Rafiki,
Karibu tena katika mwendelezo wa masomo yetu ya program ya CHUO CHA MAUZO, yanayolenga kutujenga kuwa mauzaji bora kuwahi kutokea na kukuza mauzo yetu.
Leo tutajifunza namna nzuri ya kushughulika na wateja wasumbufu tunaokutana nao katika uhudumiaji, lengo ni kutowapoteza kabisa kabla hawajafanya manunuzi kidogo na kutusaidia kuokoa muda na gharama zetu.

Ni muda sasa umepita tukikatishwa tamaa na wateja wanaotudanganya na wanaotupa ahadi za huongo na kutupa furaha bandia.
Wakati mwingine mazungumzo yanaanza vema, na tunaamini watanunua, lakini bado wanatukwepa dakika za jioni.
Katika programu zetu tumekuwa tunaelekezana kuwa, namna bora ya kushughulika na wateja wa aina hii ni kuwa na mtazamo chanya juu yao kuwa sio wasumbufu, bali wanahitaji kuelekezwa vema.
Hapa chini kuna mambo machache ya kuzingatia;
Moja; Elewa mahitaji yao.
Huwezi kutatua tatizo kama bado hujalijua. Pia, elewa kwamba mteja ameacha sehemu zingine zote amekuja kwako, ikiwa na maana anahitaji huduma kwako japo anapata utata kwenye kuamua.
Na najua unaweza kusema mtu ananisumbua, ananipima au vyovyote, upo sawa. Lakini wajibu wako mkuu ni kumtenganisha mteja na fedha zake.
Hivyo elewa kwamba wateja wako ni watu ambao ni wazito kwenye kufanya maamuzi. Hivyo, tumia silaha ya kujua hitaji kuwashawishi.
Mbili; Chuja sana wateja wako.
Kitu kimoja ambacho kila muuzaji anapaswa kujua ni kwamba, siyo lazima ufanye kazi na kila mteja anayetaka huduma kwako. Maana wauzaji wengi wamejiweka kama sheria kwamba kila anayekuja lazima apate huduma.
Ukitoa huduma kwa kila anayekuja kwenye biashara yako utajikuta unapoteza muda kushughulika na wateja wasio sahihi.
Weka mchujo kwamba vigezo au aina hii ya wateja ndio ninaowataka. Usije fanana na muuza nguo mmoja aliyeangaika na mtu mwenye uhitaji wa maombi.
Tatu; Fanya ufuatiliaji kwa msimamo.
Ukiwa na wateja wengi ambao. unaoona ni wasumbufu ukiwawekea mpango mzuri wa kuwafuatilia kuna baadhi watanunua. Hata kama ni kiwango kidogo, hii itasaidia kuokoa muda na gharama zako.
Nne; Wagawanye katika makundi tofauti kulingana na mahitaji yao.
Faida ya kuwagawa katika makundi tofauti ni kuwafuatilia kwa nyakati tofauti. Leo unawasiliana na mteja wa kundi hili, kesho kundi jingine huku ukiendelea na ratiba zako zingine.
Tano; Waweke katikati ya ratiba yako.
Kama unafanya utembeleaji, aina hii ya wateja unaweza kuwafikia baada ya utembeleaji wa wateja wawili watatu.
Kama ni simu, unaweza kuwapigia baada ya simu kadhaa kuzipigia. Lengo ni kuondoa hali ya kuwa disappointed (kukatishwa tamaa).
Namna nzuri ya kutokuchoka kuwasiliana na wateja wasumbufu katika uhudumiaji ni kumchukulia kila mteja kuna pesa yako anayo na unapaswa kuichukua.
Tambua haupo peke yako kukutana na hali au wateja wa aina hiyo. Wauzaji wengi wanakutana nao na wanawasumbua, lakini baadaye wanawauzia.
Wakati ndio huu, kwenda kuwauzia wateja wako kwa msimamo bila kuwakatia tamaa.
Wako Wa Daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo.
0767702659 / mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi.