wanatembea taratibu na hawana mwelekeo. Ni kama tu wanazurura na hawaelewi ni wapi hasa wanapokwenda.

Watu wanaofanikiwa huwa wanatembea haraka na wana mwelekeo. Kwa kila mwendo walionao wanajua wapi wanaenda na wanaenda kufanya nini.

Kwa sababu muda ni muhimu kwao, hawapo tayari kuupoteza kwa jambo lolote lisilokuwa na tija kwao.

Utajua kama mtu anajali muda kwa kuangalia kasi aliyonayo kwenye mambo yote anayofanya.

Watu wenye kasi huwa wanajali muda na wanafanikiwa.

Anza kujijengea sifa hii kama huna, ongeza kasi kwenye kila unachofanya.

Anza kwa kufanya kitu kwa nusu ya muda ambao huwa unafanya kwa kawaida.

Kama huwa unakula kwa nusu saa, anza kula kwa robo saa.
Kama huwa unaenda eneo fulani kwa saa nzima, anza kwenda kwa nusu saa.

Kwa nusu ya muda, hakikisha unakamilisha yale ambayo umekuwa unayakamilisha kwa muda uliozoea sasa.

Hapo utakuwa umeongeza kasi kwenye ufanyaji wako.
Lakini pia unakuwa umepata muda wa ziada, ambao unaweza kuupeleka kwenye mambo muhimu ambayo umekuwa unakwama kuyafanya kwa sababu ya kukosa muda.

Kama umekuwa unataka kusoma vitabu ila unakosa muda, anza kwa kufanya vitu binafsi kwa nusu ya muda.
Kula chakula kwa nusu ya muda uliozoea, kisha hiyo nusu tumia kusoma.

Kama umekuwa unataka kuanzisha biashara lakini unakosa muda, anza kufanya majukumu yako ya sasa kwa nusu ya muda.
Kamilisha kazi zako kwa nusu ya muda uliozoea kisha hiyo nusu tumia kwenye biashara unayotaka kuanzisha.

Ukiongeza tu kasi yako ya ufanyaji, utaweza kufanya mengi na makubwa kwenye huo huo muda ulionao.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe