3489; Kamilisha mzunguko.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaocheza michezo ya fedha, wanajua umuhimu wa mzunguko kukamilika.
Yaani hata ukipokea zamu yako, mchezo haujaisha mpaka wa mwisho amepata.
Na wa mwisho akishapata, mchezo unaanza tena upya.

Kinachofanywa kwenye hiyo michezo ya fedha ndiyo kanuni kamili ya mafanikio.
Ambayo kila mtu akiifuata kama anavyozingatia hiyo michezo, lazima atafanikiwa.
Na akimaliza mchezo, yaani mafanikio, anachopaswa kufanya ni kurudia mchezo.

Mzunguko wa mafanikio una vituo saba.

Kituo cha kwanza KUAMUA nini hasa unachotaka. Huwezi kufanikiwa kama hujaamua nini unataka.
Lazima ueleze wazi kabisa kile unachotaka. Kama hujui unachotaka, huwezi kukipata.

Kituo cha pili ni KUJITOA kwa kile unachotaka. Hapa unaamua kwamba ni lazima utapata hicho unachotaka na hakuna namna nyingine. Unaachana na mengine yote ambayo hayana mchango kwenye kile unachotaka.
Bila ya kujitoa hasa, utazongwa na usumbufu mwingi sana ambao unakuwa kikwazo kwako.

Kituo cha tatu ni KUFANYA. Hapa unachukua hatua ya kufanya ili kupata kile unachotaka. Haijalishi unataka kitu kiasi gani, kama hutachukua hatua ya kufanya, hutaweza kukipata.
Na hata ikatokea bahati umepata unachotaka, kama siyo mfanyaji, utakipoteza.

Kituo cha nne ni KUSHINDWA. Hapa unapata matokeo ambayo ni tofauti kabisa na ulivyotarajia. Unakuwa umefanya vizuri kabisa, lakini matokeo yanakuja tofauti na matarajio.
Hiki kituo huwa ndiyo mwisho wa safari ya wengi.

Kitu cha tano ni KUFANYA. Haijalishi umeshindwa mara ngapi, unajifunza na kufanya kwa ubora zaidi. Ni lazima uendelee kufanya bila ya kuacha, hata kama umekutana na nini.
Wale wanaoweza kuendelea kufanya licha ya kupata matokeo tofauti na matarajio, huwa wamesogea karibu zaidi na mafanikio.

Kituo cha sita ni KUFANIKIWA. Hapa ndipo unapopata kile hasa unachotaka. Unakuwa umefika pale ulipokuwa unataka kufika.
Kwa wasiofanikiwa, husherekea kituo hiki kwa muda mrefu na kuishia kurudi nyuma.

Kituo cha saba ni KURUDIA. Hiki ni kituo ambacho wengi huwa hawajui hata kama kipo. Wanapofika wanapotaka, wanaona wameshamaliza kila kitu.
Wasichojua ni safari ya mafanikio huwa haina mwisho, mapambano ni kila siku ya uhai. Mwisho wa safari ya mafanikio ni kifo.
Hivyo unapopata kile ulichotaka, unapanga kingine kikubwa zaidi na kuianza upya safari ya mafanikio.
Unarudia vituo vyote hapo juu.

Kwa haya tunayoona hapa, unakuwa unahitaji vitu viwili kufanikiwa; kukamilisha mzunguko na kurudia baada ya kukamilisha.

Je wewe upo kwenye kituo gani kati ya hivyo saba? Shirikisha kwenye maoni hapo chini.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe