
Rafiki,
Karibu katika mwendelezo wa masomo yetu ya ufuatiliaji yenye lengo la kuifichua pesa ya mteja ili ije kwenye biashara.
Na leo tunajifunza namna gani tunaweza kutumia silaha ya upendo kuwashawishi wateja tunaofuatilia.
Karibu kila mtu duniani, kuna kitu anachopenda kutoka moyoni mwake. Kutokana na upendo alionao katika kitu hicho huwezi kumwambia chochote.
Inaweza kuwa ni upande wa mpira, muziki, magari, nguo, nyumba, vitabu, lugha, safari na vitu vingine.
Ili uweze kuelewana, kuenenda naye au kumshawishi mtu huyo njia ni moja. Ambayo ni kuwa upande wake.
Njia hii inashauriwa na wataalamu wa biashara na sababu ni kama zifuatazo;
Ufanano.
Sisi binadamu tunapenda kutoa au kushirikisha taarifa zetu kwa wale tunaofanana nao. Hata wahenga wanasema, ” ndege wanaofanana huruka pamoja”.
Kwa kila mteja unayezungumza naye jiulize, je, kuna namna ushawishi au mazungumzo yangu yanafanana na hitaji lake?
Usalama.
Mazingira ya sasa usalama wa watu umekuwa mdogo sana, sio kila mtu unaweza kumshikisha mambo yako. Lakini mtu anayeonekana kuwa karibu ni rahisi kumwelezea changamoto au jambo lolote unalohitaji au linalokusumbua ili kupata suluhisho.
Namna ya kumfanya mteja aone kama upo karibu naye;
Kumpatia nafasi ya kujielezea.
Kadiri siku zinavyokwenda mambo yanazidi kuwa mengi na nafasi ya mtu kujielezea vema na kusikilizwa ipangua.
Ili umfanye mteja awe karibu yako, lazima umsikilize vema. Muache aongee, baadaye mpe hatua zinazofuata.
Ufuatiliaji endelevu
Unapomfuatilia mteja kwa muda mrefu kuna namna anaona una nia njema naye.
Kuwa mshauri badala ya muuzaji.
Hii ni baada ya kumwelezea mteja manufaa anayoenda kupata kutokana na matumizi ya bidhaa zako, ikiwemo jinsi ya kupata faida, namna ya kuitumia au kuiuza.
Kumpongeza na kumsifia.
Hii inapofanyika kwa msimamo bila kuacha kwenye kila mazungumzo inakuwa na tija kwa sababu unafanya aone unamjali mteja wako.
Hatua Za kuchukua leo, kwa kila mteja unayezungumza naye hakikisha unazingatia mambo mawili matatu kama nilivyoelezea hapo juu.
Kuza Mauzo Kupitia Kushirikiana Na Wenzako Katika Uhudumiaji
Kumbuka, ushindani wa kibiashara ni mkubwa, wateja wanawindwa na wauzaji wengine. Hivyo, lazima tuwe na mbinu mbadala kuwafikia, kuwashawishi, kuwauzia, kuwafuatilia na kuwabakiza katika biashara zetu milele.
Wako Wa Daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo
0767702659 / mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi.